Tuesday, November 6, 2018

AJALI YAUA SITA MSATA BAGAMOYO.

 Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa, (katkati) akionesha Gari lililopata ajali, kushoto ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya kipolisi Chalinze Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Janeti Magomi.
 .............................................................

WATU sita kati yao akiwemo mtoto mchanga jinsia ya kike ,wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ,iliyotokea kijiji cha Msata, barabara kuu ya Segera /Chalinze mkoani Pwani. 

Akitoa taarifa za awali kuhusu ajali hiyo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Mzaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa, alisema ajali hiyo ,imetokea novemba 5, majira ya saa moja usiku baada ya gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster ikitokea Mkata kwenda Mbezi -Dar es salaam ,kuligonga kwa nyuma bila kuchukua tahadhari ,lori namba KBV 746C/ZE2861 FAW iliyokuwa imeegeshwa barabarani kutokana na kuharibika. 

Aidha alisema, dereva wa Toyota coaster iliyosababisha ajali ambae hajafahamika jina lake, alikimbia baada ya kutokea ajali. 

Kamanda Wankyo alisema, waliopoteza maisha ni wanaume watano wenye umri kati ya miaka 30-40 ambao majina yao bado kufahamika .
Alisema ,watu saba walipata majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya mili yao.

“Waliopata majeraha ni pamoja na wanaume wanne na wanawake watatu ambao wote wamepelekwa zahanati ya jeshi Kihangaiko -RTS na kituo cha afya Lugoba kwa matibabu zaidi “alisema Wankyo. 
 
Kamnada Wankyo alisema, miili ya marehemu imehifadhiwa hospital ya wilaya ya Bagamoyo kwa uchunguzi wa daktari. 

Alitaja chanzo cha ajali, ni uzembe wa dereva wa gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster kujaribu kulipita bila tahadhari gari jingine lililokuwa limeegeshwa baada ya kuharibika na kwamba wanaendelea kumsaka. 

Kutokana na ajali hiyo kamanda huyo alitoa wito kwa madereva, kutii sheria za usalama barabarani na kuacha tabia za kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi ili kuepuka ajali ambazo chanzo chake ni kukiuka sheria za usalama Barabarani.

Kamanda ACP. Wankyo alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya madereva wasiotii sheria za usalama Barabarani ili iwe fundisho kwa wengine. 

Kwa upande wa mashuhuda wa ajali hiyo akiwemo, mwenyekiti wa kitongoji cha Pugini, kijiji cha Msata Siasa James alisema hii ni ajali mbaya ambayo haijawahi kutokea eneo hilo. 

“Tulisikia mshindo, na kuona tukimbilie eneo la tukio ndipo tulipokuta gari ya abiria imelivaa lori kwa nyuma na kisha kukatika upande wa kondakta “alieleza. 

Nae Stephen Hinjo alieleza kwamba, gari ya abiria walikutana nayo ambapo ilipita hata dakika mbili hazijapita walisikia kishindo na kutahamaki waliona limekwenda kujikita nyuma ya lori lililokuwa limepaki pembeni mwa barabara. 

“Kufika eneo la tukio tulikuta abiria upande wa kondakta umebanwa huku vichwa viwili vikiwa vinaning’inia chini, wengine wamekatika mikono na shingo, ni ajali haijawahi tokea, “kikubwa tulichokifanya ni kuopoa miili na polisi walifika eneo la tukio “alifafanua Hinjo. 

No comments:

Post a Comment