Sunday, November 11, 2018

WAISLAMU WANAWAKE WASHAURIWA KUANZISHA VIWANDA

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya WAnawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) kutoka wilaya za mkoa wa Mwanza, wakati wa hafla ya kuwatambulisha Mwenyekiti na katibu mteule wa jumuiya hiyo jana, Amina Ali Masenza na Dotto Mangu.
………………….................

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

WANAWAKE wa dini ya Kiislamu mkoani Mwanza wameaswa kuanzisha viwanda vidogo na vikundi vya ujasiriamali vitakavyotoa ajira na kuwasaidia  kujikomboa na umaskini wa kipato wakiwemo Watanzania wengine.

Rai hiyo ilitolewa jana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke wakati akimtangaza mwenyekiti na katibu mteule wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) mkoani hapa.

Alisema akinamama wakianzisha viwanda vidogo watapata fursa ya kujikwamua na umaskini wa kipato lakini pia wakiwa na viwanda hivyo vitawasaidia na watanzania wengine maskini kupata ajira na hakutakuwa na ubaya wakishirikiana na wasio waislamu kujenga na kuanzisha viwanda.

Sheikh Kabeke alisema sera ya viwanda inalenga kuwafanya Watanzania kufikia uchumi wa kipato cha uchumi, hivyo haiwezekani wakafungiana wenyewe kwa wenyewe katika boksi na kuhoji, kuna ubaya gani kwa wanawake wa kiislamu kuanzisha viwanda.

 “Viwanda vidogo vya akina mama wakiwa navyo vitawasaidia na wengine masikini kujikomboa kiuchumi maana wapo watakaopata ajira hata kama ni vya kusindika nyanya,mananasi, mbogamboga na mazao mengine na hakuna ubaya kushirikiana na wasio waislamu,”

“Tunataka tuondokane nakubaguana huyu si mwislamu, huyu mkristo. Mbona damu tunayoongezwa hatuhoji , tunaishi kwenye nyumba na kusoma kwenye shule zisizo za waislamu.Hivyo kila mmoja wetu aimbe wimbo wa viwanda kuunga mkono serikali ya viwanda,”alisema Sheikh Kabeke.

Pia aliwashauri, kwa kuwa serikali imeondoa riba kwenye mikopo hiyo ya wanawake, vijana na walemavu, ni muda muafaka wa kuunda vikundi vya ujasiriamali na kuvisajili ili kuchangamkia fursa za mikopo ya fedha hizo zinazotolewa kwenye halmashauri za majiji,wilaya na miji.

Kaimu sheikh wa mkoa alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais John Magufuli kwa kutmiza miaka mitatu Ikulu kuwa uongozi wake ni makini kwa jinsi anavyosimamia rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wanyonge na kupinga ufisadi.

“ Rais Magufuli ni kiongozi wa mfano, tunampongeza kwa umakini na ujasiri pamoja na serikali yake.Amesimamia kwa umakini na umahiri wa hali ya juu rasilimali zilizokuwa zinaporwa na wajanja wachache,hana ubaguzi na BAKWATA katupatia msikiti na anawajali wananchi wanyonge,”alisema.

Aidha, alieleza kuwa waislamu wanahitaji maendeleo ya elimu dini,kisera na kiuchumi wakiwemo watu wazima na watoto lakini walikatishwa tama na baadhi ya watu waliwachangisha na fedha hizo hazikufanya kazi iliyokusudiwa hima iliwanufaisha wao kwa kujimilikisha miradi.

“Tunahitaji maendeleo, viongozi wachangie dini yao na kila baada ya miezi mitatu tutakutana kufanya tathmini ya kilichopatikana na kuamua kifanye kazi gani maana huko nyuma waislamu walikatishwa tama na wajanja kujinufaisha na michango yao,” kaimu sheikh huyo wa mkoa.

Kuhusu vitendo vya ushoga alidai vimetokana an kumomonyoka kwa maadili na utandawazi mambo yaliyotufikisha kwenye dhambi hiyo ingawa wapo watu wanaofanya vitendo hivyo kwa kulazimisha na umaskini wa kipato na kiakili.

Hivyo ili kuondokana na hali hiyo viongozi wa dini waliopo serikalini waungane na washirikiane kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili waislamu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watoto wa kiislamu kupata elimu bora ya dini.

No comments:

Post a Comment