Tuesday, November 13, 2018

MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI MKUBWA WA MAJI WA MWANGA, SAME NA KOROGWE.

Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akitoa maelezo kuhusu mradi mkubwa wa maji wa Mwanga, Same na Korogwe kwa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.Mradi huo utanufaisha zaidi ya wananchi 438,000.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Mwanga, Same na Korogwe. Kulia ni Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa, akifuatiwa na Mhe. Mathayo David na Mhe. Jumanne Magembe (Mb) Mbunge wa Mwanga.
........................................
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) leo wameshiriki hafla ya kuweka jiwe la msingi wa mradi mkubwa wa maji wa Mwanga, Same na Korogwe. Hafla hiyo imefanyika katika chanzo cha mradi huo wilayani Mwanga, katika mkoa wa Kilimanjaro.

Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akiongea kabla ya kuweka jiwe la msingi amewataka wananchi kuwa walinzi wa miradi ya maji kwasababu miradi hiyo inajengwa kwa ajili yao, hivyo wanawajibu wa kuitunza ili iwe indelevu.  Makamu wa Rais amefafanua kuwa vyanzo vya maji vinatakiwa kulindwa na kutunzwa ili miradi ya maji inayojengwa iwe indelevu na kutoa huduma ya uhakika kwa wananchi.

Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Maji Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wa vijiji 38 vinavyopitiwa na mradi huo kupata huduma ya majisafi na salama.

Waziri Mbarawa amesema kuwa mradi huo umegawanyika katika awamu mbili, ambapo hivi sasa utekelezaji upo awamu ya kwanza iliyogawanyika katika maeneno matatu na utagharimu kiasi cha shilingi milioni 336.4 na katika hatua ya kwanza mkandarasi  ameshalipwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 20 na ujenzi umefika asilimia 76 ikihusisha ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha maji, ikiwamo dakio la maji, 
mfumo wa kutibu maji pamoja na tanki. 

Ameongeza kuwa awamu ya pili yenye gharama ya kiasi cha Shilingi milioni 80.6 inahusu usambazaji maji kwenda Same kwa ujenzi wa bomba kubwa,  matanki mawili moja likiwa na uwezo wa lita za ujazo milioni 9 na jingine lita za ujazo milioni 7, na matanki madogo. Kazi hii hadi sasa imetekelezwa kwa asilimia 50 na mkandarasi ameshalipwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 18.

Waziri Mbarawa amesema awamu ya tatu ni usambazaji wa maji Mwanga  kwa gharama ya Shilingi milioni 106.89 na kuainisha kuwa awamu hii imechelewa kwasababu mkandarasi aliyepatikana awali hakuwa na viwango vinavyostahili.

Mradi wa maji wa Mwanga, Same na Korogwe unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi za kifedha kutoka nchi za Kiarabu ikiwemo Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi wa Afrika( BADEA), Mfuko wa Maendeleo wa Opec (OFID), Mfuko wa Maendelo wa Saudia (SFD), na Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (KFD).

No comments:

Post a Comment