Sunday, November 25, 2018

WAKAZI WA BAGAMOYO, DAR ES SALAAM KUPATA MAJI YA UHAKIKA- ENG. KALOBELO.

 Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo, (katikati) akifafanua jambo wakati alipotembelea Mradi wa ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji kata ya Magomeni wilayania Bagamoyo,  wa tatu kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi, Cyprian Luhemeja, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira kutoka wizara ya Maji ambae pia ni mjumbe wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Nadhifa Kemikimba.
....................................................

Wialaya ya Bagamoyo na Jiji la Dar es Salaam sasa kufaidika na huduma ya maji ya uhakika kutokana na mradi mkubwa unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na maji taka Dar es Salaam, (DAWASA) wilayani Bagamoyo.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo alipokuwa katika ziara ya kutembelea miradi ya upanuzi wa huduma ya maji inayotekelezwa na DAWASA.

Alisema kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya maji na DAWASA na utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Tenki la kuhifadhia maji linalojengwa kata ya Magomeni mjini Bagamoyo ni wazi sasa kero ya maji itakuwa historia kwa wakazi wa maeneo ya Bagamoyo na Dar es Salaam.

Mhandisi Kalobelo alisema kuwa, Tenki hilo la Bagamoyo lina ukubwa wa mita za ujazo 6000, ambalo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita ambapo litahudumia watu wengi zaidi na kuondoa shida ya maji.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kuomba huduma ya maji ya DAWASA ili kila mtu apate huduma hiyo ya maji.

Alisema lengo la serikali ni kuwaondolea adha wananchi katika swala la upatikanaji wa maji hivyo ni vyema wananchi walio karibu na miundombinu ya maji kuomba kusogezewa huduma hiyo majumbani mwao ili lengo la serikali lifikiwe.

Mhandisi Kalobelo, ameipongeza DAWASA kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi jambo ambalo linaleta matumaini kwa wananchi kuendelea kutumia huduma ya maji kutoka DAWASA.

Alisema kwa sasa ndani ya DAWASA kuna mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji kuwataka waendelee hivyo ili kufikia malengo.

Aliongeza kwa kusema kuwa, wizara peke yake haiwezi kutekeleza miradi hiyo bila ya kuwepo kwa mamlaka za maji hivyo uwepo wao (DAWASA) unaleta ufanisi pia katika kazi za wizara na kupelekea malalamiko kuhusu maji  kupungua.

Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya maji ameipongeza DAWASA pia kwa kuimarisha kitengo cha kupokea malalamiko kwani wanachukua hatua haraka mara tu wanapopata malalamiko kutoka kwa wateja au yale yanayotumwa kutoka wizarani.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa wizara ya maji alikuwa katika ziara ya kutembelea miradi ya upanuzi wa huduma ya maji inayotekelezwa na DAWASA miradi ambayo ni Ujenzi wa matenki na upanuzi wa mtandao.

Miradi hiyo itanufaisha Manispaa za Kinondoni na Ubungo na Halmashauri ya Bagamoyo.
 
Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo, akikagua ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji kata ya Magomeni wilayania Bagamoyo.
 
Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo, (wa tatu kushoto) akifafanua jambo wakati alipotembelea Mradi wa ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji kata ya Magomeni wilayania Bagamoyo,  wa pili  kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi, Cyprian Luhemeja, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira kutoka wizara ya Maji ambae pia ni mjumbe wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Nadhifa Kemikimba. 

Sehemu ya muonekano wa Tenki kubwa la kuhifadhia maji mjini Bagamoyo mradi unaoetekelezwa na DAWASA.

No comments:

Post a Comment