Mkuu wa wilaya Arusha mjini Gabriel
Daqarro akifungua wiki ya usomaji iliyofanyika kwenye maktaba ya mkoa Arusha
pembeni ni mkutubi mkuu wa maktaba hiyo Bi Rafiki Mvamba na kushoto ni Afisa
elimu Vielelezo Godfrey Augustino wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi mkuu
huyo wa wilaya picha zote na mahmoud ahmad arusha
..........................
Na Ahmed Mahmoud Arusha
Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro amewataka waalimu na
Afisa elimu kuhakikisha mpango wa KKK (LANES) unatiliwa mkazo sanjari na
kuhakikisha wanafunzi wanajua kusoma kuandika na kuhesabu ili kuleta matokeo
chanya na kufikia malengo ya serikali ya wananchi wote kujua kusoma.
Akiongea wakati akifungua wiki ya kusoma na stadi za kukuza
kusoma kuandika na kuhesabu (LANES) iliyofanyika katika Maktaba ya mkoa Dc
Daqarro amesema kuwa wajibu huo ni wetu sote kuanzia nyumbani hadi mashuleni
kuhakikisha kila moja wetu anatimiza wajibu wake.
Amesema kuwa wiki kama hiyo ni ya kujitathmini tumefika wapi na
tunaelekea wapi kama taifa kwa ajili ya kukuza uelewa wa vijana wetu kujua
kuhesabu kusoma na kuandika ili kuwa na taifa linalopiga hatua kwa wananchi
wake kujua kusoma.
“Taifa limejipanga kuondoa wananchi wasio jua kusoma na
kuandika ndio maana ilikaja na mkakati wa kkk hivyo kila mmoja wetu anawajibu
kuhakikisha tunafikia malengo ya mkakati huu”alisema Daqarro
Kwa Upande wake Afisa elimu vielelezo Godfrey Augustino amesema
kuwa wajibu wa wazazi ni kufuatilia maendeleo ya watoto wao na wao kama waalimu
watahakikisha kila kijana anayepata nafasi anajua kusoma kuandika na kuhesabu
lengo ni kuondoa vijana wanaomaliza elimu wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Amesema kuwa hatavumilia kuona wilaya hiyo ikiwa ina vijana
ambao hawajui kusoma wala kuandika na amejipanga kuhakikisha wanafikia malengo
yalioanza kuonekana kwenye ufaulu kwa wilaya kushika nafasi ya kwanza kitaifa
katika ufaulu wa Darasa la saba mwaka huu.
Awali mkutubi mkuu wa maktaba ya mkoa Rafiki Mvamba amesema kuwa
analishukuru shirika Kwa kufadhili wiki hiyo na kuwataka watanzania kupenda
kujisomea na kufuatilia watoto wao ili kujua kusoma na kuandika itakayopelekea
taifa kuwa na wananchi wenye elimu ya kuweza kufikia malengo endelevu.
Amesema kuwa mpango huo LANES wa wiki ya kusoma
ni kujitathmini na kuwafikia wanafunzi kujua uelewa wao katika kukuza stadi za
kusoma kuandika na kuhesabu kuanzia watoto wa awali hadi vyuo vikuu kupenda
kujisomea kwani elimu haina mwisho.
“sisi kama maktaba tumejipanga kuhakikisha wanafunzi wote
wanaofika hapa wanapata vitabu vyote wanavyohitaji sanjari na kuwapa nafasi na
kuwaongoza pale wanapohitaji ili lengo ya kuwa na taifa lenye watu wanaojua
kusoma na kuandika linafikiwa”alisema Mvamba.
Afisa elimu Vielelezo Godfrey
Augustino akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa wiki ya usomaji Lanes kabla ya
kumkaribusha mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro (Picha na Mahmoud Ahmad- Arusha)
Pichani juu na chini ni sehemu ya
wanafunzi wa shule sita za wilaya ya Arusha walioshiriki mashindano mbali mbali
ya kusoma kuandika na kuhesabu wanaoonekana pichani ni wanafunzi wa shule ya
msingi Mwangaza na sombetini wakifuatilia kwa makini matukio mbali mbali
yalioendelea kwenye hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment