Saturday, February 24, 2018

DC BAGAMOYO ATOA SIKU 3 WINDE (RAZABA)

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga,kihutubia wakuu wa idara katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo Tarehe 23 February 2018.

Na Athumani Shomari 
.....................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kufuatilia taarifa za watu wanaogawana viwanja katika shamba linalomilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) lililopo kijiji cha Winde kata ya Makulunge.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo Tarehe 22 Februry 2018 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kufuatia taarifa za kuwepo watu wanaogawana viwanja ndani ya shamba hilo bila ya kujali mipaka na umiliki halali walionao RAZABA.

Alimtaka mkurugenzi kumpa taarifa za kitaalamu kuhusu mipaka ya RAZABA ili kubaini ukubwa wa eneo lililovamiwa na kuangalia hatua za kuchukua ili kunusuru eneo hilo ambalo lipo chini ya umiliki wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar .

Alisema hatua za haraka zichukuliwe ili kusitisha zoezi linaloendelea katika eneo la RAZABA na kuwaepusha watu wasie kutapeliwa kwa kuuziwa au kugaiwa eneo linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Mkuu  huyo wa wilaaya aliwataka wataalamu wa Ardhi Halmashauri ya Bagamoyo kufanya kazi zao kwa weledi ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili ya kazi zao.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa wananchi wanaotaka Viwanja wilayani Bagamoyo kufika ofisi za Ardhi ili kupewa maelekezo yaliyokuwa sahihi juu ya wapi hakuna mgogoro wa kiumiliki ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwa kupewa eneo ambalo tayari lina umiliki wa mtu mwingine.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wananchi wa kijiji cha Winde waliwasilisha malalamiko yao mbele ya Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi ambapo walitaka mipaka ya RAZABA iwekwe wazi ili kutenganisha kati ya eneo la wananchi na RAZABA jambo ambalo tayari limeshafanyika.

KAULI YA CCM WILAYA YA BAGAMOYO NOVEMBA 18, 2017

Tarehe 18 Novemba 2017, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Abduli Rashidi Sharifu alisema Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Bagamoyo kinatambua uwepo wa kjiji cha Winde na kwamba hakijawahi kuvunjwa wala kuondolewa kwenye ramani ya Bagamoyo.

akizungumza katika Mkutano ulioitishwa katika kijiji cha Winde kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, Sharifu alisema Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) ina mipaka yake na wananchi wa winde wana mipaka yao hivyo kila mmoja anapaswa kuheshimu mipaka yake.

KAULI YA HALMASHAURI YA BAGAMOYO JUNI 22, 2016.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Aliy Aliy alipiga marufuku utoaji wa hati za ardhi ikiwemo hati za kimila, katika maeneo yanayopakana na ardhi iliyohifadhiwa kama vile Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) inayomilikiwa na wizara kilimo na maliasili Zanziba, na Ranchi ya ruvu iliyopo wilayani Bagamoyo ambayo iko chini ya umiliki wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Mwenyekiti huyo wa Halmashauri alitoa kauli hiyo Juni 22, 2016. katika Mkutano Mkuu Maalum wa kijiji cha Kidomole kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo na kuongeza kuwa Afisa aridhi atakaebainika kutoa hati ndani ya maeneo hayo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kusimamishwa kazi.

Kauli hiyo ya Mwenyekiti huyo ilikuja kufuatia taarifa za kuuzwa kwa baadhi ya maeneo ndani ya Ranchi hizo jambo ambalo ni kinyume na sheria kwakuwa kampuni zinazomiliki maeneo hayo bado hazijavuliwa umiliki wake.

MSIMAMO WA WANANCHI WA WINDE.
  Wananchi wa kitongoji cha RAZABA Kata ya Makurunge Halmashauri ya Bagamoyo wilaya ya Bagamoyo,wakionyesha mabango yao kudai Ardhi yao ambayo kwa sasa inamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) kwenye mkutano uliofanyika Tarehe 18 Novemba 2017, kitongoji cha RAZABA. ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdul Rashid Sharifu.

HISTORIA YA MGOGORO KWA UFUPI
Mgogoro  wa watu wa kijiji cha Winde na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) umedumu kwa zaidi ya miaka 40 sasa huku RAZABA ikidai kuchukua eneo hilo kwa kuwalipa fidia wananchi hao toka mwaka 1977 na wananchi wa kijiji cha Winde wakidai hawajawahi kulipwa fidia.

MSIMAMO WA RAZABA.
Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) inasema RAZABA imeanzishwa rasmi mwaka 1977 mwezi wa kumi na kwa makubaliano kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo jumla ya  heka 77,663 zilikabidhiwa kwa serikali ya mapinduzi Zanzibar chini ya wizara ya kilimo na maliasili kwa lengo la ufugaji wa Ng'ombe na kwamba wananchi wote walilipwa fidia toka wakati huo. 
Bango linaloonyesha kwamba eneo hilo linamilikiwa na Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) chini ya wizara ya kilimo na maliasili ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
Ramani ya eneo la Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA).

No comments:

Post a Comment