WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua huduma za
viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki na amewataka watu wote watakaopewa
vibali hivyo kutii sheria kwa kufanya shughuli ambazo wameelekezwa kwa mujibu
wa vibali vyao na si vinginevyo.
Amesema utoaji wa huduma hizo ni miongoni mwa
jitihada za Serikali katika kuvutia uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda
kwani hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na
kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba
26, 2028) wakati akizindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya
kielektroniki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini
Dar es Salaam
na kwamba hatua hiyo itasaidia kuondoa urasimu na ucheleweshwaji wa huduma
pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
Amesema Idara ya Uhamiaji inatarajia kuanza kutoa
huduma tajwa kwa raia wa kigeni muda wowote kuanzia sasa na kwa kupitia huduma
hiyo, raia wa kigeni wataweza kuomba vibali hivyo kwa njia ya kielektroniki
wakati wowote na mahali popote walipo.
Waziri Mkuu amesema watakaopewa vibali wanatakiwa
kufanya shughuli zao kwa mujibu wa vibali vyao kwa sababu kufanya shughuli
tofauti na ilivyoainishwa kwenye kibali ni kosa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni
za Uhamiaji.
Amesema matumizi ya mtandao katika utoaji wa
huduma za viza na vibali vya ukaazi ni hatua ya mfano, kwani inakwenda sambamba
na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na sera ya Serikali ya matumizi ya
TEHAMA katika shughuli za Serikali (e-government).
Amesema Serikali inatarajia kuwa, matumizi ya
mifumo hiyo itaongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuwa mteja ataweza
kulipia huduma hizo mwenyewe moja kwa moja pasipo kupitia kwa mawakala au mtu
yeyote.
“Natoa wito kwa Maafisa, Askari pamoja na
Watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inatunzwa
pamoja na kuendeleza miundombinu yote ya kiutendaji.”
Waziri Mkuu amesema kwa kuzingatia ahadi ya
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kuimarisha
utoaji wa huduma kwa wananchi na raia wa kigeni, Maafisa Uhamiaji wanatakiwa
kutoa huduma hiyo kwa wakati, weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Taratibu za Uhamiaji.
Amesema mfumo wa huduma hizo utaunganishwa na
mifumo mingine ya Serikali, ambayo inatoa huduma kwa wananchi na wageni kama
vile Mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara
na Leseni (BRELA), Idara ya Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) na Mfumo wa Malipo ya Serikali Kimtandao (GePG).
No comments:
Post a Comment