Sunday, December 18, 2022

HAKUNA MAENDELEO WALA AMANI BILA YA UHURU WA HABARI.-NAPE.

 No description available.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mnauye, amesema hakuna Maendeleo, hakuna amani na hakuna furaha katika jamii ikiwa hakuna uhuru wa habari katika jamii hiyo.

Waziri Nape amebainisha hayo wakati akifungua Kongamano la kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini lililofanyika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambalo limehudhuriwa na washiriki wasiopungua 1000 wa ndani na nje ya nchi.

Alisema uhuru wa habari ni muhimu katika maendeleo ya nchi kwani jamii inapaswa kupata habari za mambo mbalimbali ambazo serikali inatekeleza.

Alifafanua kuwa, ikiwa wananchi hawatapata habari ni wazi kuwa watakuwa hawaelewi mambo mengi yanayotekelezwa na serikali yao na hivyo kuwafanya kuwa na manung’uniko ambayo yataondoa furaha yao na kuwakosesha amani.

Aidha, Waziri Nape aliwapongeza wanahabari kwa kufanya kazi yao kwa weledi, juhudi na moyo wa kujituma kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zilizo sahihi na kwa wakati.

Alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini uhuru wa habari hali iliyopelekea Rais Dkt. Samia kuiagiza wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuandaa mkutano mkubwa wa wanahabari ili kuangalia mambo mbalimbali yanahusu habari hapa nchini.

Waziri huyo wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema kwa umuhimu huo, serikali imeandaa kongamano hilo ambalo lengo ni kujadili namna ya kuboresha sekta ya habari ambapo majadiliano yanatakiwa kutoka na maazimio yatakayotekelezwa.

Aliendelea kusema kuwa, uhuru wa habari unapaswa kulindwa na sheria na wala sio utashi wa mtu ili kuufanya uhuru wa habari uwe ni endelevu kwa kiongozi yeyote atakaekuwepo madarakani.

Aliwahakikishai wanahabari kuwa ifikapo januari 2023 muswada wa marekebisho ya sheria ya habari utawasilishwa bungeni ili kupitisha baadhi ya vingele vya sheria kwa lengo la kutoa uhuru wa habari.

No description available.

 

Saturday, December 17, 2022

BALILE ATAKA UHURU WA HABARI NCHINI ULINDWE KISHERIA

 No description available.

Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, licha ya kuwepo kwa uhuru wa habari nchini, ameomba uhuru huo ulindwe kisheria.

Akizungumza katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 leo tarehe 17 Desemba 2023 amesema, wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru uliopo lakini haujalindwa kisheria.

“Wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru wa habari uliopo nchini, tunaamini serikali italinda uhuru huu kisheria katika Mabadiliko ya Sheria ya Habari yajayo.

Kwenye mkutano huo Balile amesema, mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari yatafikishwa bungeni Januari 2022.

“Nimezungumza na Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kuhusu mjadala wa Sheria ya Huduma za Habari, amesema Januari (2022) mapendekezo yatafikishwa bungeni,” amesema.

Akizungumzia madeni ya vyombo vya habari katika serikali na taasisi zake, Balile amesema licha ya juhudi kufanywa, bado taasisi za serikali ikiwemo halmashauri hasijalipa madeni yao kwa vyombo vya habari.

“Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, madeni ambayo vyombo vya habari vinadai kwa serikali na taasisi zake ni Tsh. 7 bilioni.

“Ukijumuisha na deni la Gazeti la Daily News la serikali (Tsh. 11 Bilioni), jumla ya deni ni Tsh. 18 Bilioni na zaidi,” amesema.

“Halmashauri wana roho ngumu, hawajalipa mpaka leo licha ya kuandikiwa barua na TAMISEMI. Tunaomba mheshimiwa waziri (Nape) liwekee mguu chini, utusaidie,” amesema Balile.

Katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa habari, ni kuweka sheria itakayowalazimisha watangazaji kwenye vyombo vya habari kulipa fedha ndani ya miezi sita baada ya matangazo yao kuchapishwa.

Miongoni mwa adhabu iliyopendekezwa iwapo mtangazaji atashindwa kulipa, walau kifungo cha miezi Sita.

 No description available.

WADAU WA BIASHARA WATAKIWA KUJISAJILI UPYA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

 No description available.

Serikali imetoa rai kwa wadau wa biashara ya kaboni wahuishe miradi yao na kujisajili upya kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni kilichopo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro ili iendane na matakwa ya Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni.    

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo Dkt. Jafo amesema hayo wakati akitoa taarifa ya uzingatiaji na utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni leo Desemba 16, 2022 jijini Dodoma.

 

Amebainisha kuwa uzingatiaji na utekelezaji wa kanuni na mwongozo huo utasaidia kuboresha usimamizi mzuri wa miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta zote. Hivyo, amesema utekelezaji wa biashara ya kaboni utachangia kupunguza gesijoto zinazosababisha ongezeko la joto duniani na hatimae kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuchangia katika utunzaji endelevu ya mazingira na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

 

Waziri Jafo amesisitiza kuwa uzingatiaji na utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni ni jukumu la wadau wote, ikiwemo Wawekezaji wa Kimataifa na wanaotoka ndani ya nchi, Wizara za Kisekta, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.  

 

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika na hali hii inajidhihirisha kupitia matukio ya mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame na mafuriko.  

 

“Athari hizi za mabadiliko ya tabianchi zimeathiri sekta za kijamii na kiuchumi na maendeleo kama vile kilimo, utalii, nishati, maji, afya, mifugo na mifumo ikolojia ya bahari na ardhi, hivyo kuathiri ongezeko la pato la taifa.

 

Aidha, ukame wa muda mrefu na mafuriko yamechangia gharama kubwa za kiuchumi, kuathiri maendeleo na maisha ya jamii za vijijini na mijini,” alisema Dkt. Jafo.  

 

Aidha, amesema kanuni na mwongozo huo vimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na hivyo kupunguza athari za mazingir

 

Friday, December 2, 2022

TaSUBa YAPONGEZWA KWA USIMAMIZI MZURI WA RASILIMALI FEDHA PAMOJA NA KUWEKA HISTORIA YA UDAHILI MKUBWA

 No description available.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu Desemba Mosi, kulia kwake ni Mkuu wa TaSUBa, Dkt. Herbert Makoye.

........................................

Na Mwandishi Wetu Bagamoyo

 

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Sanaa na utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa usimamizi mzuri wa fedha zinazoletwa katika taasisi hiyo kwa kuzitumia vyema kuendana na mahitaji ya taasisi ili kuifanya taasisi kufikia malengo yake.

 

Mbali na hilo, pia ameipongeza TaSUBa kwa ongezeko kubwa la udahili wa Wanafunzi katika chuo hicho hata kufikia hatua ya kuweka historia ya kudahili idadi kubwa ya wanafunzi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

 

Naibu Waziri Gekul ametoa pongezi hizo leo Desemba Mosi, 2022 akiwa ni mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya TaSUBa yaliyofanyika katika kampasi ya TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani na kusisitiza kuwa, taaluma ya utamaduni na sanaa inayotolewa chuoni hapo ni taaluma muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote duniani.

 

Kufuatia hilo naibu waziri Gekul amebainisha kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona wazi umuhimu wa taaluma hiyo na hivyo kuanzisha sera maalum kusimamia.

 

“Taaluma inayotolewa hapa chuoni ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii yoyote duniani, ndio maana serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, imeweka sera ya kusimamia sanaa na utamaduni kwa ujumla wake” alisema Naibu Waziri Gekul na kuongeza.

 

“TaSUBa ni taasisi ya pekee nchini kwetu na ukanda wa Afrika Mashariki inayotoa mafunzo ya sanaa kwa ngazi ya stashahada na astashahada hivyo basi kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha taaluma hii ili iendane na mazingira ya sasa ya utandawazi”

 

Naibu Waziri huyo ameutaka uongozi wa TaSUBa kuendeleza ubunifu zaidi kwa kuanzisha kozi ambazo zitawavutia watu wengi kujiunga na chuo hicho.

 

Naye Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye amesema kuwa, kwa miaka mitatu mfululizo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi chuoni hapo na hiyo ni kutokana na jitihada mbalimbali zilizochuliwa na serikali ya awamu ya sita, wadau pamoja na wao wenyewe kama taasisi.

 

Dkt. Makoye amezitaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uamuzi wa serikali kuwapangia wahitimu wa kidato cha nne moja kwa moja kujiunga na chuo hicho pamoja na uhamishaji wa kila siku unaofanywa na TaSUBa pamoja na wadau wengine katika kukitangaza chuo hiko.

 

Dkt. Makoye ameongeza kuwa, kwa mwaka huu wa masomo pekee wameweka kudahili wanafunzi 835 kutoka kwenye lengo la kudahili wanafunzi 700 na hivyo kuweka historia ya udahili mkubwa chuoni hapo.

 

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la wahitimu na kwa mwaka huu tuna wahitimu 217. Aidha, mwaka huu wa masomo 2022 /2023 tumeweza kudahili wanafunzi 835, lengo lilikuwa ni kudahili wanafunzi 700. Hii ni rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa TaSUBa” alisema Dkt. Makoye.

 

Kuhusu maono ya TaSUBa kumiliki kituo chake cha redio na televisheni kwa ajili ya kuwezesha wepesi wa utendaji kazi na mazingira wezeshi ya ufundishaji na kujifunza Dkt. Makoye amesema.

 

“Endapo tukipata fedha ambazo tuliziomba katika mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ununuzi wa vifaa vya kuanzisha na kusimika mitambo ya televisheni na redio, basi TaSUBa itakwenda kumiliki televisheni na redio yake”

 

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TaSUBa, Bw. George Yambesi ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika taasisi hiyo unalenga kupanua wigo zaidi wa vijana wa Kitanzania kupata mafunzo katika tasnia za sanaa na utamaduni.

 

Aidha, Bw. Yambesi ametumia fursa hiyo, kuishukuru serikali kwa uwezeshaji mkubwa unaoendelea kutolewa kwa TaSUBa, uwezeshaji ambao umeleta matokeo chanya katika taasisi hiyo ikiwemo kufanikisha uboreshaji wa miundombinu kujifunzia na kufundishia kinyume na iliyokuwa awali ambao pia ameendelea kuisihi serikali kuendelea na uwezeshaji huo ili malengo mahususi yaliyowekwa na TaSUBa yaweze kutimiza na taasisi hiyo iweze kuleta tija kw mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.

 

Nao wahitimu wa chuo hicho kupitia risala yao iliyosomwa na Richard Julius Mtambo wameeleza kuwa changamoto kubwa mbili zinazowakabili chuoni hapo ni ukosefu wa basi la taasisi na hivyo kupata adha kubwa pale wanapopanga kufanya safari za kimasomo, utalii, maonesho, mafunzo, mashindano na za kikazi.

 

Changamoto nyingine ni ukosefu wa uzio kwenye taasisi hiyo jambo ambalo linahatarisha usalama, kuwa kichocheo cha wizi na kupelekea kukosekana kwa faragha.

 

Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni kituo chenye ubora uliotukuka Afrika Mashariki katika kutoa mafunzo ya sanaa za maonesho na ufundi ambapo majukumu yake makubwa ni kuhudumia mahitaji ya nchi washirika wa jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutunza, kuhamasisha na kuendeleza sanaa za maonyesho na ufundi ikiwa na majukumu makuu matatu ambayo ni utoa mafunzo,


kufanya utafiti katika masuala yanayohusu sanaa na utamaduni pamoja na kutoa ushauri katika masuala yanayohusu sanaa na utamaduni.

 No description available.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akitoa hotuba yake.

No description available.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Bw. George Yambesi akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya taasisi hiyo ambayo yamefanyika Desemba Mosi, 2022 katika kampasi ya TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani. Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul 

No description available.

Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye akitoa hotuba yake wakati wa mahafali ya 33 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Desemba Mosi, 2022 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

No description available.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo Desemba Mosi, 2022.

No description available.

Wahitimu wa ngazi za stashahada na astashahada katika tasnia za sanaa na utamaduni.