Thursday, May 16, 2024

WAZAZI NA WALEZI MKOANI LINDI WATAKIWA KUTUMIA MIFUMO RASMI KATIKA KUMALIZA MIGOGORO YAO

 

NA HADIJA OMARY

LINDI.


Wazazi na walezi Mkoani Lindi wametakiwa kuitumia vyema mifumo iliyowekwa na Serikali katika kushughulikia migogoro na tofauti zinazojitokeza katika familia zao  ambayo kwa kiasi kikubwa huchangia kuachana na  kusababisha watoto kuathiriwa kwa kukosa  malezi imara.



Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo  katika maadhimisho ya siku ya Familia ambayo kwa ngazi ya Mkoa yamefanyika katika viwanja vya soko la majengo halmashauri ya Mtama Mkoani humo.


Ndemanga amesema  Mifumo hiyo ni pamoja na madawati ya jinsia na Ofisi  za ustawi wa jamii zilizopo kwenye kila halmashauri.


Ndemanga ametaka wazazi kuitumia siku hiyo kutafakari namna ya kuimarisha ubora wa familia ikiwemo kutafuta suluhu ya tofauti zao kwa njia zinazofaa ili zisiendee kuathiri malezi na makuzi ya watoto.


“Watoto wetu wakati wanaimba wamekuambia kwa lugha nyepesi sana kwamba tunapogombana baba anakuwa na lakwakwe na mama pia anakuwa na lakwakwe hakuna anauejihusisha na malezi tunawapa shida watoto, lakini kwa hapa Lindi tunautamaduni wetu, wazazi tunapofarakana na kuachana tunaacha jukumu la ulezi kwa babu na bibi na wazazi hawawajibiki tena’ Alisema Ndemanga.


Awali, Akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Omari, Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt Kheri Kagya ameweka wazi namna ambavyo migogoro ndani ya familia inavyoathiri watoto ambapo amesema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 Mkoa wa Lindi unajumla ya Watoto 3797 walio katika mazingira magumu ambao wametokana na familia ambazo zina migogoro na malezi yasiyofaa huku katika madawati ya jinsia na ustawi wa jamii kukiwa na mashauri ya migogoro ya familia 13796 ambayo kwa sehemu kubwa yanahusu wazazi waliotelekeza watoto na kutotoa matumizi.


Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Lindi Joyce Kitesho amesema Jeshi la Polisi wanayo kampeni ya ushirikishwaji wa jamii isemayo familia yangu haina muhalifu kwani uhalifu huwa unaanzia kwenye ngazi ya familia endapo wazazi  hawatotimiza majukumu yao kikamilifu na akatumia nafasi hiyo kuwaomba wazazi kuwa walezi na sio watoa huduma.


Siku ya Familia Kimataifa Imeenda sambamba na kauli mbiu isemayo tukubali tofauti zetu kwenye familia kuimarisha malezi ya watoto.






BUWASA IPO TAYARI KUSAIDIA KPC

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mwakilishi wa mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba BUWASA mhandisi Matage Doto amesema mamlaka hiyo iko tayari kushirikiana na wadau wengine kusaidia  chama cha waandishi wa habari mkoa wa Kagera (KPC) katika ujenzi wa ofisi ya chama hicho.

Hayo yamekuja baada ya mwenyekiti wa club ya waandishi wa habari mkoani hapa Mbeki Mbeki, kumuomba mgeni rasmi kutoa msaada katika ujenzi wa ofisi ya waandishi wa habari kutokana na club hiyo kuwa na kiwanja ambacho tayari kimeishapata hati miliki.

Mhandisi Doto wakati akihutubia waandishi hao Mei 15,2024 wakati akiwa mgeni rasmi kwa niamba ya Mkurugenzi wa BUWASA katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika kimkoa mjini Bukoba ametoa pongezi kwa club hiyo kwa mawazo ya ujenzi wa ofisi na kusema kuwa, endapo club hiyo itaanza ujenzi ishirikishe wadau mbalimbali ikiwemo mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA.)

“Niwapongeze kwa kuwa na mawazo ya kuwa na ofisi yenu, mtakapoandaa mchanganuo wa bajeti ya ujenzi wa ofisi yenu pamoja na kubainisha taasisi zilizopo mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuwapa msaada na pale mtakapoona kwamba na sisi BUWASA tunaweza kusaidia tutakuwa tayari” amesema Mhandisi Doto

Aidha, akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi amesema waandishi wanapaswa kubobea katika kuandika habari Fulani ili waweze kuingia kwa undani juu ya makala wanazokuwa wanaandika.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Club ya waandishi wa habari mkoa wa Kagera Mbeki Mbeki amesema kuwa, maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu ni ya 31, na kutokana na takwimu kutoka World Press Freedom 2024 zimeonyesha Tanzania kufanya vizuri katika kuheshimu uhuru wa habari kwa kushika nafasi ya 97 kwa mwaka 2024 kutoka nafasi ya 142 kwa mwaka 2023.

Amesema Tanzania imepanda kwa kasi kwa nafasi 46 na kuziacha nchi nyingine za ukanda wa Afrika mashariki nyuma.

Mathias Byabato ni mwandishi wa habari mkoani Kagera akichangia juu ya kauli mbiu ya mwaka huu amesema kuwa, licha ya waandishi wa habari kuwa na wajibu wa kuelimisha jamii juu ya changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia wataalamu wa mazingira kutoka serikalini wanao wajibu wa kulinda maeneo ya vyanzo vya maji kwa kusimamia sheria.

Byabato ametolea mfano wa eneo la Kasalani na Rwamishenyi manispaa ya Bukoba ambalo ni eneo la maji ya mto Kanoni lakini kimemwagwa kifusi kikionyesha kuna mtu anahitaji kufanya ujenzi katika eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa, siku ya uhuru wa vyombo vya habari huadhimishwa kimataifa kila mwaka Mei 3 na mwaka huu imeadhimishwa Kitaifa jijini Dodoma kwa kusimamiwa na Muunganiko wa Umoja wa Vilabu nchini UTPC na mgeni rasmi alikuwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasimu Majaliwa na Kimataifa iliadhimishwa nchini Ghana na baada ya siku yenyewe yameadhimishwa ngazi ya mkoa.





Tuesday, May 14, 2024

ZAIDI YA WANANCHI ELFU 40 MTAMA KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA

 

Na HADIJA OMARY 

LINDI.

Zaidi ya wananchi Elfu 40 kutoka katika Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi wanatarajiwa kunufaika na mradi wa Maji na usafi wa mazingira unaotekelezwa  na taasisi isiyo ya kiserikali ya 'Heart to Heart' chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la KOICA utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.6

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katibu tawala Mkoa wa Lindi Bi zuwena Omary amewahimiza wananchi na taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa huo kutunza na kulinda vyanzo vya maji ili viendelee kutoa maji kwa muda mrefu. 

amesema upatikanaji wa maji safi na ya uhakika unategemea na utunzaji wa mazingira kuzunguka vyanzo vya maji  ikiwemo upandaji miti huku pia akitaka kamati za maji na mazingira zishirikishwe ili kufikia malengo ya mradi huo.

Mratibu wa mradi kutoka Heart to Heart Innocent Deus  amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa miaka sita kwa awamu tofauti ambapo kwa awamu ya kwanza utatekelezwa kwa miaka mitatu katika halmashauri ya Mtama na kuvifikia vijiji 87, na kaya zaidi ya elfu 40.


Amesema  Mradi huo una dhumuni la kupeleka huduma ya maji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa kuanzia ngazi ya vijiji hadi Wilaya.

Kwa upande wake Ismail Mbani Afisa afya na  mazingira Halmashauri ya Mtama amesema Mradi  huo wa maji  utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo na kuboresha usafi wa mazingira kwa Wananchi.

"Mradi huo utawasaidia hasa katika swala la uboreshaji wa vyoo ambapo kwa sasa hali ya vyoo katika halmashauri hiyo ni asilimia 54% ambapo hata hivyo kutokana na mvua zilizonyesha zilipelekea asilimia 1.7 ya kaya katika halmashauri hiyo kukosa vyoo kabisa hivyo basi kupitia mradi huu kutakuwa na maboresho makubwa katika eneo hii"





Monday, May 13, 2024

WASITISHA MASOMO BAADA YA SHULE YAO KUGEUKA MAKAZI YA WANANCHI WAATHIRIKA WA KIMBUNGA HIDAYA.

 

Na Mwandishi wetu

Lindi


Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha tarehe 04 Mei 2024   kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa saa 36 mfululizo ilisababisha  maafa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi huku wengi wao waliofikwa na maafa hayo wakijikuta wamekosa makazi, malazi na hata chakula.


 
Kijiji cha Mchakama kilichopo Wilayani Kilwa ni miongoni mwa  maeneo yaliyokumbwa na athari hizo za mafuriko ambapo zaidi ya kaya 400 zimekosa makazi huku wananchi1000 wakilazimika kuishi katika vyumba vya Madarasa vya Shule ya msingi Mchakama.


 
Hali hiyo ya vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Mchakama kutumika kama makazi kwa wananchi hao imesababisha wanafunzi zaidi ya 200 wanaosoma shuleni hapo kulazimika kukatisha masomo yao.


 
 
Mohamedi Mwadini ambae ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mchakama alisema shule hiyo inajumla ya Wanafunzi 291 ambao kati yao  138 ni wasichana na 153 wavulana wakijumuisha wanafunzi wa Darasa la Awali mpaka Darasa la saba.


 
“kati ya hao wanafunzi wa darasa la awali 43, darasa la kwanza55, lapilli 34, latatu 34, lanne 27, la tano 24, la sita 27na la saba 47 ambapo 52 kati yao wakiishi upande wa pili wa kijiji (ng’ambo) ambapo kutokana na mto kujaa maji hawana uwezo wa kuvuka upande wa pili ambako shule ilipo” alisema Mwl. Mohamed.


 
Aliongeza kwa kueleza kuwa ni siku ya saba tangu maafa hayo yalipotokea na Wananchi walioathirika na mafuriko kukosa makazi na kuhamia katika Shule hiyo ambapo kwa sasa wanafunzi wa Shule hiyo wamelazimika kusitisha masomo yao na kuziacha familia zikiishi katika madarasa ya Shule hiyo.


 
" kama Wananchi hawa wataendelea kubaki hapo kwa muda mrefu wanafunzi wataendelea kukosa masomo na pengine hata kiwango chao cha ufaulu kikashuka" alizidi kueleza Mwl. Mohamed.


 
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Mchakama Mussa Abdallah Mussa amesema baada ya mafuriko hayo kutokea jumla ya wakazi 1000 makazi yao yameharibika ikiwa ni pamoja na kupoteza mali zao, vyakula na malazi.


 
Alisema kati ya watu hao 1000 waliokutwa na Athari za mafuriko watu 600 kati yao wamelazimika kujihifadhi katika shule hiyo ya Mchakama kama Sehemu yao ya Makazi ya muda.


 
 
"Kijiji cha Mchakama ni kijiji cha asili watu hawakujikusanya pamoja hivyo Mto huu umegawanyisha  tuna kambi mbili ambazo zinawananchi 500 wakiwemo na hao wanafunzi mpaka sasahivi hawana huduma yoyote ya kijamii hawana chakula, hawapati matibabu na hata masomo kwa wanafunzi na hawawezi kuja huku kwa maana maji ni mengi".


 
 
"Jingine wananchi hawa waliopata Maafa tumewaweka pale katika vyumba vya madarasa kutokana na ukosefu wa maeneo na tunafahamu hivi karibuni mitihani ya mihula itaanza siku si nyingi hivyo ili kuwapisha wanafunzi hawa kuendelea na Masomo tunaiomba Serikali  kutupa maeneo pamoja na Mahema yatakayotuwezesha kuishi kwa muda huku wanafunzi hao wakiendelea kusoma".alisema Mussa.


 
Asia Josephat ni mzazi wa mwanafunzi  Zuhura Hassan anaesoma Darasa la kwanza katika shule hiyo ya msingi Mchakama amesema   baada ya mafuriko hayo kutokea miongoni mwa vitu vilivyosombwa  ni pamoja na vifaa vya shule vya  watoto.


 
" kwa hivyo hapa hata shule itakapofunguliwa na watoto kuruhusiwa kuendelea na masomo bado watoto wetu wanachangamoto za vifaa vya shule hivyo tunaiomba Serikali kutusaidia vifaa hivyo ili Wanafunzi hao watakaporuhusiwa kurudi shuleni waweze kuendelea na Masomo " alisema Asia.


 
"Lakini si hilo tu, sasa hivi ni muda wa magonjwa ya mlipuko tunapokusanyika watu wengi kwa wakati mmoja sehemu moja inakuwa ni rahisi kuingia ugonjwa ukizingatia hapa pia tunaishi na watoto wadogo wa miaka miwili, mitatu na kuendelea kwa hivyo mi niiombe serikali kwa muda huu mfupi hata kama tungeletewa maturubai ilimradi tukapisha hapa shuleni wanafunzi wakaendelea na shule maana kwa sasa hivi imejifungwa huwezi kuwaambia wanafunzi waje hapa kwa sababu madarasa yote ndo tumefanya majumba ya watu” aliongeza kusema Bi Asia.


 
 
Akizungumza Bungeni Alhamisi ya Mei 9 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema maeneo ya Kilwa na Mtwara yalirekodi kiwango kikubwa cha mvua zilizotokana na kimbunga Hidaya.


Kwa kawaida, wastani wa mvua kwa kituo cha Kilwa ni milimita 96.6 na kwa kituo cha Mtwara ni milimita 54.


 
Alisema hata hivyo, kuanzia Mei 3 hadi 4, 2024, jumla ya milimita 316 za mvua zilipimwa katika kituo cha Kilwa, sawa na asilimia 327 ya kiwango cha mwezi huku upande wa Mtwara, jumla ya milimita 99 zilipimwa katika muda huo ambazo ni sawa na asilimia 183 ya kiwango cha mwezi.


 
“Kwa hali ya kawaida, mvua ya milimita 316 iliyonyesha Kilwa kwa saa 36 tu, ni sawa na mvua ya miaka mitatu kwa mwezi Mei, yaani Mei 2024, Mei 2025 na Mei 2026”


 
Hiki ni kiwango kikubwa sana na ndiyo maana kumekuwa na madhara makubwa ya uharibifu wa miundombinu mbalimbali” alisema  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

 

Mei 1, 2024 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa taarifa ya uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa Pwani ya Mtwara ambapo mifumo ya hali ya hewa iliyopo ilionesha kuwa mgandamizo huo mdogo wa hewa ulitarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya kimbunga kamili siku ya  Mei 2, 2024.


 
Taarifa ya Mamlaka hiyo ilieleza wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, ulitarajiwa kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya Pwani ya Tanzania ikiwamo Mkoa wa Lindi kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa Mei 3, 2024 na kuendelea kuwepo katika maeneo ya ukanda huo hadi Mei 6,2024 kisha kukadiriwa kupungua nguvu baada ya Mei 6, 2024.


 
Uwepo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa ulitarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es salaam na maeneo ya jirani hivyo Wananchi walishauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya Wataalamu katika Sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.






 

 
 


Sunday, May 12, 2024

MANISPAA YA LINDI YAINGIA MAKUBALIANO YA BIASHARA YA HEWA UKAA

 

NA HADIJA OMARY 

LINDI.

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Lindi  limepitisha mkataba wa makubaliano ya Biashara ya hewa ukaa katika vijiji 10 , jumuhiya za uhifadhi wa Misitu 3  na msitu wa hifadhi wa manispaa na kampuni ya village climate solution limited (VCSL).

Wakizungumza katika kikao cha robo ya tatu ya baraza hilo ,  madiwani  hao wamesema kuwepo kwa biashara hiyo kutaiongezea Halmashauri chanzo kipya cha mapato na kwamba mradi huo utakuwa na manufaa kwa Manispaa na wananchi kwa ujumla


Meneja wa Mradi huo  yahya Mtonda amesema Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi kisichopungua miaka 40 katika Vijiji   vya Kiwawa, Mputwa, Milolo magharibi, Ruhoma, Muungano, Kinyope, Likwaya, na Makumba.

" sambamba na vijiji hivi mkatamba huu umehusisha jumuhiya za uhifadhi wa Misitu ambazo zimeanzishwa pembezoni mwa Mtaa wa Nandambi, pamoja na msitu wa hifadhi wa Makangara katika Manispaa hii ya Lindi nao pia umeingia katika Biashara ya hewa ukaa"

Amesema  miongoni mwa sababu ya mradi huo kutekelezwa kwa miaka 40  ni kufanya ulinzi wa Misitu hiyo kwa muda mrefu  ili kupunguza hewa ukaa kwa kuhifadi  Misitu hiyo ili viweze kuwasaidi vizazi vya sasa na vijavyo.

" ki asili misitu inaweza kuishi kwa muda mrefu hivyo basi kutokana na sababu hiyo basi miti inaweza kuendelea kuruhusu kufanyika kwa biashara hii ya hewa ukaa kwa kipindi hicho cha miaka 40

Kama tutaweza kuwezesha malipo ya fedha zinazotokana na biashara ya hewa ukaa kwa  kipindi cha miaka 40 basi fedha zile zitaenda kwenye shughuli mbalimbali za vile vijiji na ni matumaini yetu vijiji vitaenda kukua kwa kuboresha vijiji vyao

Pamoja na kusaidi makubaliano hayo pia Baraza limepitisha  mipango na sheria ndogo za uhifadhi wa Misitu kwa kijiji cha Milola, Mputwa na kijiji cha Namtamba  baada ya kusaidiwa na shirika la kuhifadhi misitu tanzania TFCG kuanzisha misitu ya hifadhi kwa kufanya matumizi bora ya Aridhi ya vijiji vyao kwa kipindi cha miaka 40.





JUMUIYA YA WAZAZI BAGAMOYO YASIMAMISHA UPIMAJI ARDHI CHALINZE.

 

Na Omary Mngindo, Chalinze.

JUMUIA ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imeitaka Idara ya Ardhi halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani hapa kusitisha upimaji wa ardhi katika eneo linalomilikiwa na Jumuia hiyo.


Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Aboubakary Mlawa, katika kikao kilichojumuisha wanachama wa Jumuia kwenye kuelekea sherehe za Wazazi Kitaifa, itayotanguliwa na ya Mkoa ambapo kiwilaya imefanyika Kata ya Bwilingu.


Alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa  ekari 50, Jumuiya hiyo ilipewa na uongozi wa Kijiji mwaka 2000 kwaajili ya kujenga shule ya wazazi, lakini wavamizi wametoa alama za mipaka ya eneo hilo na kujenga na sasa wanarasimisha  rasmi ili wapatiwe hati.


"Ardhi ni yetu hivyo kuwabana wale ambao wameingia watalazimika kutulipa hela yetu kulingana na thamani ya ardhi ya sasa, hatutawanyang'anya ila watafidia maeneo yetu kulingana na thamani ya sasa," alisema Mlawa.


Aliongeza kwamba "Mimi msimammo wangu ni huo zoezi lisimame kwa wale waliochukua mali zetu waturudishie, uzuri ni kwamba tunajua eneo letu lina ukubwa gani na linaanzia wapi," alisema Mwenyekiti huyo.


Kwa upande wake Diwani Wa Kata ya Bwililingu Nasser Karama alithibitisha kuwepo kwa eneo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limevamiwa na watu baadhi huku baadhi yao wakiwa wamejenga na wengine kuuza.


"Leo itanibidi niongee ukweli, moja ya vitu vinavyofanya nichukiwe na baadhi ya  wananchi ni namna ninavyotetea mali za chama na serikali, ninapofanya hivyo naambiwa naleta wawekezaji, lakini nashukuru wengi wameelewa sasa baada ya watu kuona ukweli," alisema Karama.


Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuia hiyo wakati huo ikitambulika Kata ya Chalinze Mzee Kibindu ameelezea namna ardhi hiyo ilivyogawanywa kwa viongozi, huku nae akipatiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo.


"Baada ya zoezi hilo kulikuwepo na hatua mbalimbali za kesi, na katika mchakato huo kila tulipokuwa tunakwenda tulikuwa tunashindwa, hivyo ninachojua pale hatuna eneo," alisema Kibindu huku wajumbe wakionesha kushangazwa kutokana na kauli hiyo.


Anold Mtumuyu aliyewahi kushika wadhifa mbalimbali wakati huo aliwaambia wanaJumuia hiyo kwamba akiwa kiongozi katika Kata amewahi kutembelea eneo hilo mara kadhaa, huku akisikitishwa na kauli ya Mzee Kibindu ya kwamba Jumuia haina ardhi katika eneo hilo.


"Mwenyekiti binafsi nimesikitishwa na kauli ya mzee wetu, kumbe wakati akiwa kiongozi kumbe nae alijimegea eneo lake, mimi nashauri tuanze na yeye kwani kuna mengi tutayafahamu zaidi," alisema Mtumuyu.


Wakichangia mada Alhaj Abdallah Sakasa na Amir Mramba wameelezea masikitiko yao kuhusiana na kuchukuliwa kiholela kwa ardhi ya Jumuia, huku wakishauri hatua za kisheria zichukuliwe kuwabaini wote ambao wamehusika na kuhujumu ardhi hiyo.






Saturday, May 11, 2024

RUNALI WAGAWA VITENDEA KAZI KWA WAKULIMA KUELEKEA MSIMU WA UFUTA NA MBAAZI

 

CHAMA kikuu cha ushirika (RUNALI) kinachounganisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa,  Nachingwea na Liwale Mkoani Lindi kimegawa jumla ya viroba laki 800,000, vitabu pamoja na kamba kwa wakulima wa wilaya ya Nachingwea, Ruangwa na Liwale kuelekea msimu wa mauzo ya mazao ya ufuta,Mbazi na Korosho.


 uzinduzi wa ugawaji wa vifungashio hivyo ulioenda sambamba na utoaji wa mafunzo wa matumizi mfumo wa TMX kwa watendaji wakuu wa vyama vya msingi (AMCOS) yaliyofanyika huko Wilayani Nachingwea.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo meneja wa chama hicho Jahida Hassan alisema kuwa wamegawa vifungashio hivyo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuhifadhi mazao kwenye ubora unaotakiwa sokoni.


Bi. Jahida  alisema kuwa RUNALI wamekuwa wanatoa elimu mara kwa mara kwa wakulima ili waweze kulima kilimo kilicho bora na kufanikiwa kupeleka mazao yaliyo bora sokoni.


" tupo  tayari kwa kuanza msimu mpya wa Mbaazi na ufuta na lengo la mafunzo haya ni kuwajengea utayari wa kwenda kwenye msimu mpya pia wametoka kufahamishana umuhimu wa kufanya ukaguzi.


  mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Adinan Mpyagila amewasihi wakulima kutouza mazao kiholela na kuweka vituo kwenye mipaka ya wilaya ili mazao yasiuzwe nje ya wilaya kwa kuwa itapelekea kupoteza mapato ya Halmashauri kwenye mazao ya mbaazi na ufuta.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha ushirika (RUNALI) Odas Mpunga amewapongeza vyama vya Ushirika kwa kazi kubwa waliyofanya na kuingiza mapato makubwa. Pia, amewataka kuyatumia vyema mafunzo haya kwa vitendo ili kuleta Matokeo chanya.






MLAO AWAASA MADIWANI MKOA WA PWANI.

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwishehe Mlao akizungumza na Madiwani hao (Hawapo pichani) Picha na Omary Mngindo.

...................................

Na Omary Mngindo, Pwani.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao, amekutana na Madiwani kutoka katika Halmashauri zote zinazounda mkoa wa Pwani, lengo ni kutathmini kuelekea uchaguzi ujao.


Katika kikao hicho kilichofanyika wilayani Mkuranga, Mlao amewaagiza madiwani hao  kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo katika chaguzi za Serikali za mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa mwaka 2024.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti huyo akiwakumbusha kuzingatia maadili, kuepuka udini, kutumia mitandao ya kijamii kwa tija, ukaribu na wananchi wakiwemo wana CCM kuelezea mazuri yanayofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu.


"Yeyote atakaye kiuka maadili ya chama chetu kwa kutukana mitandaoni, ninaagiza kuanzia sasa aitwe katika vikao husika na kujadiliwa sanjali na kuchukuliwa hatua za kinidhamu" alisema Mlao.


Aidha amewasisitizia madiwani hao pamoja na wanaCCM kuacha mara moja kujichukulia dhamana ya kuwa wasemaji katika mitandao au vijiwe bila kuwa na uhalali huo.


Kwa upande wake Katibu wa chama hicho mkoani hapa Bernard Ghaty alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha madiwani hao, akiwataka kuhakikisha hawapotezi  mitaa, viijiji wala vitongoji katika kata zao.


"Lengo la chama chetu ni kuhakikisha mitaa, vijiji na vitongoji vyote vinarudi CCM, mkumbuke Mwenyekiti wetu alipokea kijiti hiki nafasi zote za uongozi zikiwa CCM, ndoto yake ni kuona vijiji vyote vinarudi,' alisema Ghaty.


"Madiwani wa viti maalum fanyeni ziara kwenye Halmashauri zenu na si katika kata mnazoishi, nendeni mkakiimarishe chama, shughulikieni masuala yote pia kuzisimamia kwa mujibu wa sheria na kanuni katika majukumu yenu," alisisitiza Ghaty.


Aidha Katibu huyo amehitimisha kwa kuwataka Madiwani hao kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, kwa kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi ili chama hicho kiweze kushinda kwa asilimia zote.


Katika kikao hicho Madiwani hao wameahidi kwenda kutekeleza maagizo yaliyotolewa, na kwamba watafanya kazi kwa bidii na uzalendo ikiwa ni kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa.





DIBIBI AGAWA VITENDEAKAZI KISARAWE

 

Na Omary Mngindo, Kisarawe

MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Khamis Dibibi, mwishoni mwa wiki amegawa vitendeakazi kwa viongozi wa matawi 119 yaliyopo Kata zote 17 wilayani hapa.


Katika hafla hiyo chini ya mgeni mualikwa Kaimu Katibu wa Jumuia hiyo mkoani hapa Sophia Abdul, Dibibi alikabidhi vifaa hivyo lengo  ni kuwawezesha viongozi kutekeleza shughuli za kuwatumikia wanachama.


Vifaa alivyokabidhi ni pamoja na mihuri, reja za kusajiria wanachama wapya katika matawi, vidau vya mihuri (Stap Pad), kadi za Jumuiya ya wazazi 300 kila tawi sanjali na bips (Reflector).


"WanaJumuia wenzangu nimeamua kununua vitendeakazi hivi, lengo kubwa kuwawezesha katika kutekeleza majukumu yetu ya Jumuia, pia niwaombe tuhamasishe wanachama wapya wajiunge," alisema Dibibi.


Akizungumza na wanaJumuia hao, mgeni mualikwa amehimiza umoja, mshikamano na upendo huku akiwataka kujitokeza kuwania nafasi ya Wenyeviti wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.


"Tumpongeze Mwenyekiti wetu Khamis Dibibi kwa kutuwezesha vitendeakazi hivi, niwaombe tukavitumie katika kuhakikisha vinatusaidia kuwatumikia wanaJumuia," alisema Sophia.


Aidha aliongeza kwamba "Twendeni tukahamasishe wanachama wapya wajiunge katika Jumuia yetu, pia tugombee uenyekiti wa serikali katika uchaguzi ujao," alimalizia Kaimu Katibu huyo.





MTU MMOJA AFARIKI KWA KUSOMBWA NA MAJI BUKOBA.

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kifo cha mtu mmoja katika kata ya Bakoba manispaa ya Bukoba mkoani Kagera huku barabara zikifungwa kwa muda kutokana na baadhi ya madaraja katika barabara hizo kufunikwa na maji.


Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Kagera Zabron Muhumha akizungumza leo ametaja aliyefariki kwa jina moja la Lea anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 19 ambaye wakati anachota maji mtoni aliteleza na kusombwa na maji ya mvua.


"Mei 09,2024 majira ya saa 4:00 jioni binti huyo akiwa anachota maji katika mto aliteleza na kusombwa na maji na mwili wake ulipatikana  na kupelekwa kuhifadhiwa hospitali ya Rufaa ya mkoa, Bukoba" alisema Muhumha.


Ametaja madhara mengine yaliyopatikana na mvua hizo kuwa zimesababisha nyumba nyingi ambazo ziko mwambao wa mto Kanoni na ziwa Victoria kuzingirwa na maji na baadhi ya barabara kufungwa kwa muda.


Ametaja maeneo ambayo yamezingirwa na maji kuwa ni Kiwanja cha Jymkana kata ya Miembeni, baadhi ya nyumba Kasalani na Nyakanyasi kata ya Bakoba, Nyamkazi kata ya Miembeni na  Omukigusha  kata ya Bilele.


Aidha amesema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu na linazungukia maeneo ambayo ni hatarishi na kuwajuza wananchi wahame maeneo hayo, kila mwaka yamekuwa yakijaa maji kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha ardhi imejaa maji hata ikinyesha mvua ya wastani maji yanajaa mengi sana hivyo wahamie maeneo salama.


Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bakoba Shaaban Rashid amesema kuwa, katika kata yake mtaa wa Nyakanyasi eneo la Mwizinga mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Mei 10,2024 ilisababisha eneo hilo kujaa maji na walikuwa wanaendelea na zoezi la kutoa watu ndani ya nyumba na kuwapeleka maeneo salama.


Amewaomba wananchi ambao maeneo yao huwa yanajaa maji hata kama bado hayajawafikia kuhama maeneo hayo kwa ajili ya kulinda usalama wao.


Aidha diwani wa kata ya Miembeni
Richard Gaspal amesema kuwa katika mtaa wa Nyamkazi eneo hilo limejaa maji kwani ni eneo ambalo liko mwambao wa ziwa Victoria na hata barabara hazipitiki zimejaa maji  na daraja lililojengwa hivi karibuni limefunikwa na  maji hivyo wananchi wanapita kwenye vichochoro wanapanga mawe wanapita ili kuhama katika maeneo yao na kwenda maeneo salama.


Amesema, baadhi ya waathirika wamehamia kata ya Kashai na wengine wamewawekwa sehemu moja katika shule ya msingi Nyamkazi.


Ikumbukwe kuwa, mji wa Bukoba ni mji ambao uko katika mwambao wa ziwa Victoria na kuna mito inapita katika mji huo ikimwaga maji yake katika ziwa hilo na nyumba zaidi ya 70 zimeathiriwa na maji.