Saturday, March 30, 2024

TUISOME KWA WINGI QURAN TUKUFU-DK.MWINYI



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi amewahimiza Waumini wa Dini ya kiislamu kuendelea kuisoma kwa wingi Quran Tukufu katika kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika fainali za kwanza za Mashindano  ya kuhifadhi Quran  Tukufu  Afrika Mashariki yanayosimamiwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ikiwemo washiriki tisa kutoka nchi za Afrika Mashariki katika Uwanja wa  New Amaan  Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 30 Machi 2024.

Aidha Rais Dk.Mwinyi ameiomba Ofisi ya Mufti  Mkuu wa Zanzibar kuzidisha juhudi za malezi ya vijana na kuwaongoza katika maadili na tabia njema ili wawe raia wema na wenye hofu ya Mungu.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mashindano hayo  kufanyika kila mwaka.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amezipongeza Taasisi za Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuandaa mashindano  hayo makubwa ambayo yanaitangaza Zanzibar.

Mshindi wa kwanza wa Mashindano hayo ni Mahmoud Kassim Nassor wa  Zanzibar aliyepata shilingi milioni  30 mshindi wa  pili Abdourahamane Papa Said  kutoka Comoro shilingi milioni 20 ,  na mshindi wa tatu Abdulrahman Mussa   kutoka Kenya shilingi milioni 10.














Saturday, March 16, 2024

MSIMAMIZI WA UCHAGUZI BAGAMOYO, AWAAPISHA MAKARANI WA UCHAGUZI MDOGO KATA YA FUKAYOSI.


 

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bagamoyo Shauri Selenda, amewataka makarani waongozaji katika uchaguzi mdogo wa kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mafunzo watakayopewa.


Selenda ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo kwa Makarani waongozaji wa uchaguzi mdogo kata ya Fukayosi Haashauri ya Bagamoyo ambapo alisema makarani wanapaswa kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi katika kutekeleza majukumu yao kama watakavyoelekezwa katika mafunzo hayo.


Alisema kazi ya ukarani wa uchaguzi inahitaji uvumilivyu, subira na busara katika utendaji wake kwani kazi hiyo inawakutanisha na watu tofauti ambao wanahitaji kusikilizwa, kuelekezwa na kuongozwa juu ya kile wanachopaswa kufanya katika kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi.


Makarani hao walikula kiapo cha kutekeleza majukumu hayo tayari kwaajili ya uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2024.


Kiti cha udiwani kata ya Fukayosi kimebaki wazi baada ya aliyekuwa Diwani wa kata hiyo kufariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu mnamo mwezi Novemba mwaka 2023.


Akizungumza kwa niaba ya Makarani wenzake, Athumani Hassan Fundi, amesema watahakikisha wanazingatia kile wanachofundishwa ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi

Alisema nia wameipokea kazi hiyo kwa moyo mmoja na wapo tayari kufuata maelekezo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kufanikisha kazi hiyo muhimu.