Sunday, December 31, 2017

KOROSHO ZAINGIZA BILIONI 39 PWANI



Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga.

MKOA wa Pwani ,tayari umeuza tani 19,815 ambazo zimeingiza  zaidi ya bilioni 39 tofauti na msimu uliopita ambapo uliuza tani 13,000 na kupata bilioni 33.##

Mkoa huo umejiwekea lengo la kuuza tani 25,000 hadi 30,000 kwa msimu huu ambao  minada yake ya korosho ikiwa bado inaendelea .

Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,aliyasema hayo Mkuranga ,wakati akizungumzia changamoto na mafanikio waliyoyapata msimu wa korosho 2017/2018 .

Alieleza ,mbali ya hayo wakulima wa korosho mkoani Pwani wakiwa bado wanadai zaidi ya bilioni tano.

Mhandisi Ndikilo alisema ,kuuza tani 19,815 hadi sasa ni mwanzo mzuri wa kufikia malengo yao waliyojiwekea msimu huu.

Alisema ,hatua hiyo imetokana na serikali kutoa pembejeo bure katika msimu huu na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Alibainisha ,licha ya mafanikio hayo lakini kuna changamoto zimejitokeza tangu kuanza kwa minada mwaka huu ikiwemo uhaba wa magunia .

Kero nyingine ni ile iliyojitokeza sasa ya kuchakachua ubora wa korosho unaofanywa na baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).

“Changamoto ya magunia inaweza kuwa historia endapo tutakubaliana kwa kukaa na mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha wawekezaji waje wawekeze kiwanda cha magunia lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo hili” alifafanua .

Akizungumzia kuhusu tatizo la ubora wa korosho, mhandisi Ndikilo ,alisema baadhi ya Amcos zimejiingiza kwenye kuhujumu minada hiyo kwani baadhi yao wameweka michanga na mawe kwenye magunia ya korosho .

Alisema huo ni wizi,uhujumu uchumi na kuaibisha sifa ya nchi ya Tanzania nje ya nchi kwani magunia hayo yangefika India na nchi nyingine ingekuwa aibu na fedheha.

Kutokana na upuuzi huo ndio maana nimeamua kutoa maagizo kuwa Amcos 10 zilizojihusisha na ubabaishaji huo viongozi wake wakamatwe na kuhojiwa.

Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo ,kuwepo kwa maghala makubwa itainua soko la korosho msimu ujao na kuondoa ubabaishaji wa maghala ya vichochoroni yanayoleta dosari .

Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani  ni mkombozi kwa wakulima hivyo anawashangaa wale wanaobeza na kuyumbisha mfumo huo.

Mhandisi Ndikilo ,aliwataka wakulima wa korosho kuacha kukubali kurubuniwa na madalali ama wanunuzi wachache hali inayosababisha kukosa mapato kulingana na korosho zao.

Serikali mkoani humo imewatoa shaka wakulima wa korosho ambao bado hawajalipwa fedha zao na kudai itasimamia makampuni na wanunuzi kulipa kwa wakati na changamoto zinazojitokeza.

CGP. DKT. JUMA MALEWA AHUTUBIA BARAZA LA KUFUNGA MWAKA 2017.



Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akiongoza Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018. Baraza hilo limehudhuriwa na Maafisa na Askari kutoka vituo mbalimbali vya Magereza Mkoani Mbeya, Chuo cha Magereza Kiwira na Chuo cha Ufundi Mbeya ambapo Baraza hilo limefanyika leo Desemba 31, 2017 katika Viwanja  vya Magereza Mkoani Mbeya.


Baadhi ya Askari wa kike wa Jeshi la Magereza kutoka vituo mbalimbali vya Magereza ya Mkoa wa Mbeya wakisikiliza hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(hayupo pichani) katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018.

Wakuu wa Magereza yaliyopo Mkoani Mbeya wakifuatilia kwa umakini mkubwa maelekezo ya Kamishna Jenerali wa Magereza aliyoyatoa katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018.

Mkuu wa Magereza Mkoani Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Kijida Mwakingi akitoa taarifa fupi ya Mkoa wake katika Baraza Maalum la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018.

Naibu Kamishna wa Magereza, Tusekile Mwaisabila akitoa ufafanuzi wa masuala yahusuyo Divisheni ya Huduma za Urekebishaji mbele ya  Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa pili kulia) katika Baraza la kufunga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018 (wa kwanza kushoto) ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Mbaraka Semwanza. Baraza hilo limefanyika katika Viwanja  vya Magereza Mkoani Mbeya.

Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu katika Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Chacha Binna akitolea ufafanuzi kuhusiana na masuala ya madeni ya watumishi yaliyoulizwa na Maafisa na Askari wa Jeshi hilo Mkoani Mbeya(hawapo pichani) katika Baraza hilo.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akikagua gwaride la Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kabla ya kuhutubia Baraza Maalum la Maafisa na Askari wa Jeshi hilo lililofanyika katika Viwanja vya Magereza Mkoani Mbeya leo Desemba 31, 2017

Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza