Friday, August 30, 2019

MICHEZO YA WATOTO HUCHANGIA KATIKA UKUAJI WAO.

Na HADIJA HASSAN, LINDI.

Zaidi ya asilimia 75% ya Watoto wanaolelewa kwenye mazingira ya upweke, (geti kali) na wanaokosa vifaa vya kuchezea katika mazingira wanayoishi huchelewa kufikia hatua za ukuwaji kwa haraka.

Hayo yameelezwa na Mtaalamu wa Lishe wa Manispaa ya Lindi, Mwenda Gellah alipokuwa anazungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG ofisini kwake.

Mwenda alisema kitendo cha baadhi ya wazazi ama walezi kuwalea watoto wao kwenye mazingira ya upweke, kunawanyima watoto hao kutofikia hatua za ukuwaji kwa haraka kutokana na kushindwa kujifunza kutoka kwa watoto wengine.

Alisema hali ya Mtoto kujichanganya katika michezo na watoto wengine ni namna bora ya kupata uchangamshi ambao unamuwezesha mtoto kujenga uwezo wake wa kukuwa kiakili hata kimwili.

Kwa upande wake Muuguzi mkunga wa Kituo cha Afya mji Manspaa ya Lindi Victoria Mlope alisema kuwa kitendo hicho cha wazazi kuwafungia Watoto ndani licha ya kutofikia hatua za ukuwaji kwa haraka lakini pia kitendo hicho kinawafanya watoto hao kushindwa kupata mahusiano ya kijamii na watoto wenzao.

Hata hivyo Mlope aliongeza kuwa michezo kwa mtoto humsaidia kuongeza uwezo wa kujifunza kwa kuujenga ubongo wake ambapo alisisitiza kuwa ni vizuri wazazi wakatenga muda wa kuwaacha watoto wakachanganyika na watoto wezao katika michezo mbali mbali ili waweze kujifunza.

Akizungumzia juu ya Baadhi ya Wazazi/walezi kuwalea Watoto wao kwa geti kali Mkazi wa Manispaa ya Lindi Othumani Mzee alisema kuwa baadhi ya wazazi wanaowalea watoto wao kwa namna hiyo mara nyingi wanahofia tabia ovu kutoka kwa watu wanaowazunguka huku akisema kuwa hiyo ni dhana potofu

“Mtoto anaweza kuwa na tabia ovu hata asipochangamana na watoto wenzake wa Mtaani msingi wa kumlea mtoto unatokana na wazai wenyewe kumfungia mtoto sio suluhisho tunatakiwa kuwafundisha watoto kwa kuwaelewesha lipi zuri na lipi baya bila hata kuwafungia ndani” alisema Chilewa

UHABA WA KONDOM LINDI, MADIWANI WAPAZA SAUTI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Mkoani humo wametaka kufahamu sababu ya kuadimika kwa Kondomu katika Halmashauri yao Madiwani hao walihoji hilo, wakati wa kikao cha Baraza kupitia na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kamati mbalimbali, ikiwemo ya Ukimwi katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo uliopo mjini Lindi.

Miongoni mwa wajumbe wa Baraza hilo waliotaka kufahamu sababu za kutopatikana kwa zana hizo muhimu katika maeneo mbali mbali ya Halmashauri yao ni Diwani wa Kata ya Namangale, Sudi Kanduru (CCM).

Kanduru alisema amelazimika kuuliza Swali hilo kutokana na kupokea malalamiko kutoka kwa Wananchi wa kata yake ambapo alidai kuwa hata hivyo alifanya uchunguzi katika baadhi ya maeneo hayo na kubaini kuwepo kwa ukweli juu ya malalamiko ya wakazi wake.

Hoja hiyo ya Kanduru liliungwa mkono na madiwani wenzake akiwemo Mohamedi Mkulyuta {Kiwalala}, Halima Mwambe (Rondo) na Hassani Kunyong’onyea (Mtama) ambapo kwa pamoja walishauri jitihada za makusudi na haraka zifanyike zipatikane Kondomu ili kunusuru Afya za Jamii zao.

Nae Hasani Kunyongonyea Diwani wa Kata ya Mtama (CHADEMA) alisema iwapo jitihada za upatikanaji wa zana hizo hautaharakishwa kuna hatari kubwa ya idadi ya wananchi kuathirika na maambukizi ya VVU pamoja na magonjwa mengine ya Zinaa katika Wilaya hiyo.

Akijibu madai ya Madiwani hao, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Samweli Gunzari amewaondoa hofu wananchi kupitia wawakilishi wao kwa kusema anatambua uwepo wa upungufu wa zana hizo na kueleza Serikali inalifanyia kazi ili ziweze kupatikana ili jamii iweze kuzitumia.

Thursday, August 29, 2019

WAKULIMA WA MUHOGO MKURANGA WAPATA KIWANDA KWA AJILI YA KUCHAKATA ZAO LA MUHOGO


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Ndikilo kushoto akipeana mkono wa pongezi na Mkurugenzi mtendaji wa  kiwanda cha kuchakata zao la  muhogo mara baada ya halfa ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho amabcho kimejengwa katika kijiji cha Mgenge kata ya Beta Wilayani Mkuranga.
.............................
VICTOR  MASANGU, MKURANGA

KILIO cha muda mrefu ambacho kilkuwa kinawakabili wakulima wa zao la muhogo katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani hatimaye hivi karibuni  wanatarajia   kuondokana na changamoto sugu ya upatikanaji wa soko la uhakika   kufuatia kuanza  kwa  ujenzi wa mradi  wa kiwanda kikubwa cha kuchakata zao hilo  ambacho kitagharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.5.


Hayo yamebainishwa na baadhi ya wakulima hao wakati wa Ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa halfa ya uwekeaji wa jiwe la msingi katika kiwanda hicho ambacho kimejengwa na mwekezaji kutoka nchini China katika kijiji cha Mkenge  kata ya Beta Wilayani Mkuranga ambapo wamedai hapo awali walikuwa na tatizo la kuuza mihogo yao  kwa bei ya hasara.


“Sisi kama wakulima wa zao hili la muhogo katika Wilayah hii ya Mkuranga tumefarijika sana kwa ujio wa mradi wa kiwanda hiki ambacho kimejengwa na marafiki zetu wa kutoka nchini china, na tunashukuru kwa jitihada ambazo zinafanywa na Mkuu wetu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Rais wetu Dk. John Pombe Magfuli kwa kuwaleta wawekezaji hawa ambao watatusaidia kuondokana na tatizo la kupata soko la uhakika,”walisema wakulima hao.


Kwa  upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka maafisa kilimo wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuwasimamia vema wakulima wa zao hilo la muhogo  kutonyonywa na walanguzi na  kupata haki zao stahiki na kuahidi kuwaondoa kazini wale wote ambao watabainika kukwamisha juhudi za serikali  katika uwekezaji wa sekta ya  viwanda.


Aidha Ndikilo alisema kuwa lengo kubwa la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inawasaidia kwa hali na mali wananchi wake katika kuondokana na changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika na ajaira, hivyo atahakikisha zao hilo la muhogo linapata soko kupitia viwanda ambavyo vinajengwa na wawekezaji katika maeneo mbali mbali na kuwahimiza wasikate tamaa na badala yake waendelee zaidi kulima mazao ya biashara ikiwemo ufuta, muhogo na korosho.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto  Sanga amesema kuwa  kipindi cha nyuma wakulima wengine walikuwa tayari  wameshakata tamaa  katika kilimo  cha zao la muhogo, hivyo kukamilika kwa kiwanda hicho kitaweza kuleta mabadiliko chanya kwa kuwapa fursa wananchi kuwa na soko la uhakika.


“Kwa kweli wananchi wangu hasa kwa wakulima wa zao hili la muhogo katika Wilaya ya Mkuranga baadhi yao walikuwa tayari wameanza kukata tamaa kabisa kutokana na mfumo ambao ulikuwepo wanauza mazao yao kwa bei ya hasara lakini kwa sasa kiwanda hiki kinachotarajiwa kukamilika mwaka huu wataondokana kabisa na changamoto ya soko,” alismema Sanga.


Awali akisoma Risala ya ujenzi wa mradi huo  mmoja wa vongozi  wa kiwanda hicho, Leonard Jambeli  kwa niaba ya Mkurugenzi amebainisha kwamba waanategemea kutoa fursa za ajira za moja kwa moja  kwa wazawa zaidi ya mia moja pindi uzalishaji utakapoanza kufanyika rasmi.


Kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa kiwanda mwishoni mwa mwaka huu  kutaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa zao hilo katika halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani  ambao kwa miaka mingi walikuwa wanapata hasara kutokana na kunyonywa na walanguzi  kununua zao hilo  kwa bei ndogo.

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kushoto Ramadhani Maneno akimshika mkono Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ikiwa ni moja ya ishara ya kumpongeza katika juhudi zake za kuunga mkono juhudi za serikali katika ujenzi wa viwanda.


 Mkuu wa Mkoa wa Pwani kushoto Mhandisi Evarist Ndikilo akipata maelekezo kutoka kwa mkurugenzi mtendaji wa kiwanda cha kuchakata muhogo wakati alipofanya ziaara yake ya kikazi kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho, (PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU)