Thursday, November 8, 2018

KAWAMBWA APONGEZWA JIMBONI KWAKE.

 Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.

Na Omary Mngindo, Bagamoyo

Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa amepongezwa kwa kitendo cha kutoa ardhi ekari 6 na nusu kwaajili ya ujenzi wa shule ya msingi.
Pongezi hizo zimetolewa na WAKAZI wa Kitongoji cha Kitopeni Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, na kuongeza kuwa kitendo hicho ni cha kizalendo na wanamshukuru kwa hatua hiyo.

Wakizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mbunge huyo mbele ya Mwenyekiti wao Bushir Kitumboi, wakazi Sapi Ibrahimu na Lumpa Rajabu kwa niaba ya wenzao walisema kuwa, wamefurahishwa na hatua ya Mbunge huyo kwa kujitolea ardhi hiyo kwa ajili ya shule.

Sapi alisema kwamba hatua ya mbunge wao kuwapatia ardhi eneo la mjini, ni kitendo cha kiubinadamu na kujali elimu kwa watoto na kwamba angetaka kuiuza angepata mamilioni ya shilingi.

"Binafsi nimegushwa na juhudi hizi za Mbunge, ameamua mwenyewe kutupatia eneo, umeamza ujenzi, kwa mapenzi yake akatuongezea nguvu ya trekta kwa ajili ya kufanikisha ujenzi, binafsi namshukuru kwa ubinadamu aliouonesha," alisema Sapi.

Nae Lumpa alisema kwamba kabla ya kupatikana kwa eneo hilo na ujenzi huo, wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma ya kielimu, lakini kwa sasa wanashukuru kwa shule kuwa karibu.

Mwenyekiti Kitumboi alisema kuwa wananchi wanatambua juhudi zinazofanywa na mbunge wao, sanjali na viongozi wote ngazi mbalimbali katika kuiletea maendeleo Kitopeni, na Jimbo kwa ujumla, huku akiwaomba kuendelea kuwapatia ushirikiano viongozi hao.

"Kwa hili la ardhi ambayo tumeshaanza ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, wana- Kitopeni tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele kupitia Mbunge wetu, ameonesha kutujali kwenye sektq muhimu ya elimu kwa watoto wetu," alisema Kitumboi.

Akizungumza na wananchi hao, Dkt. Kawambwa alisema kuwa ameshawishika kuwakabidhi ardhi hiyo baada ya kuona uwepo wa umuhimu wa shule kwenye eneo hilo, ili kuwakomboa watoto waliokuwa wanateembea umbali mrefu kufuata masomo.

"Nimeona watoto wetu wanavyotembea umbali mrefu kwenda kusoma, nimetoa ardhi ile kwa moyo mmoja ili tujenge shule itayosaidia vizazi vyetu, pia nimetoa trekta kwa ajili ya shughuli mbalimbi za ujenzi wa shule," alisema Dkt. Kawambwa.

No comments:

Post a Comment