Mbunge wa Buchosa Mkoani
Mwanza Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Kulia) akifurahi jambo pamoja
na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa hafla ya
makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo
tarehe 22 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).
..............................................
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Aliyewahi
kuwa Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa Mkoani
Mwanza leo tarehe 22 Novemba 2018 amemkabidhi rasmi ofisi Waziri wa kilimo Mhe
Japhet Hasunga (Mb).
Makabidhiano
hayo yamefanyika katika Ukumbi wa mikutano maarufu kama Kilimo IV Jijini Dodoma
na kuhudhuriwa na Naibu mawaziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent
Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, na Wakuu
wa idara na Vitengo.
Akizungumza
katika hafla hiyo fupi Mhe Dkt Tizeba amempongeza Mhe Hasunga kwa kuteuliwa
kuhudumu katika nafasi hiyo ambapo amesisitiza kusimamiwa kwa weledi huduma za
ugani ambazo kwa kiasi kikubwa hakuna jambo la kujivunia katika eneo hilo
kutokana na mgawanyo wa kimajukumu kuwa katika wizara mbili ya kilimo na
TAMISEM jambo ambalo linapunguza ufanisi wa kiweledi.
Alisema
kuwa wizara inapaswa kuendelea kusomesha wataalamu mbalimbali nchini wakiwemo
wa ugunduzi na utafiti ili kuongeza tija ya kilimo na utoaji elimu kwa wakulima
na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa wananchi sambamba na Taifa kwa ujumla.
Vilevile
amesema kuwa Wizara ya kilimo ni tanuru muhimu kwa mahitaji ya wananchi hivyo
inapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi na serikali ikiwa ni pamoja na kupewa fedha
kwa wakati ili kukamilisha miradi mbalimbali ambayo tayari imeanzishwa.
Kuhusu
mfumo wa uzalishaji wa mbegu alisema kuwa serikali ina Wakala wa mbegu za
kilimo (ASA) ambao wanafanya kazi nzuri ya uzalishaji wa mbegu lakini wanapaswa
kuwezeshwa ili waweze kuzalisha mbegu kwa kutumia mfumo wa umwagiliaji badala
ya kuzalisha mbegu wakati msimu wa kilimo unaendelea.
“ASA
wanazalisha mbegu wakati ambapo msimu wa kilimo umefika hivyo mbegu zao
zinakosa umuhimu kwa wakulima, hivyo wanapaswa kuzalisha mbegu kabla ya msimu
wa kilimo kufika” Alisisitiza Dkt Tizeba.
Kuhusu
mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa unaendelea vyema lakini
hausimamiwi ipasavyo na Taasisi zingine za serikali zilizopewa jukumu kubwa na
muhimu la kusimamia shughuli hiyo wakiwemo Wakala wa majengo Tanzania (TBA).
Kwa
upande wake Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amempongeza waziri huyo
mstaafu Mhe Dkt Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa kwa kazi kubwa
aliyoifanya kwenye wizara ya kilimo ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa weledi
ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kipindi cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka
2018/2019 ambayo imekuwa kwa asilimia 7.1
Waziri
Hasunga alisema kuwa Dkt Tizeba ni mfano wa kiongozi bora nchini ambaye
ametekeleza majukumu yake kwa weledi na kutoa ushirikiano mkubwa kwa viongozi
wengine jambo ambalo linatoa chachu na kuonyesha jinsi alivyo mzalendo kwa
Taifa.
“Kutokana
na alama alizoziacha Dkt Tizeba kwenye wizara ya kilimo hakika tunastahili
kumuona kama Mtakatifu kwani kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa
chakula nchini lakini alisimamia kidete na kuhakikisha kuwa swala hilo linamalizika na sasa
nchi ina ziada kubwa ya chakula hakuna njaa”
Alikaririwa
Mhe Hasunga na kuongeza kuwa“Dkt Tizeba alihakikisha kero ya Tozo na Kodi
zinafutwa na kusaliwa na Tozo na Kodi chache jambo ambalo limeongeza ufanisi
katika wizara, usimamizi huu mzuri uliofanywa hauwezi kusahaulika daima
Mhe
Hasunga aliongeza kuwa mfumo wa uagizaji mbolea wa pamoja ulisimamiwa vizuri na
Dkt Tizeba jambo hilo
litasalia kuwa muhimu na alama kwa Taifa.
Aidha,
Alisema kuwa katika uongozi wa Dkt Tizeba nchi imezidi kuimarika kupitia
manufaa wanayoyapata wananchi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na
mfumo wa ushirika ambao wananchi walipoteza imani kwa kiasi kikubwa na Ushirika
lakini kwa kipindi cha muda mfupi umeimarika kwa kiasi kikubwa.
Waziri wa kilimo Mhe
Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya kilimo wakati
wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo
tarehe 22 Novemba 2018.
Picha ya pamoja waziri wa
kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), Mbunge wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe
Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Naibu mawaziri wizara ya kilimo Mhe Omary Mgumba
na Mhe Innocent Bashungwa, na Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew
Mtigumwe wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wote wakati wa hafla
ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo tarehe 22 Novemba 2018.
Mbunge
wa Buchosa Mkoani Mwanza Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa
hafla ya makabidhiano ya Ofisi Jijini Dodoma leo
tarehe 22 Novemba 2018.
No comments:
Post a Comment