Sunday, November 25, 2018

MAHAFALI KIDATO CHA NNE 2018 YEMEN DYCCC, WADAU WATAKIWA KUWEKEZA KWENYE ELIMU.



Wahitimu wa kidato cha nne 2018 na elimu ya awali katika shule za Yemen DYCCC Chang'ombe jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Pazi Mwinyimvua akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne na elimu ya awali katika shule za Yemen DYCCC, kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu ya shule za Yemen DYCCC, Hassan Akrabi na kulia ni Mwalimu Mkuu wa sekondari Hamisi Togwa.
................................................


Wadau wa Elimu wametakiwa kuwekeza kwenye elimu ili kuwawezesha vijana kujiondoa kwenye fikra potofu.


Akizungumza kwenye mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne 2018 na elimu ya awali,  katika shule za Yemen DYCCC, mgeni rasmi katika mahafali hayo Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Pazi mwinyimvua alisema uwekezaji katika elimu ndio msingi mzuri kwa vijana utakaowasaidia katika maisha ya dunia na akhera.

Alisema uislamu umehimiza elimu zote zenye manufaa bila ya kuchagua, hivyo vijana wanapaswa kujengewa katika misingi ya kutafuta elimu.

Alifafanua kuwa, Nabii Adam alianza kufundishwa majina ya vitu vyote na baadae kupokea muongo kutoka kwa mola wake, hii dalili ya kuwa katika elimu ni lazima upate elimu ya mazingira itakayokusaidia katika maisha ya dunia na ile ya muongozo itakayokuongoza katika maisha ya akhera.

Dkt. Pazi alisema ili kuyafikia hayo ni wazi kuwa waanzilishi wa shule wanatakiwa kusukumwa na nia iliyo thabiti ya kujua kuwa wanachokifanya ni katika sadaka inayoendelea kwa jamii.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuipongeza Taasisi ya DYCCC inayomiliki shule za Yemen kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kusomea hali inayopelekea mtoto kupata hamu ya kusoma.

Akizungumzia misingi ya elimu Dkt. Pazi alisema inaanzia kwenye majengo, vitendea kazi, walimu wenye moyo wa kujituma, wanafunzi waliopata malezi mazuri ya wazazi na wazazi au walezi wenye kufuatilia maendeleo ya vijana wao na kuongeza kuwa kwa mkusanyiko wa aina hiyo ndipo inapatikana elimu bora yenye manufaa kwa vijana.

Kwa kuzingatia hayo aliwataka wamiliki wa shule kuwajali walimu kwa kutoa motisha kwa wanaofanya vizuri ikiwa njia ya kumfanya mwalimu aongeze juhudi na kupata matokeo mazuri kwa wanafunzi.

Akizungumzia, wajibu wa mwalimu alisema mwalimu ana wajibu wa kutumia taaluma yake kwa kuchunga kanuni na misingi ya kazi yake huku akitakiwa kuhakikisha kile anachokifundisha kinafika kwa mwanafunzi kama ilivyokusudiwa,

Katika hatua ya kujenga muhimili mmoja amewataka wazazi na walezi kusimamia malezi ikiwa ni pamoja na nidhamu na maadili kwa kushirikiana na walimu kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyokuwa sahihi huku watoto wakitakiwa kuwatii wazazi wao na kuzingatia kile wanachofundishwa na walimu wao.

Mwenyekiti wa Bodi ya shule za Yemen Hassan Akrabi aliwataka wahitimu kuzingatia kile walichofundishwa shuleni hapo ili waendelee kuwa na tabia njema.

Alisema katika jamii kuna vishawishi vingi vinavyopelekea vijana wengi kutoka nje ya maadili hivyo ni wajibu wao kuwa makini ili kulinda heshima yao.

Aliongeza kwa kusema kuwa, kwa muda mrefu waliokuwepo shuleni wamejifunza mabo mbalimbali kwa lengo la kwenda kendelea na kile walichokipata katika masiha ya kawaida.

Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi kwa niaba ya meneja wa shule za Yemen, Mwalimu Mkuu wa Sekondari, Hamisi Togwa alisema shule za Yemen kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita zimeanzishwa kwa lengo la kuwalea watoto kimwili na kiroho katika maadili mema yanayozingatia haki na uadilifu ili waje kuwa viongozi bora kwa Taifa.

Alisema shule za Yemen ni miongoni mwa shule zenye wastani wa kati hapa nchini na zinaendelea kufanya vizuri katika kiwango hicho tangu kuanzishwa kwake katika ngazi ya wilaya, Mkoa, Kanda na Taifa kwa ujumla.

Jumla ya wanafunzi wa elimu awali 95 wamemaliza ngazi ya awali kwa kipindi cha miaka mitatu na wahitimu 65 wamehitimu elimu ya kidato cha nne 2018


  
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu ya shule za Yemen DYCCC, Hassan Akrabi akiongea katika mahafali hayo.

 
Mwalimu Mkuu wa sekondari Hamisi Togwa akizungumza katika mahafali hayo.
 Wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Yemen DYCCC wakipunga mikono kama ishara ya kuaga.
 Wahitimu wa elimu ya awali katika shule ya awali ya Yemen DYCCC, Chang'ombe jijini Dar es Salaam wakionyesha baadhi ya vitu walivyofundishwa.
 
Wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Yemen DYCCC wakionyesha miongomi mwa masomo waliyofundishwa shuleni hapo.
 
Wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Yemen DYCCC wakionyesha namna mitandao ya kijamii invyo athiri jamii.



Meza kuu wakifuatilia maonyesho mbalimbali yalikuwa yakitolewa na wahitimu katika shule za Yemen DYCCC Chang'ombe jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment