SERIKALI imesema kamwe haitokatishwa
tamaa na kauli ya baadhi ya Viongozi na wanasiasa kuhusu dhamira yake ya
kutekeleza miradi mikubwa ya kimamkati yenye malengo ya kuleta maguezi ya
kijamii na kiuchumi kwa Watanzania.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali,
Dkt. Hassan Abbasi wakati wa ziara ya kutembelea Kituo cha Redio ya TBC Taifa
na tathmini ya utendaji kazi katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya
Awamu ya Tano.
Dkt. Abbasi alisema tangu kuingia
madarakani kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Serikali ya Awamu imekuwa
ikitekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo wadau mbalimbali wa maendeleo
wameipongeza Serikai yake kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa lakini wapo baadhi
ya baadhi ya Viongozi na wanasiasa wachache wamekuwa wakipinga mageuzi hayo
pasipo na kutoa hoja za msingi.
“Mageuzi yanayoendelea kufanywa
hayatakuwa na mwisho, Serikali ya Awamu ya Tano na Watendaji wote tunaomsaidia
Rais John Pombe Magufuli tumedhamiria kuleta mapinduzi ya kweli kwa kuboresha
huduma za msingi kwa wananchi na tutapokea maoni na ushauri lakini kamwe
haturudishwi nyuma na Viongozi na watendaji wanaopinga mageuzi haya” alisema
Dkt. Abbasi.
Akitolea mfano Dkt. Abbasi alisema
mara baada ya Serikali kutangaza dhamira ya kuanzisha mradi wa kihistoria wa
kufua umeme wa Stiegler’s Gorge uliopo Wilayani Rufiji mkoani Pwani wapo baadhi
ya wanasiasa na Viongozi wamekuwa wakipinga mradi huo kwa kigezo cha uharibifu
wa mazingira ya eneo hilo, jambo ambalo lililenga kupeleka taswira hasi kwa
wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Anasema mageuzi mengine yaliyofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na ujenzi wa ukuta katika machimbo ya
madini ya Tanzanite, ambapo kutokana na hatua hizo katika kipindi cha mwezi
Julai hadi Novemba Serikali imeweza kukusanya mapato ya kiasi cha Tsh Milioni
890.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema
katika kuelekea katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi, Serikali ya Awamu ya
Tano imeendelea kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na kuweka
mfumo imara wa usimamizi wa fedha za umma ikiwemo makusanyo ya kodi, hatua
inayoiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kutekeleza sera
na programu mbalimbali ikiwemo sera ya elimu bure katika ngazi za elimu ya
awali, msingi na sekondari, ambapo Serikali imekuwa ikitoa Tsh Bilioni 23 kila
mwezi kwa ajili ya gharama za uendeshaji wake.
Akifafanua zaidi alisema kutokana na
kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji wa kodi, Serikali imeweza kufanya mageuzi
makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii ikihusisha afya, maji, barabara
pamoja na ununuzi wa ndege mpya nne za Serikali na hivyo kufufua upya huduma za
Shirika la ndege Nchini (ATCL) ambazo zilisimama kwa kipindi kirefu.
Akianisha mafanikio ya ATCL, Dkt.
Abbasi anasema moja ya mageuzi makubwa yaliyofikiwa kwa sasa na shirika hilo ni
pamoja na ongezeko la abiria kutoka abiria 3000-4000 kwa mwezi ambapo kwa sasa
wateja wanaotumia Ndege za Shirika hilo wamefikia 30,000 kwa mwezi.
“Mpaka sasa tuna ndege nne za
Serikali, na mwezi Desemba tutapokea ndege nyingine 2 aina ya Airbus na mwakani
(2019) mwezi Oktoba tutapokea ndege nyingine 1 na kuzifanya ndege mpya za
Serikali kufikia saba, na hivyo kufanya sekta ya uchukuzi kuwa katika
mabadiliko makubwa ya utendaji na uendeshaji” alisema Dkt. Abbasi.
No comments:
Post a Comment