MSHAMBULIAJI
wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Emmanuel Okwi amechaguliwa kuwa Mchezaji
Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
Okwi
anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda
wenzake wawili, Yahya Zayd wa Azam na Eliud Ambokile wa Mbeya City alioingia
nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya
Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo
ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Kwa
mwezi huo Oktoba timu 18 zilicheza michezo mitano kila moja, isipokuwa
Simba na Yanga zilizocheza mechi nne.
Katika
michezo hiyo minne ambayo Simba ilicheza, Okwi raia wa Uganda alitoa mchango
mkubwa kwa kupata pointi 12 kwa kushinda michezo yote na kumaliza ikiwa
nafasi ya pili, huku Okwi akifunga mabao 7 kwa mwezi huo, matatu akifunga
katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao
5-0.
Kwa
upande wa Ambokile naye alitoa mchango mkubwa kwa Mbeya City kufanikisha kupata
pointi 11 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare miwili na kushika
nafasi ya nane katika msimamo, akifunga mabao manne.
Kuhusu
Zayd alitoa mchango mkubwa kwa Azam akifunga mabao matatu katika michezo mitano
ambayo Azam ilicheza ikishinda yote na kupata pointi 15 ikishika nafasi ya
kwanza.
Pia
Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha wa Azam FC, Han Pluijm kuwa Kocha Bora wa
mwezi Oktoba akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa
Mbeya City, Ramadhan Nsazwarimo.
Pluijm
aliiongoza timu yake kupata pointi 15 baada ya kushinda michezo yote mitano
iliyocheza na kushika nafasi ya kwanza, huku Aussems akiiongoza Simba kushinda
michezo yote minne iliyocheza hivyo kupata pointi 12 na kushika nafasi ya pili,
wakati Nsazwarimo alipata pointi 11 akishinda michezo mitatu na kutoka sare
mitatu akiiwezesha timu yake kupanda hadi nafasi ya nane.
Bodi
ya Ligi Kuu Tanzania Bara ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi,
huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo
msimu wa mwaka 2017/2018 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada
mbalimbali, ambapo kwa ushindi huo Okwi atazawadiwa tuzo, king’amuzi kutoka
Azam na Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.
Washindi
wengine wa tuzo hiyo kwa msimu huu na miezi yao katika mabano ni mshambuliaji
wa Simba, Meddie Kagere na mshambuliaji wa Mbeya City Eliud Ambokile.
Kwa
upande wa makocha walioshinda tuzo hizo kwa msimu huu ni Amri Said wa Mbao FC
aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa Agosti na Mwinyi Zahera wa Yanga aliyeshinda
tuzo ya Kocha Bora wa Septemba.
No comments:
Post a Comment