Monday, November 19, 2018

WAFUGAJI WATEMBEZA KIPIGO KIJIJI CHA NYANI KISARAWE.

Na Omary Mngindo, Kisarawe

WAFUGAJI jamii ya Wasukuma Kitongoji cha Kimeremeta Kijiji cha Nyani Kata ya Mafizi Kisarawe Pwani, wametembeza kichapo na kuvunja mlango nyumbani kwa Mohamed Rashid, kisa kizuiliwa wasiingize mifugo shambani.

Tukio hilo limetokea Nov 13 katika Kitongoji hicho baada ya wafugaji hao kuingiza mifugo kwenye shamba ambalo limeshalimwa kwa trekta wakisubili mvua tayari kwa kupanda.

Kitendo hicho kinachoelezwa ni cha kinyama, watuhumiwa hao baada ya kuzuiliwa wasiingize mifugo, walianza kumshambulia mdogo wake Rashid kwa fimbo sehemu za mwili, alipofika mwenyewe nae alipigwa mikononi na mgongoni.

"Usiku wa kuamkia Nov 14 alfajili walikuja wakavunja mlango kama mnavyouona, wamebomoa ukuta wa nyumba, wamechukua fedha kisha wakasema watakuja tena usiku kuendeleza vipigo," alisema Rashid.

Nae Amina Salum mke wa Rashid alisema kwamba usiku wa kuamkia Nov 15 walilazimika kukimbia nyumba wakihofia vipigo kwani wafugaji hao walifikia kutamka wataua mtu, kwanini wanakatazwa wasiingize mifugo.

"Tumelala mbali na Kitongoji chetu kuhusuru maisha yetu kwa kuhofia maisha yetu, walipomaliza kufanya fujo kuna mmoja wa wananchi waliwaomba wasifanye fujo ndio wakaondoka," alisema Amina.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyani Selemani Mnandi alisema kuwa baada ya kutokea hali hiyo, aliwasiliana na Polisi Kituo cha Mzenga ambapo walifika na kuwachukua aliyejeruhi na kujeruhiwa kwa ajili ya mahojiano.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.


No comments:

Post a Comment