SERIKALI imetoa siku nne kwa wanunuzi
wote 35 waliojiandikisha kununua korosho wawe wamepeleka barua katika Ofisi ya
Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini
watazichukua.
“Hivyo wanunuzi waliojiandikisha
wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi
kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa
10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24.”
Hayo yamesemwa leo (Ijumaa, Novemba
9, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu
ununuzi wa zao la korosho, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.Baada ya kupita
siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua
zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa
ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho imesema haitakubaliana nacho.
“Mwenye nia ahakikishe katika siku
hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwani ofisi yangu
ipo wazi saa 24 wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na
kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo Serikali haitoruhusu kampuni yoyote
kununua korosho tena.”
Waziri Mkuu amesema kwenye msimu wa
ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia kusuasua kwa minada, ambapo
Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho katika kikao kilichoongozwa na Rais
Dkt. John Magufuli ambapo walikubaliana kununua kwa bei inayoanzia sh 3,000 na
kuendelea.
“Mjadala ulikuwa wa wazi na
wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia sh. 3,000,
hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada imeendelea kusuasua na
hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo sana. Sisi tunaiona hali hii
kama mgomo baridi ambao si sawa sawa sana kwani malengo yetu sisi na sekta
binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri.
Hali hii haifurahishi kwa sababu
Serikali imedhamiria kuboresha mazao yanayolimwa na wakulima kwa kuwasaidia
kuanzia katika hatua za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na
masoko ili waweze kunufaika na kilimo na kupata tija katika mazao hayo.”Waziri
Mkuu amesema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo Serikali ilifanya jitihada za
kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ambayo
bado inatosha kumlipa mkulima sh 3,000.
Hatua hiyo imekuja baada ya zao la
korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya chini na idadi ya wanunuzi kuwa ya
chini licha ya uzalishaji wa mwaka huu kuwa mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka
jana.Amesema msimu wa mwaka jana uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na
mwaka huu zinatarajiwa tani zaidi ya 200,000 hivyo wafanyabiashara wanao uwezo
kununua korosho zilizopo.
Hata hivyo Serikali imewataka
wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na
watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment