Friday, November 23, 2018

MABORESHO YA MWONGOZO WA UTOAJI HUDUMA ZA KIELIMU KUSAIDIA WENYE UONI HAFIFU

Mwanasheria wa Shirika la kimataifa la kutetea haki za watu wenye ualibino (Under The Same Sun) nchini Tanzania, Bw. Madulu William, akifafanua jambo wakati wa warsha hiyo ya kupitia na kurekebisha mwongozo wa utoaji elimu kwa wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu iliyofanyika Novemba 22 na 23, 2018 Dodoma Hoteli Jijini Dodoma.
........................................

Maboresho ya mwongozo wa utoaji huduma za kielimu kusaidia kutatua changamoto za mazingira ya kielimu kwa wenye ulemavu wa ngozi (ualbino) na uoni hafifu.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Wenye Ulemavu Bi. Magreth Malunda alisema kuwa Serikali imekuwa ikisirikiana kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za wenye ualbino Duniani (Under the Same Sun) pamoja na wadau mbalimbali katika harakati za kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili wanafunzi wenye ualbino, hususan suala la uoni hafifu.

“Mwongozo huo utakuwa ni nyenzo muhimu katika utoaji huduma za kielimu kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu hapa nchini, maana utasaidia kutambua mahitaji yao muhimu,” alisema Malunda.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Shirika la Under the Same Sun, Bw. Madulu William alisema kuwa matatizo wanayokumbana nayo wanafunzi wenye ualbino ni pamoja na kushindwa kusoma vizuri mitihani na mwandiko ubaoni wanapokuwa madarasani, hivyo kusababisha wengi wao kushindwa kufanya vizuri katika masomo.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha mwongozo unakuwa na njia bora ya kuwawezesha walimu kujua jinsi watakavyoweza kuwajumuisha wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu wanapata fursa sawa kama walivyo wanafunzi wengine,” alisema William.

Naye Meneja Mradi Jumuishi wa Watu wenye Ualbino (KCBRP) Bw. Florence Rugemalira alisema kuwa ni vyema jamii ikaelimishwa juu ya watu wenye ulemavu ualbino na uoni hafifu ili waweze kutambua kuwa wanaouwezo kama wengine katika kupata elimu.

Warsha hiyo imehusisha Wizara mbalimbali na wadau wanaofanya kazi kwa ukaribu na watu wenye ualbino ambapo walikutana kwa siku mbili kupitia na kurekebisha mwongozo wa utoaji elimu kwa wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu.
Mratibu wa Elimu Maalum Kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Janneth Mwocha akionesha kitabu cha mwongozo wa utoaji wa huduma za kielimu kwa Watoto wenye ulemavu wa Ngozi.

Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Oliver Njogopa, akichangia mada wakati wa warsha hiyo.

Mwanasheria wa kujitegemea Bi. Neema Ndemno akiwasilisha mada kwa washiriki waliohudhuria warsha hiyo iliyofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika warsha hiyo.Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika warsha hiyo.

No comments:

Post a Comment