Tuesday, November 6, 2018

AMANA BANK KUWEZESHA MADEREVA WA TAXI KUMILIKI GARI ZAO KUPITIA TAXIFY.

 Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa, (kulia) wakipeana mikono na kubalishana hati za mkataba na Meneja wa Taxify Tanzania, Remmy Eseka.
 
Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa, (kulia)akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Serena Hoteli jijini Dar es Salaam, kushoto ni Meneja wa Taxify Tanzania, Remmy Eseka.
...............................................
 
Amana Bank Tanzania imekuja na njia mpya ya mikopo isiyo na riba ambapo mara hii watatoa mikopo kwa madereva wa Taxi ili waweze kumiliki Gari zao.

Akizungumza wakati wa kutiia saini mkataba wa makubaliano kati ya Amana Bank na Kampuni ya usafirishaji ya Taxify Tanzania, Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa alisema vijana wengi wamkuwa hawana vigezo vya kukopesheka kwenye Taasisi za kifedha hali inayopelekea kushindwa kufikia malengo yao.

Alisema Amana Bank, ni Benki inayokwendaa na wakati kwa kuangalia changamoto zilizopo kwenye jamii na kuzitafutia ufunmbuzi ikiwa ni njia moja wapo ya kuwajali wateja wake na jamii kwa ujumla.

Dasu aliongeza kwa kusema kuwa, kwa sasa Benki hiyo kwa kushirikiana na Kampuni ya usafirishaji ya Taxify itawawezesha madereva kupata mkopo wa magari ambayo wakimaliza mikopo yao magari hayo yatabaki kuwa ya kwao.

Alisema Amana Bank, kama Benki inayoendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kiislamu hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kuifanya Benki hiyo kuwa kiongozi katika kutoa huduma za kibunifu zinazolenga kuinua jamii kiuchumi.

Aidha, alisema mikopo hiyo itatolewa kwa vikundi, hivyo madereva wanapaswa kuunda kikundi cha madereva kumi ambao watajidhamini wenyewe.

Alifafanua kuwa, Dereva atatakiwa kuweka amana isiyopungua asilimia kumi 10% ya thamani ya Gari anayohitaji kuwezeshwa ili kiasi hicho cha asilimia kumi kiwe kama dhamana mapaka atakapomaliza kufanya marejesho ya mkopo wake.

Sambamba na hilo, Dasu alisema kuwa, Dereva atatakiwa kuweka akiba kiasi cha shilingi elfu kumi na tano 15,000 kwa wiki ambayo ndiyo itakayomsaidia kukusanya kiurahisi marejesho yake.

Hata hivyo alisisitiza kuwa, moja ya sifa za kupata mkopo huo ni Dereva kuwa na Akaunti Amana Bank ili kujenga ukaribu kati ya Amana Bank na mteja husika.

Alisema miongoni mwa vigezo vitakavyozingatiwa katika kutoa mkopo huo ni pamoja na Dereva kuwa na uzoefu wa kutosha na rekodi nzuri katika kazi yake na jamii kwa ujumla.

Amana Bank, ni Benki pekee hapa Tanzania inayotoa huduma zake kwa kuzingatia sheria ya kiislamu katika miamala ya kifedha haibagui mteja kwa dini yake na kwamba hata mikopo hiyo haitabagua Dereva kwasababu ya dini yake bali vigezo ndio kitu pekee kitakachomuwezesha mtu kupata mkopo huo usiokuwa na riba.

Alisema kuwa Amana Bank katika kutua huduma zake mwaka huu wa 2018 inatimiza miaka saba ambapo katika kipindi chote hicho imeweza kuwa na wateja wa dini zote na kushirikiana nao katika biashara kwa karibu zaidi jambo ambalo wateja wenyewe wanaotumia Amana Bank wamethibisha namna wanavyofarijika kuhudumiwa na Amana Bank.

Hata hivyo Dasu alifafanua kuwa, katika sheria ya kiislamu imeharamishwa riba na imehalalishwa biashara kwahiyo Amana Bank itanunua magari na kuyauza kwa faida kidogo kwa njia ya mkopo.
Alisema katika uislamu hakuna biashara ya fedha kwa fedha bali ni lazima biashara ifanyike kwa kubadilishana fedha na kitu ambapo hilo ni katika mambo yanayozingatiwa na Amana Bank ili kuepuka kupokea na kutoa riba.

Akizungumzia sifa za ujumla zitakazomuwezesha Dereva kuingi kwenye mkopo huo alisema Kampuni ya Taxify ndio itakayowatahini madereva kulingana na sifa wanazotaka na baadae kuwasilisha majina ya madereva hao kwa Amana Bank.

Dasu alimalizia kwa kusema kuwa, kitendo hicho cha kutoa mikopo kwa madereva kitawasidia katika kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuongeza pato la serikali litakalotokana na ulipaji wa kodi.

Akizungumza mara baada ya kutia saini mkataba wa makubaliano, Meneja wa Taxify Tanzania, Remmy Eseka alisema anaishukuru Amana Bank kwa kuanzisha wazo hilo ili kuwasaidia vijana kiuchumi.

Alisema ni vigumu kwa Taasisi za kifedha kumuamini mtu kumpa mkopo bila ya kuwa na dhamana inayolingana na kitu anachokopeshwa lakini kwa Amana Bank inawezekana.

Alisema ushirikiano huo kati ya Amana Bank na Taxify umekuja kufuatia changamoto zinazowakabili madereva wengi wanaofanya kazi na Taxify kwakuwa madereva wengi hawamiliki magari yao binafsi.

Remmy alisema madereva wa Taxify kwa sasa asilimia 40 ya kipato chao kinakwenda kwa wamiliki wa magari jambo ambalo linawarudisha nyuma kiuchumi.

Akizungumzia utoaji wa huduma wa Taxify alisema Taxify ipo katika nchi 25 duniani ambapo hapa nchini ipo katika miji mitatu tu ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.

Alisema katika kutuo huduma ya usafiri Taxify inatumia Gari za kawaida, Bajaji na Bodabodo.
 
Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa, wakitiliana saini na Meneja wa Taxify Tanzania, Remmy Eseka kuhusu utoaji wa mikopo ya magari isiyokuwa na riba  kwa madereva wa Taxify Tanzania. 
Meneja wa Masoko wa Amana Bank, Jamali Issa (kushoto) akiwaongoza waandishi wa Habari katika kuuliza maswali kwenye hafla hiyo fupi ya kutiliana saini mkataba wa makubaliano kati ya Amana Bank na Taxify Tanzania uwawezesha madereva wa Taxify Tanzania kukopeshwa magari bila ya riba, wanaotia saini mezani ni Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa, (kulia) na Meneja wa Taxify Tanzania, Remmy Eseka.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakishuhudia na kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment