Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewasimamisha kazi watumishi watatu wa
sekta ya ardhi katika halmashauri ya Jiji la Arusha kwa tuhuma ya
kushirikiana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo.
Aidha, Lukuvi ameagiza
maofisa hao waliosimamishwa kazi kutokanyaga katika eneo la ofisi za Jiji mpaka
hapo uchunguzi utakapofanyika na maamuzi dhidi ya tuhuma zao yatakapotolewa.
Lukuvi alichukua uamuzi
huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Jiji la Arusha jana
kufuatia kuwepo tuhuma nyingi za matapeli ya viwanja kushirikiana na
baadhi ya maofisa wa ardhi wasiokuwa waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki
halali wa viwanja.
Maafisa ardhi
waliosimamishwa kwa tuhuma hizo za kushirikiana na matapeli kudhulumu viwanja
kwa wamiliki halali katika jiji la Arusha ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na
Zawadi Mtafikikolo.
Mbali na kusimamishwa kazi
kwa watumishi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza maafisa
Ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na
watumishi hao wasipatiwe huduma katika masuala yoyote ya ardhi kufuatia
kuonekana kujihusisha na mipango ya utapeli wa viwanja kwa kushirikiana na
baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi katika jiji la Arusha.
Katika ziara yake hiyo ya
kushtukiza pamoja na kuelezwa na Afisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha Dicley
Nyato uwepo wa watumishi wawili Lassen na Zawadi huku Elizabeth akiwa katika
likizo ya uzazi, watumishi hao walipotea ghafla ofisini bila taarifa mara baada
ya kuelezwa wanahitajika kwa waziri na hata pale walipopigiwa simu za
mkononi hazikupatikana.
Kwa mujibu wa Lukuvi,
watumishi hao wa sekta ya ardhi katika jiji la Arusha wamekuwa na mawasiliano
ya mara kwa mara na matapeli wa viwanja katika jiji hilo jambo linalotia
mashaka utendaji wao wa kazi na kubainisha kuwa maafisa hao wamekuwa na
tabia ya kufuatilia kesi zilizopo katika Mabaraza ya Ardhi kwa nia ya
kuwasaidia matapeli.
Kufuatia kadhia hiyo,
Lukuvi ameagiza kuanzia sasa hati zote za wito wa Mahakama nchini kusainiwa na
Afisa Ardhi Mteule au Msajili wa Hati ama Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda
na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi lazima
afahamishwe uwepo wa kesi husika.
“Kuanzia sasa summons zote
zipokelewe na Maafisa Ardhi Wateule, Makamishna au Wasajili wa Hati wa Kanda na
watumishi wengine wasipokee wala kujihusisha” alisema Lukuvi
Lukuvi alisema matapeli wa
viwanja wamekuwa wakifungua kesi katika Mabaraza ya Ardhi dhidi ya
wamiliki halali na wakati mwingine matapeli hao hawawafahamu hata
wamiliki lengo lao likiwa kuwakatisha tamaa pale kesi inapochukua muda
mrefu hasa ikizingatiwa baadhi ya wamiliki hawana uwezo wa kuweka mawakili na
hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao.
Alisema, tabia hiyo
haiwezi kuvumiliwa na kusisitiza kuwa mtandao wote wa matapeli wa viwanja
katika jiji la Arusha ataukomesha kama alivyofanya katika jiji la Dar es Salaam
ambalo huko nyuma lilishamiri sana kwa tabia hiyo ili kusaidia haki za
wanyonge.
Kwa upande wake Afisa
Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha Dicley Nyato alimueleza waziri Lukuvi kuwa
wamekuwa wakisumbuliwa sana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo na wakati
mwingine matapeli hao huwashitaki lengo likiwa kujipatia viwanja kwa njia ya
udanganyifu na kuviuza.
Lukuvi alifanya ziara hiyo
ya kushtukiza katika ofisi za jiji Arusha akitokea wilayani Babati mkoa wa
Manyara ambako huko aliweza kutoa faraja iliyopotea kwa muda mrefu kwa wananchi
wa vijiji vya Singu na Endasago kwa kuamuru kubaki katika maeneo yao
kufuatia mgogoro wa muda mrefu wa takriban miaka hamsini kati ya wana kijiji na
wamiliki wa mashamba ambao ni kampuni za Agric Tanzania Ltd na Endasago
Co Ltd.
No comments:
Post a Comment