Friday, November 23, 2018

WADAU WA KILIMO WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizundua Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
............................................


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Mageuzi ya kilimo nchini Tanzania yanapaswa kutiliwa mkazo na wadau wote wa sekta ya kilimo wakiwemo wananchi, wadau wa maendeleo na serikali kwa ujumla.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 23 Novemba 2018 wakati akizundua Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro.

Mhe Hasunga alisema kuwa Sekta ya kilimo imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwani imekuwa ikichangia kwa Kiasi kikubwa katika kutoa ajira, kuchangia karibu nusu ya mauzo yote ya nje na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta fedha za kigeni.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kuweka juhudi zake katika kuwezesha sekta ya kilimo kwa kufanya mabadiliko mbalimbali ya kisera yenye lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa sekta ya kilimo kukua.

Pia serikali imezindua Mpango wa pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP II) wenye lengo la kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na inachangia katika maendeleo ya uchumi na kuongeza kipato cha mkulima mdogo.

Mhe Hasunga amesisitiza kuwa mpango wa SAGCOT ulianza toka mwaka 2010 kwenye mkutano wa Baraza la Uchumi la Dunia kwa Africa (World Economic Forum of Africa WEF-A) uliofanyika Jijini Dar es Salaam ambao utatekelezwa kwa miaka 20 mpaka mwaka 2030.

Alisema mpango wa SAGCOT umepangwa kutekelezwa kwa awamu katika mgawanyo wa kongani sita. Kongani hizo Ihemi, Mbarali, Kilombero, Rufiji, Ludewa na Rukwa hivyo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ameitaka SAGCOT kuongeza ufanisi na weledi katika kukamilisha kongani zote sita kama mtazamo ulivyo.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akizungumza katika hafla hiyo alisema kuwa wizara ya kilimo ina ziada ya kutosha kwenye mazao ya chakula huku akisisitiza kuwa mkakati wa kutafuta masoko unaendelea ili kuwanufaisha wakulima nchini.

Alisema nchi ina fursa kubwa kwenye sekta ya kilimo hivyo wananchi wanapaswa kujikita zaidi katika kilimo kwani ndio sehemu pekee yenye uwezo wa kuwanufaisha wananchi wengi kwa wakati mmoja.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa alisisitiza kuwa SAGCOT inapaswa kufanya haraka katika kuanzisha kongani ya nne na hatimaye mpaka ya sita ili kuajiri vijana na wananchi wengi.

Ameongeza kuwa wataalamu wengi wa kilimo wamenufaika na elimu nchini lakini ajira zimekuwa chache hivyo kuongezwa kwa kongani nyingine ajira zitaongezeka na wananchi wengi watanufaika na kipato kwa ajili ya maendeleo ya kaya na Taifa kwa ujumla wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Ndg Geofrey Kirenga alieleza kuwa malengo ya mpango wa SAGCOT yanakwenda sambamba na Dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025, mpango wa maendeleo wa miaka 5, utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo ya kilimo (ASDP II) na mpango wa uwekezaji kwenye kilimo kwa ajili ya usalama wa chakula na lishe (TAFSIP) ambao unatumika kutekeleza programu kabambe ya maendeleo ya kilimo barani Afrika (CAADP).

Alitaja lengo kuu la mpango wa SAGCOT kuwa ni kuhakikisha kuwa kilimo katika maeneo ya SAGCOT kinachangia katika kuongeza tija, kuhakikisha kuna usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kuhakikisha wakulima wadogo wanatoka kwenye kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha kibiashara na kuhakikisha mazingira yanatuzwa kwa maendeleo endelevu ya kilimo.
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizundua Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 
 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila akitoa ushuhuda toka kongani ya Ihemi na Mbarali wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Ndg Geofrey Kirenga akieleza mwelekeo wa jinsi SAGCOT itakavyoendesha shughuli zake wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 
 
Muwakilishi wa Benki ya Dunia Bi Emma Isinika Modamba akiwasilisha taarifa fupi toka kwa wadau wa Maendeleo wanaowezesha mpango wa SAGCOT wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 

No comments:

Post a Comment