Wednesday, October 31, 2018

DK. KALEMANI -TUTAHAKIKISHA TUNADHIBITI CHANGAMOTO YA KUKATIKA KWA UMEME VIWANDANI

WAZIRI wa Nishati Dk Merdad Kalemani ,wakati alipotembelea maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayoendelea viwanja vya sabasaba, Pichandege Kibaha Pwani, ikiwemo banda la shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC), na kuelekeza kutangaza vituo vinavyosambaza gesi asilia. (picha na Mwamvua Mwinyi) 
.......................................................

NA MWAMVUA MWINYI, PICHANDEGE 

WAZIRI wa Nishati Dk Merdad Kalemani ,amesema umeme ni injini ya viwanda hivyo watahakikisha changamoto ya umeme kukatika kwenye viwanda nchini inadhibitiwa kwani hali hiyo haifai viwandani .

Aidha amewataka wawekezaji waendelee kujenga viwanda kwani umeme uko wa kutosha ambapo kwa sasa kuna akiba ya umeme wa ziada wa megawati 148.

Aliyasema hayo jana mjini Kibaha alipotembelea maonyesho ya viwanda kwenye viwanja vya Sabasaba vilivyopo Picha ya Ndege wilayani Kibaha .
Hata hivyo aliielekeza TPDC kuvitangaza vituo vya gesi asilia ili wananchi wapate uelewa juu ya gesi hiyo. 

“Sera yetu kwa sasa tunataka sisi tutangulie na viwanda ndiyo viufuate na siyo viwanda kuwafuata kwani kufanya hivyo tutakuwa tumewaondolea kero ya kufuatailia masuala ya umeme,” alisema Dk. Kalemani.

“Ndiyo maana tunajenga miradi mikubwa ya uzalishaji umeme kama ule wa Rufiji hydro power unaotokana na maji utakaozalisha megawati 2,100 na Rumakali utakaozalisha megawati 358 na ule wa gesi wa Kinyerezi kuhakikisha viwanda havikwami”

“Nimetembelea na kukagua mabanda na nimeona mahitaji na kati ya mabanda 17 ambayo ni ya viwanda  wana sema umeme siyo tatizo licha ya sehemu kama mbili wamelalamika kuwa umeme kwao ni changamoto”

Alibainisha  wameona kuna mahitaji makubwa ya umeme kwa ajili ya viwanda hasa katika maeneo ya Bagamoyo Kibaha na Chalinze viwanda vinajengwa kila siku hivyo wilaya na Tanesco waainisheni maeneo ambako vitajengwa viwanda ili miundombinu ipelekwe .

Aliwataka wataalamu wa Tanesco kuhakikisha wanaondoa changamoto ndogo ndogo zilizopo .

Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alisema watayaanisha maeneo hayo ambayo yametengwa kwa ajili ya kuanzishwa viwanda ili huduma hiyo ipelekwe  kabla ya ujenzi wa viwanda kuanza.

Alisema wilaya yake ina viwanda vingi hivyo nishati ya umeme wa uhakika ni muhimu kuwepo ili kuondokana na changamoto hizo za ukosefu au kukatika kwa umeme.

MFANYABIASHARA AKRAM AZIZI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MASHTAKA 75 IKIWEMO UTAKATISHAJI FEDHA.


MDOGO wake mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz, anayetambulika kwa jina la Akram Aziz leo Oktoba 31, 2018 amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka 75, yakiwemo mashtaka 71 ya kukutwa na silaha za aina mbalimbali pamoja na kutakatisha fedha zaidi ya Dola za Marekani 6494.
........................................

MDOGO wake mfanyabishara maarufu nchini Rostam Aziz, anayetambulika kwa jina la Akram Azizi leo Oktoba 31, 2018 amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka 75 yakiwemo ya mashtaka 71 ya kukutwa na silaha za aina mbali mbali pamoja na kutakatisha fedha za Marekani dola 9018.

Mshtakiwa huyo anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 82/2018 pia anakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh. milioni 108, risasi 6496 pamoja na kosa la kukutwa na nyama ya Nyati kilogramu 65 yenye thamani ya Sh.milioni 4.35 bila kuwa na kibali.

Ambapo anadiwa kulitenda kosa hilo Oktoba 30,2018  katika eneo la Oysterbay Kinondoni Dar es Salaam.

Mshtakiwa amesomewa mashtaka yake na jopo la mawakili wawili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi aliyekuwa akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Augustine Rwizile.


Akisoma hati ya mashtaka hayo leo mahakamani hapo Wakili Kadushi amedai katika shtaka la utakatishaji mshtakiwa anadaiwa kati ya Juni 2018 na Oktoba 30, 2018 katika eneo la Oyesterbay, mtuhumiwa alijipatia jumla ya dola za Marekani 9018 huku akijua  fedha ni zao la kosa tangulizi la kujihusisha na biashara haramu ya nyara za Serikali pamoja na kukutwa na silaha bila kibali.


Katika mashtaka ya kukutwa na risasi, mshtakiwa anadaiwa kuwa Oktoba 30 mwaka 2018 (Jana) huko Oyesterbay, alikutwa na risasi 4092 bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mrajisi wa kibali cha silaha.

Pia imedaiwa Oktoba 31, 2018 (leo) huko huko Oyesterbay mshtakiwa alikutwa na risasi 2404 bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mrajisi wa silaha.

Baada ya kusomewa makosa hayo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote kwa sababu Mahakama hiyo  haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mshtaka, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hivyo mshtakiwa amerudishwa rumande.Kesi imeahirishwa hadi November 11,2018.


KAMATI YA KATIBA NA SHERIA YAKUTANA NA WIZARA YA FEDHA

Naibu waziri wa Elimu,  Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mheshimiwa Tate William Ole-Nasha  akitoa Taarifa ya Wizara ya Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu Mkakati wa Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma. Mheshimiwa Ole-Nasha alimwakilisha Waziri wa Katriba na Sheria Prof. Paramagamba Kabudi.
 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mheshimiwa Najima Giga akifurahi jambo wakati kamati hiyo ilipokutana na Wizara ya Katiba na Sheria kupokea na kujadili  Taarifa ya Wizara ya Wizara hiyo kuhusu Mkakati wa Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Kushoto kwa Mheshimiwa Giga ni katibu wa Kamati hiyo Ndg. Kagisa.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakimsikiliza Naibu waziri wa Elimu,  Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mheshimiwa Tate William Ole-Nasha  akitoa Taarifa ya Wizara ya Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu Mkakati wa Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka leo katika Ofisi za Bunge, Jijini Dodoma.  
 (PICHA NA OFISI YA BUNGE.)