Mkuu
wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus E. Mwangela akikagua shughuli za
wachimbaji wadogo wa madini Wilayani Songwe ambapo ameagiza Ofisi ya Madini
kuwatembelea wachimbaji na kuwapa elimu kuhusu sheria na taratibu za uchimbaji
wa madini.
...................................
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus E.
Mwangela akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wamesuluhisha mgogoro
baina ya wakazi wawili wa kijiji cha Saza Wilaya ya Songwe kuhusu eneo la
uchimbaji wa madini.
Brig. Jen. Mwangela amesema Suzan Karan amebainika
kisheria kuwa ni mmiliki halali wa eneo lililokuwa likigombewa kwa kuwa ana
leseni halali huku Elimbotwa Naftari ambaye hana leseni na amekuwa akidai
umiliki wa eneo hilo amebainika kuendesha shughuli za uchimbali kinyume na
sheria.
“Sheria inamtambua Suzan kama mmliki halaki
kwakuwa anayo leseni na amefuata taratibu na sheria za uchimbaji madini,
tunashauri Elimbotwa kama atataka kuendelea kuchimba madini katika eneo hilo
basi akubaliane na Suzan kufanya naye kazi”, amesisitiza.
Ameongeza kuwa serikali za vijiji hazina mamlaka
ya kuwapa vibali vya uchimbaji wawekezaji wa madini bali leseni na vibali vyote
vya uchimbaji wa madini hutolewa na ofisi za madini Wilaya, mkoa au kanda, hii
inatokana na kuwa serikali ya kijiji ilimtambua Elimbotwa kama mmiliki wa eneo
la uchimbaji kinyume na sheria.
Kwa upande wake Elimbotwa amesema anamtambua Suzan
kama mmliki halali wa eneo walilokuwa wakiligombania isipokuwa sasa anadai
fidia ya zaidi ya shilingi milioni 190 ikiwa ni gharama ya vitu alivyowekeza
kabla ya Suzan kupewa leseni ya eneo hilo.
Naye Suzan ameupongeza uongozi wa Mkoa kwa kutoa
suluhu ya mgogoro huo kutokana na kuwa ulipelekea kusimama kwa shughuli za
uchimbaji na hivyo kuathiri uchumi wake.
Aidha Brig. Jen. Mwangela ameagiza Takukuru, TRA
na taasisi zinazoweza kufanya ukaguzi, zihakiki madai ya Elimbotwa kama ni
halisi ili Suzan aweze kuyalipa.
Imeelezwa kuwa baadhi ya
migogoro ya haki ya kumiliki maeneo ya uchimbaji wa madini mkoani Songwe
inasababishwa na ukiukwaji wa taratibu na sheria za madini unaofanywa na baadhi
ya watendaji na wachimbaji.
No comments:
Post a Comment