Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza katika
mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ofisini kwake jijini
Dodoma kuhusiana na zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka Dar es
Salaam kwenda Dodoma.
.......................................
Serikali imepiga marufuku Watumishi
wa Umma waliohamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba
uhamisho wa kurejea jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alipokuwa
akifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusiana na
zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa,
Ofisi yake imekuwa ikipokea barua mbili au tatu kwa siku za watumishi
waliohamia Dodoma kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam kutokana na sababu
mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya wakati hospitali ya Rufaa ya Benjamin
Mkapa ina vifaa vya kisasa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za matibabu kwa
watumishi hao.
Dkt. Ndumbaro amefafanua kwamba,
kabla ya watumishi kuhamia Dodoma, Serikali ilitoa maelekezo kwa waajiri
kuwasilisha orodha ya watumishi wenye matatizo ya kimsingi ili wabaki kwenye vituo
vya kazi vilivyopo Dar es Salaam wakiendelea kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, baadhi
ya watumishi waliohamia Dodoma, wamegeuza uhamisho huo kuwa mradi wa
kuwaingizia kipato kwani mara baada ya kuripoti Dodoma, ndani ya kipindi kifupi
wanaomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam.
Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa,
kutokana na suala hilo, Serikali imetoa Waraka wa Barua wenye Kumb. Na. CAC
228/257/01/A/53 wa tarehe 25 Septemba, 2018 kuhusu Uhamisho wa Watumishi
Waliohamia Dodoma Kutekeleza Uamuzi wa Serikali Kuhamishia Makao Makuu ya Nchi
Dodoma ambao unazuia mtumishi aliyehamishiwa Dodoma kwa gharama za Serikali
kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam mpaka atimize miaka mitatu katika
kituo cha Dodoma.
Watumishi wa Umma kuhamia Dodoma ni
utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa
maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa.
No comments:
Post a Comment