Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Maafisa
Afya wa mikoa nchini, wakati alipofungua rasmi mkutano wa maafisa hao kwenye
ukumbi wa mipango jijini Dodoma Novemba 23, 2018.
.....................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote nchini, vya
binafsi na vya umma ili viendelee kutoa elimu ya juu yenye ubora na viwango
vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa
na kimataifa.
Amesema suala hilo ni muhimu likapewa uzito
unaostahili kwani wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika
jamii ya Watanzania na pia ya kimataifa, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa
ikazingatia ubora na viwango vinavyostahiki.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba
23,2018) kwenye mahafali ya tisa ya chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha
Tanzania Kampasi ya Chifu Mazengo, Dodoma yaliyofanyika kwenye ukumbi wa CCM.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na
Rais Dkt. John Magufuli, inatambua na kuthamini mchango wa Sekta Binafsi
hususan wa vyuo vikuu binafsi kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha
Tanzania, katika maendeleo ya elimu ya juu.
“Serikali inatambua mchango wa vyuo hivyo katika
kupanua fursa kwa Watanzania wengi kupata elimu ya juu, ambapo hadi sasa
udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwenye vyuo vikuu binafsi nchini ni
takriban asilimia 25 ya wanafunzi wote.”
Amesema Serikali inatambua mchango wa chuo kikuu
cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania katika kutayarisha watalaamu wa fani
mbalimbali. Aidha, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, chuo hicho kimetoa
wahitimu zaidi ya 10,000.
Amesema kati ya wahitimu hao wapo Wafamasia,
Wauguzi, Walimu wa Sayansi, Walimu wa Sanaa, Wataalamu wa Maabara, na
Wasimamizi na Waendeshaji wa fani mbalimbali kama Utawala, Masoko na Wahasibu,
mchango ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa Taifa
katika nyanja tajwa.
Waziri Mkuu amesema baadhi ya wahitimu watapata
ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa, hivyo Serikali
itaendelea kuunga mkono azma yao kama chuo kikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia,
utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na siyo watafuta kazi tu.
Akizungumzia kuhusuchangamoto zinazokabili sekta
ya elimu ya juu, amesema baadhi ya changamoto zinafanana katika vyuo vikuu
vyote nchini na pia zipo changamoto zinazokabili vyuo vikuu binafsi na wakati
mwingine zipo changamoto zinazohusu chuo kikuu kimoja kimoja.
Amesema moja ya changamoto kubwa katika elimu ya
Juu ni uhaba wa Wahadhiri wenye sifa stahiki ili kuendana na ongezeko la
wanafunzi wanaojiunga na vyuo vyao. “Nafahamu jitihada ambazo vyuo vikuu
binafsi vinafanya katika kuendeleza Rasilimali Watu wao na hasa katika eneo la
taaluma ili viwe na Wahadhiri na Maprofesa wa kutosha.”
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito vyuo vingine
binafsi nchini viwekeze katika eneo la kuendeleza Rasilimali Watu kwa bidii
zaidi na kwa upande wa Serikali, ipo mikakati mbali mbali ya kuajiri lakini pia
kusomesha wale waliopo kazini ili kufikia viwango vinavyokubalika Kitaifa na
Kimataifa.
Waziri Mkuu amesema changamoto nyingine
inayovikabili vyuo vikuu ni miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kama vile
mabweni na nyumba za watumishi, hivyo kusababisha baadhi ya
vyuo kushindwa kukidhi matakwa ya ithibati zao na kuzuiwa kufanya
udahili au kufungiwa kabisa.
“Ni kweli tunahitaji Watanzania wengi wapate elimu
ya juu kwenye vyuo vyetu vikuu. Hata ninyi wanafunzi, mngependa kupata elimu
iliyo bora itakayoweza kuwasaidia maishani na itakayowakomboa kifikra,
itakayowapa ujuzi na maarifa ya kupambana na changamoto za maendeleo. Kila
mmoja anataka elimu bora na si bora elimu.”
Waziri Mkuu amesema kuwa dhamira hiyo ndiyo
inayoifanya Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu kuhakikisha kuwa vyuo vyote
visivyokidhi matakwa ya ithibati yao haviendelei kutoa mafunzo ya aina yoyote.
“Nitoe rai kwa vyuo vikuu vyote vizingatie matakwa ya ithibati zao ili viweze
kutoa elimu iliyo bora itakayokidhi matamanio ya Watanzania na ushindani wa
soko la ndani na nje.”
Kuhusu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha
Tanzania ambacho kimeomba kuruhusiwa kufanya udahili baada ya kufungiwa, Waziri
Mkuu amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako kujiridhisha iwapo chuo hicho kimekidhi vigezo kabla ya kukipa
kibali cha kudahili wanafunzi wapya.
No comments:
Post a Comment