Mkurugenzi Mtendaji wa
Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud, akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika katika Tawi la Nyerere Road Jijini Dar es Salaam, kulia ni Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki hiyo, Dasu
Musa, na kushoto ni Meneja wa Tawi la Nyerere Road, Aisha Awadh.
.................................
Mkurugenzi Mtendaji wa
Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud, leo Tarehe 19 Novemba 2018, amezindua
rasmi wiki ya huduma kwa wateja ya Benki hiyo na kutoa wito kwa wateja na
wananchi kwa ujumla kutembelea matawi yote ya jijini Dar es Salaam ili kupata
huduma mbalimbali za kibenki.
Dkt. Muhsin amesema sambamba
na wiki ya huduma kwa wateja, Benki hiyo pia inaadhimisha miaka saba ya kutoa
huduma za kibeki hapa nchini huku ikijivunia mafanikio yaliyopatikana.
Alisema Benki hiyo
ilipoanzishwa Novemba 24 mwaka 2011 ilikuwa na Tawi moja tu Kariakoo Mtaa wa
Tandamti na kwamba mpaka sasa Benki hiyo ina matawi manane katika mikoa minne
ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Tanga.
Aliongeza kuwa tayari
maandalizi yanafanyika ya kufungua tawi la tisa Zanzibar na kuongeza kuwa upo
mpango wa kufungua Tawi makao makuu ya nchi Dodoma ili kusogeza huduma za Amana
Bank katika makao makuu ya nchi.
Akizungumzia mafanikio
waliyopata Dkt. Muhsin alisema ni pamoja na kuongezeka kwa wateja ambao mpaka
sasa wamefikia elfu tisini huku fedha zilizowekwa na wateja mpaka sasa zikifikia
Bilioni 192, ambapo matarajio ni kufikisha Bilioni 200 ifikapo mwishoni mwa
mwaka huu wa 2018.
Aidha, alisema mpaka sasa mikopo
iliyotolewa na Amana Bank kwa wateja wake ni Bilioni 143 jambo ambalo limesaidia
katika kukuza uchumi miongoni mwa watanzania mmoja mmoja, vikundi, na Taasisi
huku serikali ikifaidika kwa kodi zinazotokana na wananchi waliowezeshwa
kiuchumi na Amana Bank.
Alifafanua kwa kusema
kuwa, mikopo hiyo imegawanyika katika makundi tofauti ambapo ipo mikopo
mikubwa, mikopo ya kati na mikopo midogo midogo.
Alisema huduma mpya ya
kujivunia kwa wateja wa Amana Bank katika kipindi hiki cha wiki ya huduma kwa
wateja mwaka 2018 ni mikopo ya vikundi ambapo wakopaji watapewa mikopo
isiyokuwa na riba bila ya dhamana kwani dhamana itakuwa ni kikundi chao tu
walichokiunda na kufaidika na mikopo hiyo kuanzia shilingi laki tatu hadi
milioni nne.
Akitaja miongoni mwa faida
zitakazopatikana katika wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu Mkurugenzi huyo
alisema kutakuwa na punguzo maalum ya bei ya viwanja vinavyotolewa kwa njia ya
mkopo na Amana Bank kwa kushirikiana na Propert International Ltd. (PIL) ambapo
watakuwepo wawakilishi wa PIL katika matawi yote ya Dar es Salaam.
Aliendelea kufafanua kuwa,
katika kuwajali wateja wake, Amana Bank leo imezindua rasmi kampeni maalum ya
NUFAIKA NA AKIBA YAKO, katika kampeni hiyo wateja watakaoweka akiba isiyopungua
milioni tano kwa kila mwezi kwa muda wa miezi mitatu mfululizo watapata nafasi
ya kushinda pikipiki aina ya TVS.
Akielezea mikopo ya
vikundi Meneja wa Amana Bank Tawi la Nyerere Road, Aisha Said Awadh alisema
mikopo ya vikundi inawahusu kina mama, kina baba vijana na wajasiliamali wadogo
wadogo ambao kwa muda mrefu ilikuwa kilio chao.
Katika uzinduzi huo wa
wiki ya huduma kwa wateja ambao umefanyika Tawi la Nyere road, Mkurugenzi wa
Amana Bank Dkt. Muhsin Masoud ameweza kuwahudumia wateja yeye mwenyewe katika
Tawi hilo ambalo limewafurahisha watjea kwa kuwa wameweza kuuliza maswali mbalimbali
na kupatiwa majibu moja kwa moja kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji aliyekuwa
katika meza ya kutolea huduma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Amana Bank katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika katika Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud(mwenye miwani) akitoa ufafanuzi kwa mteja aliyefika mezani kwake leo kupata huduma za Benki hiyo ambapo mara baada ya kuzindua wiki ya huduma kwa wateja Dkt. Muhsin alikaa mezani kuwahudumia wateja, kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa Amana Bank, Harith Fentu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud (mwenye miwani) akitoa maelekezo kwa wateja waliofika mezani kwake kupata huduma leo Novemba 19, 2018 mara baada ya kuzindua wiki ya huduma kwa wateja, kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa Amana Bank, Harith Fentu.
Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki hiyo, Dasu Musa, akizungumza jambo na Meneja wa Tawi la Nyerere Road, Aisha Awadh mara baada ya kuzindua wiki ya huduma kwa wateja uzinduzi uliofanyika katika Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud (mwenye miwani) akibadilishana mawazo na meneja wa Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam, kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa Amana Bank, Harith Fentu.
Kabla ya kuingia ndani
unapokelewa nje kwa msaada mbalimbali wa maelezo kuhusu huduma za Amana Bank, kushoto aliyesimama ni Meneja
wa Masoko wa Amana Bank, Jamali Issa akiwa tayari kupokea wateja kuwapa maelekezo kuhusu huduma za Benki hiyo katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment