Tuesday, November 26, 2019

Korea, Tanzania yajadili Geospatial information, Tanzania kunufaika na mpango huo


Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Hamdounny Masour akisoma hotuba katika ufunguzi wa wa mkutano wa siku mbili wa Geospatial Information Road Show uliowakutanisha wataalamu wa masuala ya ardhi kutoka nchini Korea na Tanzania.


Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Tae Ick Cho akitoa hotuba yake katika ufunguzi wa wa mkutano wa siku mbili wa Geospatial Information Road Show uliowakutanisha wataalamu wa masuala ya ardhi kutoka nchini Korea na Tanzania unaofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.







Imeelezwa kuwa matumizi ya teknolojia hasa ICT yana tija sana katika kuyafikia maendeleo.

Hayo yamebainishwa katika mkutano wa siku mbili wa Geospatial Information Road Show uliofanyika jijini Dar es salaam ambao uliwakutanisha wataalamu wa masuala ya ardhi kutoka nchini Korea na Tanzania.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Tae Ick Cho amesema Teknolojia bora katika kukuza uchumi ndiyo  silaha kubwa na pekee ya kimaendeleo na yenye kuleta ushindani katika soko la dunia na hilo litafanikiwa kam ataifa litajikita zaidi katika kuwekeza katika teknolojia.

 Amesema bila hiyo hatutaweza kushindana na mataifa mengine yenye teknolojia ya juu, tukumbuke msemo wa ukiona vyaelea ujue vimeundwa , hivyo hatuwezi kuendelea bila ya kuweka mbele teknolojia, kushirikiana na kuondoa vikwazo



Amesema kwa muda mrefu Tanzania na Korea Kusini zimekuwa na ushirikiano wa hali ya juu hasa katika masuala ya biashara zilizoruhusu kuvuka mipaka na hiyo yote ni kwa malengo ya kukuza uchumi baina ya nchi hizo mbili.

Pia amesema tangu kuanzishwa kwa Geospatial Information Road Show malengo makuu ni pamoja na kuendesha semina za kiteknolojia katika usajili ardhi, mikutano ya biashara baina ya Serikali ya Tanzania Makampuni wakilishi ya Korea yaliyopo nchini pamoja na kupeana taarifa mbalimbali katika masuala ya ardhi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa upimaji na ramani kutoka Wizara ya Ardhi Hamdounny Masour amesema faida ya mkutano huo ni kwamba Taifa litaidika na taarifa mbalimbali ambazo wataalamu hao wanazo.

Amesema kupashana habari na kubadilishana uzoefu baina ya kampuni kutoka Korea na Tanzania ni moja katika ya hatua kubwa ambayo itasaidia nchi hizo mbili kufikia malengo.

Masour amesema kuwa kupitia mkutano huo wataendelea kudumisha ushirikiano huo pamoja na kupeana taarifa za kisekta katika masuala ya upimaji wa ardhi.

“Ushirikiano baina ya nchi hizo mbili umekuwa wa kindugu na kupitia Geospatial Information Road Show na Wizara ya Ardhi tutaendelea kupeana taarifa za kisekta ili kuweza kuyafikia maendeleo” ameeleza.

Mkutano huo uliodumu yangu 2013 umewakutanisha wadau kutoka Wizara ya Ardhi nchini pamoja na Wizara ya Ardhi, miundombinu na usafiri kutoka Korea pamoja na wataalamu mbalimbali yakiwemo makampuni makubwa 12 kutoka nchini Korea.



Thursday, November 21, 2019

Serikali yasisitiza udhibiti magonjwa yasiyoambukiza





Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akifungua tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza Novemba 9, 2019 jijini Dodoma ambapo kilele chake ni Novemba 14, 2019.


Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma



Michezo ni nyenzo madhubuti katika kulinda afya za wanadamu kwa kuwajengea uimara na ustahimilivu, kukuza stadi za kijamii kiubunifu na kiuongozi ili kuwawezesha wanamichezo na watu wote kujifunza vitu vipya vinavyoweza kuchangia kutunza afya zao ili waweze kujiletea maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.

Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 inatambua umuhimu wa michezo ikiwemo kuhamasisha Umma wa Watanzania kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo. Kwa kutambua jambo hilo, Serikali imewezesha upatikanaji wa viwanja na vifaa vya michezo vilivyo bora na vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya michezo nchini.  

Kama taifa, kumekuwa na mtazamo chanya kwa viongozi kuthamini michezo kuanzia ngazi ya Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa kupitia mikoa, wilaya, tarafa, kata, vijiji, mitaa na vitongoji.

Kwa kulitambua na kulithamini suala la michezo kwa watu wa rika zote kuwa ni muhimu kwa afya, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mwaka 2016 alipokuwa akizindua kampeni ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam aliagiza watu katika maeneo yao nchini kushiriki kufanya mazoezi ambayo ni sehemu ya michezo.

Ili utaratibu wa kufanya mazoezi uwe endelevu, Makamu wa Rais alisisitiza “……….kila Jumamosi ya pili ya mwezi itakuwa siku ya mazoezi kwa afya, kwa sababu mazoezi ni afya na nawaasa wananchi kufanya mazoezi na kuanzisha na kujiunga na vikundi vya mazoezi na Serikali itatimiza wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi kote nchini.”

Wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa katika kulifanyia kazi agizo hilo kwa kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ambao umeongeza idadi ya vikundi vya mazoezi ya pamoja katika maeneo mbalimbali ya nchini. 

Hamasa ya kufanya mazoezi sasa imekuwa nzuri ambapo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zimeanzisha utaratibu wa kuwa na bonanza, matamasha ya michezo pamoja na vilabu vya kufanya mazoezi. Hatua hii imekuwa ni chachu mpya ya kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mama Samia la kufanya mazoezi kwa manufaa ya afya za Watanzania.

Akiwasilisha Bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/2020 ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe aliliambia bunge na Watanzania wote kuwa, miongoni mwa majukumu ya sekta ya michezo ni kuratibu na kusimamia maendeleo ya michezo nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika michezo.

Mojawapo ya vitu vinavyoshirikisha watu wengi kujiunga na kufanya mazoezi ni kuwa na matamasha ya michezo mbalimbali ambayo yanalenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika michezo ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi  hapa nchini.

Magonjwa hayo hutokana na mitindo isiyofaa ya maisha kama matumizi ya tumbaku, lishe duni, matumizi ya pombe kupita kiasi, pamoja na kutoshughulisha mwili au kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara. Magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na mishipa, saratani, pumu na magonjwa ya akilini miongoni mwa magonjwa hayo, ambapo yasipodhibitiwa huwa na sugu na yenye kuhitaji gharama kubwa kuyatibu.

Hapo awali, magonjwa hayo yalikuwa yakiwaathiri watu wenye umri mkubwa zaidi ya miaka 45, lakini kwa sasa yanazidi kuathiri watu watu wengi wakiwemo watoto wenye umri mdogo.

Naibu Wiziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza hivi karibuni akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza lililofanyika Novemba 09, 2019 katika uwanja wa Jamhuri Dodoma alihimiza watu kuchukua uamuzi wa kufanya mazoezi ili kujenga afya zao.

“Mazoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kasi ya kupumua. Wataalam wa afya wanasema kuwa kiwango cha mazoezi kinacholeta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tatu kwa wiki na yanayomfanya mtu kutokwa na jasho” alisisitiza Naibu Waziri Shonza.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Shonza watumishi wanaofanya kazi ofisini wametakiwa kuongeza bidii ya kufanya mazoezi kulingana na mtindo wa maisha ya mtumishi mmoja mmoja kuendana na hali yake ya maisha.

Kwa watumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na watu wengine wanaotumia magari, wanapaswa kupanga shughuli ambazo zitawafanya kila siku watembee kwa miguu, wanaoishi au kufanya kazi ghorofani wajitahidi na wajizoeshe kutumia ngazi kila siku badala ya lifti, mtu anapokwenda mahali popote watumie njia ndefu kutembea badala ya njia ya mkato pamoja na kupunguza muda wa kutazama televisheni, badala yake muda huo utumike kufanya shughuli zinazotumia viungo vya mwili kama kufua, kuosha vyombo, kuosha gari, kusafisha nyumba, kazi za bustani na kufyeka majani ambazo zinasaidia kujenga utimamu wa mwili.

 Naibu Waziri Shonza ametoa rai kwa  waajiri kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha watumishi wao wanashiriki katika michezo na kufanya mazoezi hata maeneo yao ya  kazi na kutoa mfano wa kuanzisha timu mbalimbali za michezo na kutenga siku maalum katika mwezi kwa ajili ya mabonanza ya michezo. Mazingira rafiki ya kufanyia mazoezi kazini ni pamoja kutenga vyumba vya mazoezi na na kununua vifaa vya michezo. Hatua hiyo itaimarisha afya za watumishi na kupunguza gharama za matibabu katika taasisi husika.

Aliongeza kuwa ili kufanya mazoezi kuwa endelevu, maafisa michezo na utamaduni wa mikoa na wilaya wana wajibu wa kuongeza uhamasishaji na uundaji wa vikundi vya mazoezi ya pamoja katika maeneo yao.

Wizara nyingine zenye uhusisano na mchango katika kufananikisha wananchi kufanya mazoezi ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara hizo zina mamlaka ya kusimamia na kuweka mazingira bora ya watu kufanya mazoezi kwa kuendelea kutenga viwanja vya michezo na kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi hususani viwanja vya michezo na kuboresha barabara za waenda kwa miguu na baiskeli ili kuhamasisha watu kutembea na kuongeza usalama wa mazoezi.

Aidha, mamlaka  za  usafiri, zinawajibu wa kuboresha usafiri wa jumuiya ili kuongeza idadi ya watu wanaotumia usafiri wa jumuiya kwa sababu tafiti nyingi zinaonesha kuwa utumiaji wa usafiri wa jumuiya unaongeza uwezekano wa kutembea na kufanya mazoezi na hivyo kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

Matamasha ya michezo pamoja na matamasha mengine yakiwemo ya utamaduni yanatakiwa kuwa kichocheo cha kushirikisha vitu vingi ikiwemo michezo ya jadi na mashindano ya baiskeli katika maeneo mbalimbali ambayo yana mchango mkubwa katika kutunza afya za washiriki wa michezo hiyo.

Wakati wa matamasha hayo, ni vema wananchi wahamasishwe kupima afya zao hususani wa magonjwa yasiyoambukiza kwani tiba ya mapema ina manufaa kwa kuwa inapunguza uwezekano wa watu kupatwa na madhara zaidi. Hatua hiyo inaweza kuondoa magonjwa hayo moja kwa moja. Ili kuongeza hamasa ya wananchi na wanamichezo kupima afya zao, upimaji huo unapaswa kuwa ni wa bure ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kupimwa.

Hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo mataifa yameazimia kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu, (SDGs) ili kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030.

Akizungumzia mwongozo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Adhanon Ghebreyesus alisema, “Zaidi ya nusu ya watu duniani wanaishi mijini, na idadi yao inaongezeka. Viongozi wa miji wanapaswa kuchukua maamuzi ambayo yataboresha afya za wakazi wao, ili miji iweze kuchipua na kustawi. Kila mtu anapaswa kupata huduma ambazo zitaboresha afya, huduma za usafiri wa umma ziwe salama, makazi ya nje yawe safi na salama, mlo uwezo mzuri na huduma za afya ziwe bora.”

Naye Balozi wa WHO katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) na majeraha, Michael Bloomberg alisema kuwa shirika hilo lipo mstari wa mbele katika kusambaza mikakati hiyo duniani kote ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.

“Tunafanya kazi kuhamasisha uelewa miongoni mwa viongozi wa miji na watunga sera kuhusu manufaa halisi yanayoweza kupatikana pindi programu hii ya kuboresha miji inapofanya kazi.” alisisitiza Balozi Bloomberg.

Ni kweli, wataalamu wa afya wanashauri kuwa ni vema kila mtu awajibike kuitunza afya yake kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwani afya njema ni msingi wa maendeleo. Hatua hii inaunga mkono kauli mbiu tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza inayosema “Tutembee pamoja katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.”



CHUO CHA KFDC KIBAHA CHAJIVUNIA MAFANIKIO



Mkuu wa chuo cha maendeleo ya wananchi Kibaha (KFDC) Joseph Nchimbi akizungumza na wazazi, wanafunzi na viongozi mbali mbali wa serikali ambao walihudhulia katika mahafali ya kuwaga wanafunzi wa chuo hicho yaliyofanyika mjini Kibaha.(PICHA NA VICTOR MASANGU)

NA SCOLASTICA MSEWA, KIBAHA


CHUO CHA Maendeleo ya Maendeleo ya wananchi Kibaha chajivunia mafanikio  kwa kupanua wigo wa udahili wa wana chuo kutoka Mikoa yote Tanzania.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha Joseph Nchimbi wakati wa mahafali  ya chuo hicho ambapo jumla ya wanachuo 142 wamehitimu kati yake wanawake 42 na wanaume 100.

" Chuo chetu cha KFDC kimepiga hatua kubwa katika kutoa mafunzo bora na kufanya vijana wengi kuomba nafasi katika chuo hiki ,kwa kipindi cha miaka mitatu kimeweza kudahili wanafunzi wengi na kufanya vizuri"  alisema Joseph 

Joseph alisema mafanikio mengine ambayo wanajivunia wanachuo wote ambao wametoka katika chuo hicho wamepata ajira serikalini ,sekta binafsi na wengine wamejiari wenyewe sekta binafsi kutokana na ujuzi waliosomea chuoni ikiwemo ufundi umeme ,ufundi magari ufundi uchomeleaji na uundaji vyuma.

Aidha alisema idadi ya wakufunzi kila siku wanaongezeka waliohamia katika chuo hicho hivyo kupunguza uhaba wa wakufunzi waliokuwepo hapo awali wanaendelea kupata huduma bora kutoka kwa Wakufunzi wa Shirika la Elimu Kibaha.

Joseph alisema Chuo cha Maendeleo Kibaha (Kibaha Folk  Development College )kilianzishwa mwaka 1964  kikijulikana kama Farmers Training Centre  chini ya mradi wa pamoja wa serikali ya Tanganyika na nchi ya za Nordic uitwao  Tanganyika Nordic Project.

Alisema katika chuo  hicho kuna fani mbalimbali kwa ajili ya kujifunza  ikiwemo ufundi selemala,ufundi ushonaji,ufundi uashi,ufundi bomba,kilimo,mifugo na hotelia.

Joseph alisema chuo   hicho kinachangia nguvu  kazi muhimu inayohitajika katika uchumi wa viwanda uwezo wa chuo kuchukua wanachuo 500 lakini kwa sasa chuo kina wanafunzi 295 .

Kwa upande wake Mwanafunzi wa Chuo hicho cha Maendeleo ya Wananchi, Emanueli Leonard alisoma risala ya wanachuo wanaohitimu mwaka wa pili alielezea changamoto za chuo hicho ikiwemo uchakavu wa majengo,upungufu wa kompyuta,ukosefu wa jengo la kompyuta,uchakavu wa karakana za kujifunzia na ukosefu wa jengo la kujifunzia

Naye mgeni rasmi  Mjumbe wa Bodi wa shule hiyo   Elisante Ngure alipongeza Serikali kwa kuvitunza vyuo vya ufundi vilivyopo hapa nchini .

Ngure aliwataka wana chuo waliohitimu chuoni hapo watumie elimu waliopata kwa kujiongezea ajira na kuzingatia nidhamu kwani nidham ndio siri ya mafanikio  pia wajenge   umoja na  mshikamano .

Aliwataka vijana kuchangamkia fursa katika kukopa mikopo ya Serikali ambayo inatolewa ngazi ya halmashauri ya Wanawake Vijana na Watu Wenye ulemavu.

Rais Dkt. Magufuli Amestahili PhD ya Heshima








Na Mwandishi Wetu-Dodoma

Utendaji mzuri katika eneo lolote ni tunu na uwezo wa kuleta mageuzi ya kweli kwenye jamii yoyote ile inayolenga kupiga hatua  kufikia maendeleo endelevu yanayotokana na Dira ya Maendeleo iliyowekwa na jamii husika.

Kufikiwa kwa malengo hayo katika nchi yetu kunatokana na uongozi madhubuti  na utendaji  mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwekeza vyema katika Sekta ya Elimu, Nishati, Maji,Uchukuzi, Mawasiliano na Afya.

Msingi wa Mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka minne yanatokana na aina ya uongozi wa Rais Magufuli wa kuzingatia kuwapo kwa ushahidi wa mahusiano chanya kati ya  “Kiongozi na Matokeo”  sambamba na ukuaji wa uchumi.

Hivyo Basi, uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya elimu umeonesha mafanikio makubwa kupitia Mpango wa Elimu Msingi (Basic Education) bila malipo wenye lengo la kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Tanzania mwenye sifa ya kwenda shule anapata haki ya kupata elimu bila kikwazo cha ada na michango mingine.

Katika kukuza sekta hii Chuo Kikuu cha Sokoine kilipatiwa matrekta 10 mapya ili kufundishia wataalamu wa kilimo,katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulifanyika ujenzi wa mabweni,halikadhalika mikopo kwa wanafunzi wa wa Elimu ya Juu imeongezwa hadi shilingi bilioni 450 kwa mwaka 2019/ 2020 ikilinganishwa na shilingi bilioni 427.5 zilizotengwa mwaka 2018/2019.

Hatua nyingine ni pamoja na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi unaoendelea katika wilaya nyingi hapa nchini, ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo,maabara na miundombinu mingine ya sekta hii imechangia kukuza kiwango cha elimu.

Katika sekta ya nishati Rais Magufuli amewezesha kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa  maji katika mto Rufiji unaojulikana kama mradi wa kufua umeme wa  Mwalimu Nyerere utakaozalisha megawati 2115, hapa Mhe. Rais amewahi kunukuliwa akisema “Umeme ni Maendeleo, ni kichochea muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa taifa lolote,bila ya kuwepo kwa umeme wa uhakika ndoto yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haitatimia.”

Sekta ya uchukuzi nayo haikuachwa nyuma kupitia utekelezaji wa miradi ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 70 na kipande cha Morogoro Makutopora unaendelea kwa kasi na umefikia asilimia 20 , mradi huu umetoa ajira kwa watanzania wapatao 6,335 sawa na asilimia 90 ya wafanyakazi wote.

Kukamilika kwa mradi huu kutachangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi kuongezeka na hivyo ustawi wa wananchi utaleta tija katika uzalishaji.

Uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam mwaka 2018/2019 unaendelea na unalenga kuifanya kuwa ya kisasa na kuwa na gati zenye uwezo wa kuhudumia meli nyingi  na kubwa zaidi ya ilivyokuwa awali, kwa sasa gati namba 1 hadi 7 zimeboreshwa na ujenzi wa gati jipya la kuhudumia meli zilizobeba magari umefikia asilimia 65.

Bandari ya Tanga na Mtwara nazo zimeboreshwa na kuongeza uwezo wa kuhudumia meli kubwa na kwa idadi kubwa zaidi, usafiri katika maziwa yote nchini umeimarishwa kwa kujengwa kwa meli mpya na kukarabatiwa kwa zile zilizopo hivyo wananchi wanaotegemea usafiri huo katika ziwa Tanganyika, Victoria na Nyasa wameongeza kasi ya shughuli za kiuchumi.

Baadhi ya Miradi inayoendelea  katika sekta ya  uchukuzi ni pamoja na ile ya ujenzi wa  barabara za juu kwenye makutano ya Ubungo, upanuzi wa barabara ya Kimara Mwisho hadi Kibaha Km 19.2 kutoka njia mbili hadi njia nane, ujenzi wa daraja jipya  la Salenda na miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Awamu ya II na III.

Kufikia mwezi Februari 2019, jumla ya miradi 65 ya maji vijijini ilikamilishwa ambapo wananchi milioni 25.36 waishio katika vijiji hivyo wamenufaika kwa kupata maji safi na salama,hali hiyo inaendana na malengo  ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Katika kusimamia rasilimali za nchi Rais Magufuli amewezesha kutungwa kwa sheria kwa ajili ya usimamizi thabiti wa rasilimali ya madini, Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili Na.5 ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi No.6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini sura ya 123.

Kwa upande wa Sekta ya Kilimo inayoajiri wananchi takribani asilimia 75 hadi 80 ambapo kwa kutambua umuhimu wa sekta hii Rais Magufuli alizindua Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Programu hii inalenga kuleta mageuzi katika sekta hii kwa maana ya mazao, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya  kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima hususan wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.

Kwa kuwa Rais Dkt. Magufuli amewezesha ujenzi wa vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya 67 na hospitali za kanda zinaendelea kujenga ni wazi kuwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi unamfanya kuwa  na sifa za kutunukiwa shahada hii. Hakika usemi wa wahenga usemao chanda chema huvikwa pete leo umetimia kwa Mhe. Rais Magufuli kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Udaktari wa Falsafa.



Mwisho.












Tuesday, November 19, 2019

Soma tamko la pamoja la kutoka mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni (TECMN), waipongeza mahakama ya rufaa


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAMKO LA PAMOJA KUTOKA MTANDAO WAKUTOKOMEZA NDOA ZA UTOTONI TANZANIA KUIPONGEZA MAHAKAMA YA RUFAA YA TANZANIA



Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN), unaojumuisha mashirika na Asasi zisizo za kiserikali zaidi ya 50 ukiratibiwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto kwa Sauti Moja tunapongeza Mahakama ya Rufaa ya Tanzania   kwa uamuzi wake wa kubatilisha kifungu namba 13 na 17 vilivyopo kwenye sheria ya ndoa  No. 5 ya mwaka 1971 (Sura 29).

Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012 umekuwa ukifanya jitihada na mikakati mbalimbali ya uhamasishaji na uelimishaji juu ya athari ya ndoa za utotoni na kwa vipindi tofauti wanachama wa mtandao wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali kuonesha ukubwa wa tatizo la ndoa za utotoni na visababishi vyake ambavyo ni pamoja na umasikini, mila na desturi pamoja na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 and 17 ambayo inaruhusu mtoto wa kike kuolewa kuanzia umri wa miaka 14.

Kwa nyakati tofauti Mtandao umeweza kuhamasisha jamii, wanahabari, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na viongozi wa serikali katika ngazi tofauti ili wachukue hatua au washirikiane na Mtandao katika jitihada za kutokomeza ndoa za utotoni pamoja na kuunga mkono jitihada za mtandao za mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Katika kuhakikisha tatizo la ndoa za utotoni na mabadiliko ya sheria ya ndoa yanatekelezwa ili kulinda haki na ustawi wa mtoto wa kike; Mtandao uliweza kufanya mazungumzo na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ya  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Umoja wa Wabunge Wanawake Bungeni. Vilevile katika vipindi tofauti, Mtandao uliweza kufanya mazungumzo na  Spika wa Bunge, Naibu Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali zikiwa ni harakati za kutafuta kuungwa mkono jitihada za Mtandao unaolenga kuleta mabadiliko chanya yatakayomnusuru mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni.



HALI YA NDOA ZA UTOTONI TANZANIA IKOJE KWA SASA?

1.      Tanzania ni moja ya nchi zenye kiwango cha juu cha ndoa za utotoni duniani. Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF za kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda. Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni asilimia 31. Nchini Kenya, ni watoto asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza miaka 18.

2.      Kwa wastani, kati ya watoto watano (5) wakike wawili (2) huolewa kabla ya umri wa miaka 18. Utafiti wa afya na watu (TDHS 2015) unaonesha kuwa asilimia 31% ya wanawake kati ya umri wa miaka 20 – 24 waliolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.

3.      Takwimu za ndoa za utotoni kimkoa; Shinyanga (59%), Tabora (58%), Mara (55%), Dodoma (51%), Lindi (48%), Mbeya (45% -), Morogoro (42%), Singida (42%), Rukwa (40%), Ruvuma (39%), Mwanza (37%), Kagera (36%), Mtwara (35%), Manyara (34%), Pwani (33%), Tanga (29%), Arusha (27%), Kilimanjaro (27%), Kigoma (26%), Dar es Salaam (19%) na Iringa (8%).

4.      Ndoa za utotoni kwa hapa Tanzania huathiri zaidi watoto wa kike kwani kwa wastani wanawake wengi huolewa mapema zaidi kwa tofauti ya umri wa miaka 5 wakilinganishwa na wanaume.



UAMUZI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KUHUSU MABADILIKO YA SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971 KIFUNGU NAMBA 13 NA 17

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu,  hukumu ya mahakama iliyokatwa na serikali Julai 8, 2016 kupinga kesi ya kikatiba iliyofunguliwa  na Rebeca Gyumi (Mwanachama wa Mtandao-Msichana Initiative) ya kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu namba 13 na 17, hatimaye, tarehe 23 ya mwezi Julai mwaka 2019 Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubaliana  na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania kubadilisha vifungu hivyo kwa kua ni vya kibaguzi na vinakiuka haki ya kikatiba ya kujieleza kwakua mtoto mwenye  umri wa miaka 14 hawezi kuingia katika mkataba wa ndoa kwa kuwa hana  ufahamu kiasi cha kuweza kujihusisha na mkataba wa ndoa na kuiamuru serikali kuibadilisha sheria hiyo ndani ya mwaka mmoja kumruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri kuanzia miaka 18. .

Hukumu hii ni ushindi kwa watoto wa kike wa Tanzania kwani imewapa ulinzi wa kisheria, pia hii ni hatua muhimu sana kwetu sisi kama mashirika na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii tunayopigania haki za watoto wa kike kwa kuona hatua ya kwanza inayopelekea watoto wa kike kupata haki zao za msingi kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Watoto wa kike wa Tanzania wapo huru kisheria  kilichobaki ni kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja katika kuhakikisha tunatoa elimu kwa wadau, viongozi, Jamii na watoto kwa ujumla kwa lengo la kuwaelimisha wahusika wote juu ya sheria hii na athari zinazotokana na ndoa za utotoni ili kuwasaidia na kuwalinda watoto wa kike wafikie malengo na ndoto zao za kielimu.

Katiba ya Tanzania inasema  binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake (Ibara ya 12 (1)). Inaeleza zaidi kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya yeyote miongoni mwao kubaguliwa, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Sheria zinazoweka umri wa chini tofauti wa kuoa au kuolewa baina ya mvulana na msichana ni za kibaguzi na zinakiuka haki ya usawa mbele ya sheria.



ATHARI ZA NDOA ZA UTOTONI

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu ndoa za utotoni. Inakadiriwa kwamba asilimia 37 ya wasichana Tanzania wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Umasikini, mila za kijamii na kiutamaduni, unyanyasaji wa kijinsia,  , vyote hivyo vinachangia ndoa za utotoni.



ATHARI YA NDOA ZA UTOTONI

·         Kupoteza fursa za elimu na ujuzi wa kazi

·         Kupata maambukizo ya virusi vya ukimwi (VVU) au magonjwa ya zinaa (STD)

·         Kunyanyasika kisaikolojia, kimwili, kijinsia

·         Kuyumba kiuchumi na kudumu katika umasikini,

·         Kukosa au kushindwa kujitawala

·         Unyanyasaji wa kimwili  unyanyasaji wa maneno

·         Vifo vya watoto wachanga na watoto wa kike pindi wanapojifungua kwa kuwa viungo vyao vya uzazi bado havijakomaa

·         Vifo vya wajawazito

·         Kuharibika kwa mimba





SHAURI LA REBECA GYUMI

Baada ya kuona changamoto zote wanazokutana nazo watoto wa kikekatika suala zima la kuolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18, Rebeca Gyumi alifungua shauri kwa niaba ya watoto wa kike  walio katika hatari ya kuingia kwenye ndoa za utotoni. Shauri la Rebeca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Katika Shauri la Madai Na.5 ya 2016 (Shauri la Rebeca Gyumi) lilipinga uhalali wa kikatiba wa ndoa za utotoni. Matokeo yake ni kwamba mahakama kuu Tanzania ilitamka kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa ni vya kibaguzi na vinakwenda kinyume na katiba.

KUPINGA SHERIA INAYOHUSIANA NA NDOA ZA UTOTONI

Sheria ya Ndoa imeweka vigezo vinavyohitajika kwa watu wanaoingia katika ndoa. Kwa mujibu wa sheria, umri wa chini kwa wasichana kuolewa ni miaka 15 na kwa wavulana ni miaka 18. Kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha sheria, wavulana na wasichana wanaweza kuoa au kuolewa mapema zaidi, yaani wakiwa na umri wa miaka 14, kwa idhini ya mahakama na miaka 15 kwa idhini ya wazazi.

Kifungu cha 17 cha Sheria kinaelezea kwamba kwa ndoa ya msichana mwenye umri wa chini ya miaka 18, baba yake ni lazima atoe idhini kuruhusu ndoa hiyo, kama baba yake amefariki, basi mama yake. Kama wazazi wote wamefariki, walezi wake ni lazima watoe idhini. Kama hakuna mlezi , hakuna idhini inayohitajika.

Kwanini Rebeca Gyumi alipinga vifungu vya 13 na 17 vya Sheria hii kwa misingi kwamba:

1.      Vinakiuka Ibara Ya 12(1) ya katiba ya Tanzania, katiba ambayo inatoa usawa kwa watu wote mbele ya sheria;

2.      Vinakiuka Ibara ya 13(1) (2) ya katiba ya Muungano wa Tanzania ambayo inawalinda watu dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya kijinsia;

3.      Watu walio chini ya umri wa miaka 18 ni watoto na hawana uwezo wa kufanya mamuzi sahihi juu ya kuoa au kuolewa;

4.      Vinakiuka Ibara ya 21(2) ya Katiba ya Tanzania kwa kutowapa wasichana fursa ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa kuamua mustakabali wa maisha yao

5.      Vinamnyima mtoto haki ya kupata elimu na uhuru wa mawazo.

Tarehe 8 julai, 2016, Mheshimiwa Jaji Lila J., Mheshimiwa Jaji Kihio J. na Mheshimiwa Jaji Munisi J. walieleza kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa vimepitwa na wakati na vinakwenda kinyume na katiba.



MASUALA MUHIMU KWENYE UAMUZI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA

1.      Ndoa za Utotoni  Zinakwenda Kinyume na Maslahi Muhimu ya Mtoto.

Kwa sababu hiyo, mahakama ilieleza kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa vinaruhusu watoto kuingia katika ndoa. Mahakama Kuu ya Tanzania ilieleza kwamba haifai kuwaingiza watoto katika majukumu makubwa ya ndoa. Pia ilidokeza kuhusu hatari kubwa ya kiafya inayowakabili wasichana pale wanapoolewa wakiwa na umri mdogo.

2.      Haki ya Usawa Mbele ya Sheria na Kutobaguliwa kwa Namna Yoyote.

Mahakama ilisema kwamba vifungu hivyo  havitoi usawa kwa wasichana na wavulana katika njia mbili. Kwanza umri wa ndoa ni tofauti kati ya mvulana na msichana. Pili, wasichana chini ya miaka 18 wanahitaji ridhaa ya wazazi kuolewa wakati wavulana hawahitaji. Tofauti hii inaleta maana kwamba, wasichana na wavulana hawatendewi sawa chini ya vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa. Kwa hiyo, iliamuliwa kwamba vifungu hivyo vinawabagua wasichana na vinakiuka Ibara za 12 na 13 za katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

3.      Sheria ya Kimila na Kiislamu Hazitumiki Kwenye Masuala Yaliyoainishwa Kwenye Sheria Ndoa.

4.      Serikali ilijaribu kutetea sheria zinazoruhusu ndoa za utotoni kwa msingi kwamba ilifanikiwa ili kuziweka kwa pamoja Sheria tofauti za Kimila, Kiutamaduni na Kidini katika ndoa. Mahakama ilikataa hilo kwa maelezo kwamba kifungu cha 11(4) cha Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria Kinasema. “Kanuni za  sheria za kimila na kanuni za Sheria za Kiislamu hazitatumika katika suala lolote lililoanishwa katika Sheria ya Ndoa”.



5.      Haki ya Kushiriki Katika Maamuzi Yanayogusa Maisha Yako

Mahakama kuu ilibainisha kwamba itifaki ya Maputo inazihamasisha nchi wanachama kutunga sheria ambazo zitahakikisha kwamba hakuna ndoa inayofungwa bila kuwapo uamuzi wa uhuru na ridhaa kamili ya pande zote na kwamba umri wa chini wa mwanamke kuolewa lazima uwe miaka 18.

Kwakua Tanzania imeridhia chombo hicho cha kikanda, umefika wakati sasa wa kuchukua hatua stahiki za kisheria kuhakikisha kwamba haki iliyotolewa chini ya ibara 21(2) ya kikatiba inapatikana kwa wote

6.      Vifungu vya Sheria Havistahili Kutumika Tena

Katika uamuzi wake, Mahakama kuu ilitamka kwamba, vifungu katika Sheria ya Ndoa ambavyo vinaruhusu ndoa za utotoni havistahili kutumika.

Mahakama ilibaini kwamba kumekuwa na maendeleo kadhaa ya kisheria katika sheria ya Ndoa. Maendeleo haya yamefanywa ili pengine kuhakikisha kwamba, “Ustawi na ulinzi wa mtoto wa kike unaimarishwa, na utu na heshima ya mwanamke kwa ujumla vinalindwa”

Kwa mfano, Sheria Maalumu ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 imebainishwa adhabu kwa watu wanaojihusisha kimapenzi na watoto. kwa hiyo, kuruhusu ndoa za utotoni ni kama kutoa kibali cha kufanyika kwa uhalifu.

Mahakama iliona kwamba katika sheria kama za SOSPA na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Serikali kupitia sheria kama hizo ni kama imekiri kimyakimya kwamba haki ya watoto kulindwa inazidiwa nguvu na haja ya kuendeleza ndoa za utotoni.

Mahakama katika shauri la Rebeca Gyumi iliamuru Serikali kufanya marekebisho ya sheria ndani ya mwaka mmoja na kusahihisha vifungu vya kibaguzi vya 13 na 17 na kuweka miaka 18 kama umri wa chini unaostahili kwa ndoa kwa wavulana na wasichana. Shauri la Rebeca Gyumi ni ushindi wa kipekee kwa mtoto wa kike wa Tanzania. Linaonesha kwamba wanawake wanapaswa kuwa na haki ya kuridhia kuolewa na kwamba, umri wa chini wa kuoa/kuolewa lazima uwe miaka 18 kwa mwanamme na mwanamke. Pia linasisitiza kwamba mila na desturi hazipaswi kutumika kuwabagua wanawake au kuwanyima haki zao.

Tunaipongeza serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza jitihada za kuwalinda watoto kwa sheria na sera zinazowalinda watoto wa kike ikiwa ni pamoja na marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ambayo imeweka vifungu vinavyo zuia watoto wa kike kupewa ujauzito wakiwa shuleni na kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa yoyote atakeyepatikana na hatia.  .

Mwisho tunaiomba serikali kutekeleza maamuzi ya hukumu na kubadili vipengele husika.

Ni jukumu letu sote kuchukua hatua kuwalinda watoto na kukemea vikali vitendo vya ndoa za utotoni.



                     KWA SAUTI MOJA TUNASEMA   NDOA ZA UTOTONI SASA BASI !



Tamko hili limetolewa leo tarehe 19/11/2019 na Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni na kusomwa na Mratibu wa Mtandao.





Kwa Mawasiliano Zaidi:

Michael J. Sungusia

Mratibu wa Mtandao TECMN

Simu +255222775 010 au +255743 902858

Barua Pepe, michael@cdf.or.tz