Wednesday, November 7, 2018

JESHI LA POLISI MBEYA LINAWASHIKILIA WATU WAWILI KWA TUHUMA ZA KUVUNJA DUKA USIKU NA KUIBA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kupatikana na mali ya wizi. Watuhumiwa wamefahamika kwa majina ya 1. JOSEPH DESU PARAFESTO [24] Mkazi wa Sumbawanga – Majengo 2. ENWELO SINKONDE [32] Dereva Bodaboda na Mkazi wa Chunya wakiwa na fedha taslimu Millioni kumi na saba laki tisa na kumi na sita elfu [17,916,000/=].

Watuhumiwa walikamatwa mnamo 04.11.2018 majira ya saa 22.00 usiku huko maeneo ya Kijiji cha Mwansekwa kilichopo Kata ya Mwansekwa, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya na askari waliokuwepo kwenye kizuizi cha Polisi (Barrier) kilichopo kijiji cha Mwansekwa.

Watuhumiwa hao walikuwa wanasafiri kutoka Chunya kuja Mbeya mjini wakiwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 322 CAP aina ya T.BETTER iliyokuwa ikiendeshwa na ENWELO SINKONDE [32] huku JOSEPH DESU PARAFESTO akiwa amebeba begi dogo.

Baada ya kusimamishwa na askari walipekuwa begi alilokuwa amelibeba JOSEPH DESU PARAFESTO hatimaye kukuta kiwango hicho cha pesa. Mtuhumiwa alihojiwa kuhusu pesa hizo anazipeleka wapi na amezitoa wapi alidai kuwa amekabidhiwa na kaka yake wa Makongorosi – Chunya ambaye alidai ni mfanyabiashara wa madini aina ya dhahabu na kwamba amekabidhiwa fedha hizo azipeleke Sumbawanga kwa ajili ya kununulia bidhaa za duka la jumla.

Hata hivyo kutokana na kiwango hicho cha fedha kuwa kikubwa, ufuatiliaji wa kiupelelezi ulifanyika hatimaye kugundulika kuwa watuhumiwa walihusika kwenye tukio la KUVUNJA DUKA USIKU NA KUIBA huko Wilaya ya Chunya na kupora pesa hizo, hivyo walikuwa kwenye harakati za kutoroka na pesa hizo. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.

TUKIO LA MAUAJI – MBEYA MJINI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la THERESIA VENAS [26] Mkazi wa Mama John Jijini Mbeya kwa tuhuma kumuua kikatili VIKO BIKO, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60 – 65, Mkazi wa Iyela One.

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 05.11.2018 majira ya saa 13:00 mchana huko maeneo ya Iyela One, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, ambapo wa VIKO BIKO, alikutwa akiwa ameuawa chumbani na mwili wake ukiwa chini ya kitanda.

Katika uchunguzi uliofanyika, mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha sehemu za kichwani, mgongoni, mbavuni na tumboni karibu na kitovu, majeraha yanayoonyesha kuwa muuaji alitumia kitu chenye ncha kali.
Awali inadaiwa kuwa marehemu alikuwa akifanya biashara ya Grocery huko maeneo ya Iyela na kwa mara ya mwisho kabla hajafunga Grocery hiyo alikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa mavazi yaliyoficha uso wake na alikuwa hafahamiki maeneo hayo.

kufuatia tukio hilo, msako mkali ikiwemo ufuatiliaji kwa njia ya Cyber Crime ulifanyika na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa THERESIA VENAS [26] Mkazi wa Mama John Jijini Mbeya. Mtuhumiwa baada ya kuhojiwa amekiri kufanya tukio hilo akieleza kuwa chanzo cha kufanya mauaji hayo ya kikatili ni ugomvi uliotokea baina yake na marehemu wakati wakiwa chumbani kwa marehemu wakifanya mapenzi na marehemu kumlazimisha kufanya mapenzi kinyume cha maumbile. 

Mtuhumiwa ameumia bega la kulia katika ugomvi huo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu.Upelelezi wa shauri hili unaendelea.

OPERESHENI NA MISAKO MBALIMBALI.

Aidha katika misako inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoani hapa linawashikilia jumla ya watuhumiwa 63 kutokana na kujihusisha na uhalifu hasa wizi wa mali mbalimbali.

Katika misako hiyo, mali mbalimbali zimekamatwa ikiwa ni pamoja na:-
1.   Flat Screen inchi 45 tatu aina ya LG na Hisense mbili.
2.   Flat Screen inchi 32 tatu aina ya LG na Samsung mbili
3.   Flat Screen inchi 21 aina ya LG
4.   Home Theatre aina ya Sony
5.   Betri 08 za magari aina mbalimbali.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na Operesheni, Doria na Misako katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya hasa katika maeneo tete kama vile maeneo ya Mlima Nyoka, Mlima Igawilo, Mlima Mwansekwa, Mlima Iwambi ili kuhakikisha usalama kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara unakuwepo. Pia Jeshi la Polisi linaendelea na zoezi la ukaguzi katika nyumba za kulala wageni ili kuhakikisha usalama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.

No comments:

Post a Comment