Thursday, November 22, 2018

MKOA WA PWANI UMEKUSANYA KILO MIL. 17.3 SAWA NA TANI 17,313,010 ZA KOROSHO -NDIKILO

mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo
..............................................

NA MWAMVUA MWINYI,PWANI

MKOA wa Pwani umekusanya kilogramu milioni 17.3 sawa na tani 17,313,010 za zao la kibiashara la korosho katika maghala mbalimbali yaliyopo kwenye wilaya za mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha baada ya kutembelea iliyokuwa kiwanda cha kubangulia korosho cha Tanita Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema korosho hizo zimekusanywa hadi Novemba 21.

Alieleza,korosho hizo zimekusanywa kwenye vyama vya msingi na vikuu vya ushirika (Amcos )kwenye halmashauri za wilaya .

Ndikilo alisema halmashauri ya Mkuranga inaongoza kwa kukusanya kilo milioni 6.2 ikifuatiwa na Halmashauri ya Kibiti milioni 6.6.

Alitaja halmashauri nyingine ni Rufiji milioni 2.9,Kisarawe 390,000,Kibaha Mjini 354,318,Kibaha 316,205,Chalinze 86,719 Bagamoyo 90,724 na Mafia 108,000.

Alielezea,kwa utaratibu wa sasa wa serikali wa kununua korosho zote utawafanya wakulima kupata malipo yao halali na kwa wakati tofauti na ilivyokuwa zamani.

“Faida nyingine tutaweza kujua uzalishaji halisi ndani ya mkoa wetu kwani udhibiti wa usafirishaji korosho kwenda mikoa mingine kwa sasa haupo,” alisema Ndikilo.

Kipindi cha nyuma korosho ilishuka na kuuzwa shilingi 1,800 hadi 1,900 lakini kwa sasa korosho itauzwa kwa shilingi 3,300 kwa kilogramu.

Aliwaasa wakulima kuhakikisha wanakausha korosho zao ili zifikie viwango na ziwe zenye ubora unaotakiwa.

No comments:

Post a Comment