Sunday, November 18, 2018

WAKULIMA WA KOROSHO WA KIJIJI CHA KITAMA MJINI WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KUSIMAMIA BEI YA KOROSHO

Mkulima wa zao la korosho katika Kijiji cha Kitama Mjini kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara, Selemani Awadhi akiwalipa baadhi ya wakusanyaji wa korosho katika shamba lake hapo jana (Jumamosi Novemba 17, 2018) mara baada ya kupakia bidhaa hiyo katika magunia tayari kwa ajili ya usafirishaji katika maghala ya kuhifadhia zao hilo.
................................................


WAKULIMA wa zao la korosho katika Kijiji cha Kitama Mjini Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara wamempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na msimamo wa Serikali yake katika kupanga bei ya zao hilo na kuwadhibiti wafanyabiashara wasiojali maslahi ya Wakulima.

Wakizungumza na Mwandishi wa MAELEZO, Kijijini hapo jana (Jumamosi Novemba 17,2018) wananchi hao walisema hatua iliyochukuliwa na Serikali imeonesha juhudi za Rais Magufuli katika kuwasaidia wananchi wanyonge hususani wakulima ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakinyonywa na Wafanyabiashara kutokana na kununua mazao yao katika bei za chini.

Mmoja wa Wakulima hao Bw. Mohamed Aibu alisema juhudi zilizofanywa na Rais Magufuli katika kuwasaidia wakulima wa zao la korosho hazina budi kuungwa mkono na Watendaji wote wa Serikali wanaosimamia mnyororo wa thamani ya zao hilo kwani kwa sasa hakutakuwa na ukwepaji wa maagizo ya Kiongozi Mkuu wan chi.

Aliongeza kuwa zao la korosho ni miongoni mwa zao muhimu la kibiashara kwa wakulima wengi wa Mikoa ya Kusini ikiwemo  Mtwara na hivyo kuiomba Serikali kuendelea kuweka mkazo katika usimamizi na ufuatiliaji wa bei ya zao hilo kila msimu wa kilimo cha zao hilo unapoanza.

Naye Bi. Ashura Sefu anasema wananchi wa kijiji hicho wamefurahishwa na hatua ya kiutendaji iliyochukuliwa na Rais Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujumla kwani kutawaongezea ari na nguvu katika kuzalisha korosho bora zinazokidhi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aidha aliiomba Serikali kujenga kiwanda cha kubangulia korosho za wakulima hao katika kijiji hicho, kwani kulingana na takwimu zilizopo kijiji hicho ni moja ya vijiji vinavyoongoza kuzalisha korosho katika Wilaya hiyo.

Kwa upande wake Selemani Awadhi anasema tamko lilitolewa na Rais Magufuli litaamsha amri kwa wadau wa tasnia ya zao la korosho kuendelea kuzalisha korosho zilizozingatia viwango na ubora wa masoko ya ndani na nje, na hivyo kuiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika utafutaji wa masoko na pembejeo.

No comments:

Post a Comment