Wednesday, January 29, 2020

WAZIRI UMMY TANZANIA HAINA MGONJWA WA CORONA

Na. WAMJW-Dodoma

Mpaka sasa Tanzania haina Mgonjwa wala muhisiwa wa ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha Coromna (Hona kali ya mafua) hata hivyo kutokana na mwingiliano mkubwa uliopo hasa kibiashara na kijamii kati ya Tanzania na nchi za bara la Asia ikiwemo nchi ya China nchi inakuwa katika hatari pia ya ugonjwa huo.


Haya yamesemwa leo na Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akitoa tarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugponjwa huo jijini hapa.

“Ugonjwa huu unasababiswa na kirusi jamii ya Corona na ni kipya “Novel (New) Corona virus 2019” (2019-nCOV) ambacho ni tofauti na virusi vingine vya jamii hiyo ambavyo viliwahi kusababisha milipuko ya ugonjwa uliojulikana kama ‘SARS-CoV’ mwaka 2003 na MERS-CoV Corona Virus mwaka 2013”.Amesema Waziri Ummy.

Aidha, waziri Ummy amesema ugonjwa huo huambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingiwa na majimaji yenye virusi kutoka mtu mmoja kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya au kwa kugusa majimaji au makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na dalili za ugonjwa huo na dalili huanza kuonekana kati ya siku moja hadi kumi na nne tangu kupata maambukizo.


Hata hivyo ametaja dalili za ugonjwa huu ni pamoja na Homa, mafua, kuumwa kichwa, mwili kuchoka, kikohozi, kubanwa mbavu, maumivu ya misuli, vidonda vya koo, mapafu kuathirika, kupumua kwa shida na hata kifo.
 


“Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja, hivyo kama yalivyo magonjwa mengine yanayosababishwa na virusi, matibabu hufanyika kwa kuzingatia dalili zilizopo na ufuatiliaji wa karibu” Amesisitiza Waziri Ummy.

Wakati huo huo waziri huyo amewashauri wananchi kuchukua hatua ili kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuzingatia kanuni za afya na usafi ikiwa ni pamoja na kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua mwenye historia ya kusafiri katika nchi zilizokumbwa na mlipuko na kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo uliyovaa sehemu za mikono


“Kutokana na mwenendo na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo kipindi hiki cha mlipuko, Wizara inashauri kusubiri na kuepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na inapolazimu kusafiri basi

VULU ATAKA MICHEZO KUHAMASISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA.

Na Omary Mngindo, Kisarawe.  

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, amewaonba viongozi wa Vijiji na Vitongohi mkoani hapa kuandaa mashindano madogo ya kuhamasisha zoezi la uboreshaji wa daftari la wapigakura.

Vulu ametoa rai hiyo akiwa katika Kijiji cha Kisangile Kata ya Marui wilaya ya Kisarawe mkoani hapa, alipoambatana na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa UWT Sophia Gunia, ambapo amesema michezo ina nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa wananchi.

Alisema kuwa katika Mkoa wa Pwani kuanzia Februari Mosi mpaka saba mwaka huu kutakuwa na zoezi la uboreshaji wa daftari la wapigakura, litakalodumu kwa siku saba, hivyo kutokana na uchache wa siku amewaomba viongozi kuandaa mashindano hata ya kuwania sabuni.

"Kutokana na uchache wa siku za uboreshaji wa taarifa za wakazi kwenye daftari hilo, ningewaomba viongozi katika maeneo yao waandae mashindani madogo yatakayotumika kufikisha ujumbe kwa wananchi wetu, wajiandikishe ili wasipoteze sifa za kushiriki zoezi la kuchagua au kuchaguliwa," alisema Vulu.

Kwa upande wake Sophia amewataka wakazi wilayani hapa kutopuuzia zoezi hilo kwani ni la siku chache, hivyo wasipoteze nafasi hiyo muhimu kwa mustakbali wa nchi yetu, kwani ni fursa ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi za kisiasa.

"Tumekuwa na tabia ya kupuuzia maagizo yanayotolewa na serikali, tunao mfano mojawapo ni huu wa kitambulisho cha Taifa, zoezi hili lilitangazwa kwa muda mrefu lakini nananchi wamepuuzia lakini kwa sasa tunashuhudia wanavyohangaika," alisema Mwenyekiti huyo.

Nae diwani wa Kata ya Marui Selemani Mfaume amesema kuwa watafanya juhudi kubwa za kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu hiyo, ili isije ikajitokeza kama zoezi la kitambulisho cha Taifa.

"Ushauri wa mashindano nimeupokea nitakaa na viongozi wangu ngazi za vijiji kuandaa japo mashindano ya kuwania sabuni tutakayoyatumia kuwatangazia wananchi kuhusiana na uboreshaji wa daftari la wapigakura," alisema Mfaume.

SUBIRA MGALU AWAONYA WATAKAOUZA NGUZO ZA UMEME.



NA MWAMVUA MWINYI, KISARAWE.

NAIBU Waziri Wa Nishati ,Subira Mgalu ametoa tahadhali kwa vishoka na baadhi ya watumishi REA, ama shirika la umeme Tanesco kujiepusha na uuzaji wa miundombinu ya umeme na vifaa mbalimbali ikiwemo nguzo.


Ameeleza, endapo atabainika yeyote kujihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwakuwa anarudisha nyuma juhudi za serikali na ni uhujumu uchumi.


Akihitimisha ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa Peri -Urban wilayani Kisarawe, Subira alisema, msimamo wa serikali nguzo haziuzwi, hata kama mtumishi upo REA ama TANESCO.


Aidha Subira ,alitoa rai kwa wananchi wasithubutu kulipia nguzo au kufanya makubaliano yoyote nje ya utaratibu wa serikali.


Akizungumzia suala la vishoka wanaofoji vitambulisho ,alisema serikali pia imeweka msimamo ,endapo kuna mazingira hayo wananchi watoe ushirikiano ili kuwabaini wahusika.


Aliomba vyombo vya usalama vya ngazi husika kuliona hilo ni moja ya majukumu yao kubaini vishoka wanaouza miundombinu mbalimbali na vifaa na kubaini mtumishi yeyote atakaehusika.


Pamoja na hayo,Naibu Waziri huyo alitaka maeneo ya taasisi za umma ikiwemo shule na viwanda kupewa kipaombele kufikishiwa umeme na kumtaka mkandarasi aendane na kasi inayoendana na muda aliopangiwa ili jamii iondokane na adha ya kukosa huduma ya nishati ya umeme.


Nae diwani wa kata ya Msimbu, Mama Lilomo alifafanua, kata yake imeguswa na  umeme eneo la Homboza lakini bado kuna changamoto ya ukosefu wa umeme katika vitongoji saba.


Kwa upande wake ,Mkuu wa shule ya sekondari Christon ,August Minja alieleza kwamba, mradi huo utakapokamilika na kufika shuleni hapo, itakuwa ni chachu ya kuinua taaluma,pia aliipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais John Magufuli kwa kuhakikisha umeme unafika pembezoni na miji na vijijini.

Tuesday, January 28, 2020

VIJIJI 6 WILAYA YA KILWA VYAKUMBWA NA MAFURIKO.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Zaidi ya watu 4,500 katika vijiji sita vya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wameathirika na mafuriko kufuatia hali ya mvua inayoendelea katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Bagamoyo Kwanza Blog imetembelea katika kijiji cha njinjo na kukuta baadhi ya wananchi wakiwa wamekaa juu ya mapaa ya nyumba, miti na vichuguu kwa zaidi ya siku mbili mfululizo kwa ajili ya kunusuru maisha yao huku hali zao zikionekana kudhoofika kwa kukosa chakula.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya kilwa Christopha Ngubiagai alisema vijiji vilivyoathirika na mvua hiyo ni pamoja na Njinjo, kisima Mkika, kipindimbi , Luatwe mitole, Kikole, Njinjo B na Nakiu ambavyo vinapitiwa na Mto matandu.

Ngubiagai alisema zoezi la uokoaji linaendelea ambapo mpaka siku ya jana january 27, watu 1000 tayari wameshaokolewa na kuwekwa katika shule ya msingi kipindimbi wa ajili ya kuwahifadhi.

"Hali hii inatokana na kuzidiwa kwa mto matandu ambao unapita katika vijiji hivyo kunakotokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambapo kingo za mto huo kwa sehemu kubwa zimeharibika na hatimae mchanga kuingia mtoni na kufanya kina hicho cha mto kuwa kifupi hali inayopelekea maji hayo kuenea katika makazi ya watu" alifafanua Ngubiagai.

Ngubiagai pia alitumia fursa hiyo kuomba Serikali kuongeza vifaa vya uokoaji kwa ajili ya kuwaokoa wananchi waliopo maeneo ambayo hayawezi kufikika kwa urahisi pamoja na kuongeza kasi ya uokoaji

"Kutokana na ufinyu wa vyombo vya uokoaji bado watu wengi kama unavyoona bado hawajafikiwa pamoja na boti tulizonazo bado tunahitaji kuwa na faiba bot, ikiwezekana tupatiwe na helicopter ya kusaidia ukoaji, ukiangalia maeneo mbali mbali ambayo yameathiriwa na mvua hiyo"

Nae mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa huo , Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi akizungumza katika eneo la tukio alisema kwa sasa katika Mkoa huo hali sio nzuri hasa kwa Wilaya za Ruangwa, Liwale, Kilwa pamoja na Halmashauri ya Mtama.

Alisema kufuatia mvua hizo tayari watu sita wameripotiwa Kufa na maji yanayotokana na mvua hiyo huku akieleza kuwa huwenda idadi hiyo ya vifo ikaongezeka zaidi kutokana na hali ya mvua zinazoendelea kunyesha.

"Nimepokea taarifa kutoka kwa kamanda wa polisi Mkoa kuwepo kwa taarifa ya watu kufa maji, 2 kutoka Ruangwa, 2 mtama na 2 kutoka kilwa" Alisema Zambi.

Nae katibu tawala wa Mkoa wa Lindi Bi Rehema Madenge alisema kuwa tayari wameshafanya maandalizi ya chakula, dawa za dharula kwa ajili ya Magonjwa ya mlipuko endapo yatatokea kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Hata hivyo Madenge alitoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo za Serikali kwa kuwasaidia wahanga hao wa mafuriko kwa kuwaletea vyakula pamoja na magodoro kwa ajili ya kulalia katika maeneo waliyo watengea wahanga hao.

MTOTO WA DARASA LA TANO APOTEA BAGAMOYO.

Msichana aliyejulikana kwa jina la Radhia Jafari (pichani) mwenye umri wa miaka 10, anaesoma darasa la tano shule ya msingi Majengo wilayani Bagamoyo hajulikani alipo huku juhudi za kumtafuta zikiendelea.


Kwa mujibu wa taarifa za familia ya mtoto huyo walisema mtoto huyo alikuwa anaishi na mamayake mkubwa pamoja na babu yake mzaa mama katika mtaa wa Epiphany Bagamoyo mjini, Kata ya Magomeni.


Aidha, Taarifa zinasema kuwa, mtoto huyo ametoweka toka tarehe 20/01/2020, ambapo siku ya tukio mtoto huyo alitoka nyumbani kuelekea shule akiwa na sare za shule na kwamba hakurudi tena.


Juhudi za kumtafuta mtoto huyo zinaendelea na kwamba tayari taarifa yake imeripotiwa kituo cha Polisi Bagamoyo na kupewa namba BAG/RB/258/2020

Kwa yeyote atakaemuona atoe taarifa kituo cha polisi Bagamoyo, au kituo chochote cha polisi kilicho karibu nae, au awasiliane na familia kwa namba za simu  0714752915 / 0715450959