Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile akionyesha mafuta maalum kwa ajili ya kuwakinga wenye ulemavu wa
ngozi dhidi ya miale ya jua yanayotengenezwa na kitengo cha Kilimanjaro
Sunscreen Production kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile (kushoto) akihojiana na Bw. Longini Mtalo, Mteknolojia kutoka kituo
cha utengenezaji wa viungo bandia katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya
Kaskazini KCMC huku akiwa ameshika sampuli ya kiungo bandia
kilichotengenezwa na kituo hicho.
.............................................
Sekta ya afya inakua kwa kasi huku huduma muhimu
za afya kwa sasa zikiwa zinapatikana hapa hapa nchini”
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alipokua
akizungumza na watumishi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC)
iliyopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro jana Novemba 22, 2018.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Sekta ya Afya imepewa
kipaumbele cha hali ya juu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt.John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitatu mageuzi makubwa ndani
ya sekta ya afya yameanza kuonekana huku huduma za matibabu ya kibingwa yakiwa
zikipatikana hapa hapa nchini.
“Tunasimama hapa kifua mbele tukiona mabadiliko
katika hali ya upatikanaji wa dawa kuimarika zaidi, bajeti ya dawa imeongezeka
toka Shilingi Bilioni 30 mpaka Shilingi Bilioni 270 yaani mara tisa zaidi ndani
ya miaka mitatu” alisema Mhe.Naibu Waziri na kuendelea
“Tumeboresha vituo vya
afya takribani 300, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa na Vituo 8 vilivyoboreshwa
vilivyogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 na kwa mwaka huu 2018 Serikali
imeanza kujenga Hospitali za Wilaya 67 nchini”
Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali
imetenga Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya Hospitali mpya za Rufaa za Mikoa
ili ziweze kutoa huduma za kibingwa, kupunguza msongamano wa wagonjwa na
ucheleweshwaji wa huduma katika Hospitali za rufaa za kanda.
Naibu Waziri huyo Aliendelea kusema kuwa
fedha hizo Shilingi Bilioni 30 zitaelekezwa katika maeneo makuu matano ambayo
aliyataja kuwa ni kuhakikisha kila Hospitali ya Mkoa ina Kitengo cha dharura,
chumba cha upasuaji, kitengo cha uangalizi wa wagonjwa mahututi pamoja na
kitengo cha mama na mtoto.
“Hospitali hii inatakiwa kuhudumia wagonjwa
waliopata rufaa toka hospitali za mikoa ya jirani waje huku kupatiwa huduma za
matibabu na sio wagonjwa wa malaria na mafua alisema Dkt. Ndugulile.
Katika kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa
kwenye hospitali za rufaa za mikoa, Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeweka
maeneo muhimu katika mafunzo kwa watumishi wa kada ya afya huku akitaja
watumishi wenye kuhitajika zaidi kwa sasa kuwa ni madaktari wa magonjwa ya
ndani, watoto, wakina mama, upasuaji, mifupa pamoja na madaktari wa usingizi.
Kuhusu upatikanaji wa huduma za kibingwa,
Dkt.Ndugulile alisema mafanikio kuona huduma hizo zikiwa
zinapatikana hapa nchini tofauti na zamani “Tunafanya upandikizaji wa
figo pamoja na upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa wa watoto huduma ambazo
zilikuwa ni za kufikirika ndani ya miaka mitatu sasa zinapatikana hapa nchini”
alisema Dkt. Ndugulile.
Awali akitoa taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Rufaa ya KCMC Dkt. Gileard Masenga aliishukuru Serikali kwa
kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Hospitali hiyo “Licha ya
kumilikiwa na Taasisi ya kidini lakini Serikali imeendelea kutupatia wataalam,
misamaha ya kodi za malighali zinazoingizwa nchini ambazo hutumika kutengeneza
mafuta ya kuwakinga wenye ulemavu wa ngozi dhidi ya jua.
Aidha, Dkt.Masenga alisema hospitali yake
imetengewa Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya dawa za Saratani huku fedha
kiasi cha Shilingi Milioni 250 tayari zimeshapelekwa Bohari ya dawa kwa
ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto yupo Mkoani hapa kwa ziara ya kikazi
inayolenga kukagua shughuli za huduma ya Afya,Maendeleo ya Jamii pamoja na
kuongea na watumishi wa sekta hizo.
No comments:
Post a Comment