Thursday, November 15, 2018

WAZIRI UMMY AAGIZA KUANZISHWA DAWATI LA JINSIA, WATOTO NA WATU WENYE ULEMAVU

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akielezea Mikakati mbalimbali ya Serikali katika kumuwezesha mwanamke mlemavu  katika kongamano la Siku ya Wanawake wenye Ulemavu nchini iliyofanyika jana Novemba 14, 2018 Jijini Dodoma kwa kuandaliwa na Taasisi ya IKUPA Trust Fund.
...........................................

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza uanzishwaji wa Dawati la Jinsia, Watoto na Wenye ulemavu katika vituo vya polisi nchini.

Ameyasema hayo jana Novemba 14, 2018  jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kongamano la Siku ya Wanawake wenye ulemavu nchini yenye lengo la kuwawezesha wanawake wenye ulemavu.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imedhamiria kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wenye ulemavu nchini na sasa imeanzisha Dawati hilo.

“Tunalo Dawati la Jinsia katika Jeshi la Polisi ila kutokana na changamoto za wenzetu walemavu naomba Dawati hilo libadilike na liwe ni Dawati la Jinsia, Watoto na watu wenye ulemavu” alisisitiza Mhe. Ummy.

Pia Waziri Ummy  pia ametoa onyo kwa waajiri kutoka Taasisi za Serikali na binafsi watakaowanyima ajira watu wenye ulemavu kwa makusudi kwani hatua kali zitachuliwa dhidi yao.

Waziri Ummy amesema kuwa walemavu wenye sifa stahiki za kupata ajira sharti wapewe ajira wasibaguliwe kutokana na ulemavu wao.

Mhe. Ummy amesisitiza uwezeshaji kwa watu wenye walemavu hasa wanawake na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutoa mikopo yenye tija.

“Niwatake wakurugenzi wa Halmashauri kutoa mikopo yenye tija na sio laki mbili kwa kikundi kimoja ili kuofanikisha azma ya kuwezesha kiuchumi wanawake hasa wenye ulemavu” alisisitiza Mhe. Ummy.

Waziri Ummy pia amemuagiza Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii kuratibu uwepo wa uwakilishi wa wanawake wenye ulemavu katika majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika ngazi mbalimbali ili kutoa fursa sawa kwa wanawake wote.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju amesema kuwa Wizara inayosimamia masuala ya Afya inatakiwa kuanzisha chumba maalum kwa ajili ya wanawake wenye walemavu kujifungulia na kuruhusu wanawake hao kuja na wasaidizi katika vituo vya Afya na Hospitali.
 
“Naomba Mgeni rasmi hili liko ndani ya uwezo wako Wanawake wenye ulemavu wapate nafasi pekee ya kupata huduma za Afya ya Uzazi” alisisitiza  Bw. Mpanju

Aidha Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Tulia Ackson ameipongeza Taasisi ya Ikupa Trust Fund kwa kuziona changamoto za watu wenye ulemavu hasa wanawake na kuanzisha Kongamano ambalo litaleta changamoto ambazo zitasaidia kuleta majibu ya utatuzi wake yatakayowezesha ustawi wa walemavu nchini.

“Awamu hii ya Tano imekumbuka sana watu wenye ulemavu kwa kutoa fursa kwa kundi hili kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi naipongeza Serikali yetu” alisisitiza Dkt. Tulia.

Dkt. Tulia ameleza kuwa changamoto za watu wenye ulemavu hasa kwa watoto wenye ulemavu na katika fursa za mikopo, ajira elimu na sekta nyingine  uzingatie hasa mahitaji maalumu ya walemavu.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia Watu wenye ulemavu Mhe. Ikupa Stella Alex amewashukuru wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Taasisi yake ya Ikupa Trust Fund kwa kuwezesha kongamano la  Wanawake wenye Ulemavu kwani inahimiza Serikali na wadau kuzingatia changamoto zinazowakabili walemavu hasa wanawake.

Mhe. Ikupa ameongeza kuwa suala la watu wenye ulemavu lizingatiwe kwani ni kundi lenye changamoto nyingi hivyo tunahitaji ktoa kipaumbele katika kuwapa huduma stahiki. 

Nao baadhi ya wanawake wenye ulemavu nchini wameiomba Serikali kuendelea kuweka miundombinu rafiki itakayowezesha walemavu kupata huduma rafiki katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya.

Kongamano la wanawake wenye ulemavu 2018 limeadhimishwa ikiwa na Kauli mbiu isemayo “Haki sawa za Wanawake wenye Ulemavu katika kufikia Maendeleo Jumuishi ikiandaliwa na kuratibiwa na Shirika la Ikupa Trust Fund.
 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia Watu wenye ulemavu Mhe. Ikupa Stella Alex akiwashukuru wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Taasisi yake ya Ikupa Trust Fund kwa kuwezesha kongamano la  Wanawake wenye Ulemavu lililofanyika Jijini Dodoma kwa kuandaliwa na Taasisi ya yake ya Ikupa Trust Fund.

 
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Tulia Ackson akisalimiana na mmoja wa wanawake mlemavu mara baada ya kushiriki kongamano la  Wanawake wenye Ulemavu lililofanyika Jijini Dodoma kwa kuandaliwa na Taasisi ya yake ya Ikupa Trust Fund.

Baadhi ya wanawake wenye ulemavu walioshirki kongamano la  Wanawake wenye Ulemavu lililofanyika Jijini Dodoma kwa kuandaliwa na Taasisi ya Ikupa Trust Fund wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu( hayupo pichani)  akielezea Mikakati mbalimbali ya Serikali katika kumuwezesha mwanamke mlemavu  katika kongamano la Wanawake wenye ulemavu nchini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu(katikati)  Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Tulia Ackson( wa pili kulia)  Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia Watu wenye ulemavu Mhe. Ikupa Stella Alex (kulia)  na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amos Mpanju (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wanawake wenye ulemavu mara baada ya kumalizika kwa kongamano la  Wanawake wenye Ulemavu lililofanyika Jijini Dodoma kwa kuandaliwa na Taasisi ya yake ya Ikupa Trust Fund.

No comments:

Post a Comment