Sunday, November 25, 2018

HALMASHAURI YA KISARAWE KINARA UKUSANYAJI MAPATO 2018/19

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/19, ndio imekuwa kinara wa makusanyo kwa Halmashauri zote nchi. 

Halmashauri hiyo imeshika nafasi ya kwanza kiasilimia kwenye mapato yake kwa kukusanya kwa asilimia 53 katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu na ndio iliyoongoza kiujumla.

Mafanikio hayo yametokana na sababu kuu nne ikiwemo fursa ya ujenzi wa Reli ya kati ya kisasa(SGR).

Ujenzi huo umekuwa ni fursa kubwa kwa Halmashauri hiyo kutokana na kifusi kingi kimekuwa kikitoka Kisarawe na kuwezesha makusanyo makubwa ya mapato nje ya matarajio ya awali.
 
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa mapato ni kutokana na kuzuia uvujaji wa mapato kwa kuisimamia vyema mifumo ya kielektroniki.

Hiyo imedhihirika hata katika Hospitali ya wilaya Kisarawe hapo awali ilikuwa inakusanya mapato yasiyozidi Sh.Milioni sita kwa mwezi lakini kwasasa baada ya mifumo kuimarishwa na kuongezeka kwa umakini katika ujazaji wa fomu za bima ya afya,  sambamba na kuanzisha duka maalum mapato yameongezeka na kufikia wastani wa Sh.Milioni 45 kwa mwezi.

Kadhalika, usimamizi mzuri wa mapato katika vituo vya kukusanyia mapato vijijini umeimarika kutokana na watendaji kupewa onyo kwa kuonesha uzembe katika ukusanyaji wa mapato.

Pia Halmashauri hiyo kwasasa inakamikisha ujenzi wa Kituo cha mabasi ambacho kitazidi kuongeza mapato ya Kisarawe.

Novemba 24, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo akitoa taarifa kuhusu taarifa ya ukusanyaji mapato ya robo mwaka wa fedha wa 2018/2019 alitangaza kuwa Halmashauri hiyo imeongoza kwa upande wa Halmashauri za wilaya kwa kukusanya kwa asilimia 53.

Anasema kwa upande wa majiji, Halmashauri ya Jiji la Arusha ndilo lililoongoza kiasilimia ambapo limekusanya kiasi cha Sh.Bilioni 4.1 kati ya Sh. Bilioni.15.6 sawa na asilimia 26 ya malengo yao ya makusanyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19.

Aidha, Waziri Jafo anabainisha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa wingi wa kukusanya mapato ghafi ambapo limefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 14.4 kati Sh. Bilioni 68.6, sawa na asilimia 21 ya  malengo waliyojiwekea.

Anaongeza kuwa kwa upande wa Halmashauri za Manispaa iliyofanya vizuri zaidi ni Manispaa ya Musoma  na kwa Halmashauri za Mji zimeongozwa na Mbinga.

Jafo anaeleza kuwa makusanyo hayo kwa mikoa, Mkoa wa Simiyu unaongoza ukifuatiwa na Manyara, Lindi, Mara, Pwani, Arusha, Njombe,Dodoma, Mwanza na Geita.

Waziri huyo anataja Halmashauri zilizofanya vibaya zaidi kwa kukusanya chini ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi DC, Nanyamba TC, Nanyumbu DC, Newala DC,Tandahimba DC,Songea DC,Madaba DC, Rorya na Morogoro DC.

Aidha, kwa Upande wa Mikoa iliyofanya vibaya kwa kukusanya mapato kidogo ni Mkoa wa Mtwara, Ruvuma na Kigoma.

Anasema kwa mwaka wa Fedha 2018/19 Halmashauri zilipangiwa kukusanya Sh.Bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vua ndani na hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu Halmashauri zilikusanya jumla ya Sh.Bilioni 143.6 sawa na asilimia 20 ya makisio ya mwaka. 

Jafo anasema kwa mwaka wa fedha 2017/18 Halmashuri zilipangiwa kukusanya Sh.Bilioni 687.3 na hadi kufikia septemba 30 mwaka 2017 ziliweza kukusanya Sh.Bilioni 126.8 sawa asilimia 18 ya makisio ya mwaka.

“Kutokana na Takwimu hizo inaonyesha kwamba Halmashuri zimeongeza wingi wa mapato kwa kiasi cha Sh.Bilioni 16.7 na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kwa asilimia 2,” anasema Jafo.

Waziri Jafo anasema ukusanyaji wa mapato ndio kitakua kigezo cha kupimwa katika utendaji kazi wa viongozi hivyo kila mtu ajitathmini kulingana na mapato ya Halmashauri au Mkoa wake.

No comments:

Post a Comment