Tuesday, January 30, 2024

BARAZA LA MADIWANI LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 38.9 KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25

 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo limepokea na kupitisha bajeti ya shilingi Bilioni 38,982,000,000.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku shilingi Bilioni 6,482,058,127.00 ikitarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani na shilingi 32,496,016,000.00 ruzuku kutoka Serikali kuu.


Bajeti hiyo imepitishwa Tarehe 30 Januari 2024 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.


Akiwasilisha bajeti hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, ambae pia ni Diwani wa Kata ya Nianjema, Abdul Pyallah amesema ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji isimamie kikamilifu mikakati ya ukusanyaji mapato.


Akizungumza katika Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mhe. Mohamed Usinga, amemtaka Mkurugemzi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wakuu wa idara ambao watakamilisha miradi huku ikiwa na madeni.


Usinga alisema ipo tabia ya baadhi ya wakuu wa idara kutekeleza Miradi huku wakiwa wanakopa kwa wazabuni na kuisababishia Halmashauri kuwa na madeni yasiyo ya lazima.


Alisema ni Mkuu wa idara atekeleze Mradi wake kwa mujibu wa bajeti ilivyo na si vinginevyo.


Alisisitiza kwa kisema kuwa, Mkuu wa idara atakasababisha deni kwenye Mradi achukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka.


Nae Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo amesema atahakikisha anasimamia bajeti hiyo ili kufikia malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji pamoja na utekelezaji wa Miradi mbalimbali.



TAKUKURU KAGERA YAWANOA WAANDISHI KUELEKEA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA.

 

Na Alodia Babara

Bukoba

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera amewasihi waandishi wa habari mkoani humo kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika kuelimisha jamii na kufichua vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.


Mkuu huyo Pilly Mwakasege aliyasema hayo Januari 30, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Kagera ambapo amesema kuwa, wanawategemea waandishi wa habari kuwapa ushirikiano katika kuwapatia taarifa mbalimbali zinazohusu vitendo vya rushwa kwa sababu ni watu muhimu katika jamii na wanauwezo wa kufika kokote na wanaaminiwa sana na jamii.



Amesema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vitaleta mabadiliko kwa jamii kwani watapatikana  viongozi bora na si bora viongozi ambao watasimamia vizuri miradi ya maendeleo na kukemea viashiria vya rushwa.


Amewasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika mema yaliyofanywa na Serikali kuliko kuitumia tofauti kwani itakuja kuleta athari za rushwa na akaomba kupitia semina hiyo ili wakawe mabalozi na watoe ushirikiano kwa taasisi hiyo.


Aidha amesema  elimu ambayo itatolewa na Takukuru kupitia vyombo vya habari na kuwafikia wananchi itasaidia kujua kwamba  wanapaswa kuchagua kiongozi wa eneo lao ambao wanazitambua changamoto zilizopo kwa undani na watasimamia vizuri maendeleo yao.


Amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa wanapopigiwa kura ile nafasi waliyoipata siyo eneo la kutafuta fursa au mtaji bali ni sehemu ya kwenda kushirikiana na wananchi wao kuwaletea maendeleo. 


“Kiongozi anayetoa rushwa ni yule ambaye hajiamini na hakujiandaa kwa wananchi wake, mkoa wa Kagera tunataka uchaguzi utakapofanyika wachaguliwe viongozi wenye maadili mema watakaosimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi” amesema Mwakasege.


Kwa upande wake  mkuu wa dawati la elimu kwa Umma TAKUKURU mkoa  Esther Mkokota amesema kuwa, rushwa ni adui wa haki na kuwa inaminya haki za watu kuchagua au kuchaguliwa hivyo akasema waandishi wa habari waelimishe watu juu ya kuacha tamaa ambayo ni kisababishi kikubwa cha rushwa.


Amesema kuwa kuna watu wanapowaona wenzao wana mali wanazitamani mali hizo bila kujiuliza mali hizo walizipata kwa njia ipi na hivyo kusababisha wajihusishe na rushwa jambo ambalo litasababisha mtu kama huyo kuchukuliwa hatua za kisheria.


Mkokota ameeleza kuwa, jamii ijue kuwa rushwa ni njia ya mkato ambayo inatumika kufikia lengo na endapo watachagua viongozi kwa kupewa rushwa wajue watakuwa wamepata viongozi wasiokuwa na sifa, rushwa inazorotesha maendeleo ya nchi na miradi inajengwa chini ya kiwango kutokana na kusimamiwa na kiongozi asiye na maadili mema.


Ameongeza kuwa, wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachague viongozi bora wenye maadili watakaosimamia miradi ya maendeleo




Sunday, January 28, 2024

KILIMO SHADIDI CHA MPUNGA CHAANZA KUCHANGAMKIWA.


Na Mwandishi wetu- Mbeya.

Wakulima wa zao la mpunga wameeleza kufurahishwa na Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga, chenye kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mfumo wa kuongeza mpunga (SRI) ambao unapunguza  gharama za uzalishaji huku tija ikiwa inaongezeka  mara dufu ya kilimo cha kawaida.


Hayo yameelezwa  katika kikao Cha mwaka cha Wadau wa Kilimo shadidi kilichofanyika Januari 24-27 Jijini Mbeya katika viunga vya Kituo Cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Uyole.


Akielezea hili, Mkulima wa Skimu ya Mkula Wilaya ya kilombero Mkoani Morogoro Filbert Kadebe, amesema katika Kilimo cha kawaida alikuwa akipanda mbegu kilogramu 30 kwa hekari moja lakini kwa kutumia  Mfumo wa Kilimo Shadidi cha Mpunga  wenye kanuni ya kutumia kitalu mkeka anapanda mbegu kilogramu 2 hadi 3 kwa hekari moja.


Pia, Kadebe alisema upandaji wa mche mmoja katika kilimo shadidi unatoa machipukizi mengi ambayo hupelekea kuongezeka kwa mavuno ukilinganisha na upandaji wa Kilimo cha kawaida.


Kilimo shadidi cha mpunga  kinachojulikana kitaalamu  (System of rice Intesification- RSI) ni mchanganyiko wa teknolojia za kilimo cha mpunga wa umwagiliaji kwa kubadilisha mfumo wa uratibu wa mimea, udongo, matumizi ya maji na virutubisho kwa lengo la kuongeza tija.


Nchini Tanzania, Kilimo Shadidi Katika zao la mpunga ni matokeo ya utekelezaji wa mradi  wa mifumo ya uzalishaji mpunga inayokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi.


Mradi huo unatekelezwa na  TARI kwa kushirikiana na taasisi ya Utafiti ya Norway- Norwegian Institute  of Bioeconomy research (NIBIO) na taasisi ya Utafiti ya Swamination (MSSRF) ya nchini India.


Akielezea Mradi huo, Mratibu  wa  mradi ambaye pia ni Mtafiti Mkuu Kituo Cha Utafiti TARI Uyole, Dkt. Atugutonza Bilaro amesema kilimo  hicho kinatekelezwa katika Halmashauri tano ambazo ni Kilombero, Chalinze, Iringa Vijijini, Mbarali na Bunda.


Dkt. Bilaro amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tayari wamewafikia Wakulima mia tisa lengo ikiwa ni Katika kipindi Cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mradi wafikie Wakulima 4,500.


Naye kiongozi mwenza wa mradi kutoka taasisi ya (NIBIO) Prof. Udaya Sekhar anaeleza lengo la kukutana ni kujadili maendeleo ya mradi, na kuweka mipango ya kutekeleza katika kipindi cha mwaka wa pili.


kwa upande wake  Mtafiti, taasisi ya MSSRF Dkt. Ramasamy Rajkumar ameeleza kufurahishwa namna ambavyo wakulima na Wadau wengine wameanza kutumia elimu wanayofikishiwa na wataalamu.




Friday, January 26, 2024

BARAZA LA WAFANYAKAZI BAGAMOYO, LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 38.9 

 

Na Hamisi Hamisi, Zuhura Kassimu.Bagamoyo

Baraza la wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo limepitisha bajeti ya Shilingi Bilioni 38,978,074,127.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huku shilingi bilioni 6,482,058,127.00 ikitarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi Bilioni 32,496,016,000.00 ruzuku kutoka serikali kuu.


Bajeti hiyo imepitishwa januari 25,2024 katika kikao maalum cha kamati tendaji ya Baraza la wafanyakazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.


 Aidha, shilingi Bilioni 6,486,058,127.00 kutoka mapato ya ndani kati ya fedha hizo mapato huru ni Bilioni 3,417,946,627.00 na mapato fungiwa ni Bilioni 3,068,111,500.00 na makadirio hayo ni ongezeko la shilingi milioni 593,528,127.00 kutoka kiasi cha shilingi Bilioni 5,892,530,000.04 kilichoidhinishwa kutumika mwaka wa fedha 2023-2024 sawa na ongezeko la asilimia 10% 

 

Akiwasilisha bajeti hiyo, Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya Bagamoyo, Bi Huruma Eugene, amesema vipaumbele vimewekwa kupitia fedha za mapato ya ndani ikiwa ni Pamoja na kuongeza ukusanyaji kwa kuanzisha vyanzo vipya, kuimarisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira katika ngazi zote,kujenga uwezo wa jamii katika masuala ya jamii na kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa wajasiliamali wadogo, wanawake ,vijana na walemavu,kuboresha ubora wa elimu kwa kujenga miundombinu katika shule za msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya kwa kujenga miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya.


Akizungumza katika Baraza hilo mmoja wa wajumbe ameiomba Halmashauri kuwa na utaratibu wa kupandisha madaraja kwa watumishi wa kada mbalilimbali Pamoja na kuwalipa stahiki zao kwa wakati. “Naiomba Halmashauri kupitia ongezeko la mapato ya ndani  kuhakikisha wanawapandisha watumishi wa kada mbalimbali madaraja pamoja na kuwalipa stahiki zao ili kuongeza weledi katika utendaji kazi’’


Sambamba na hayo wajumbe wamemchagua  Ndg .Faraja Mponele kuwa katibu mkuu wa Baraza la wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Pamoja na wajumbe Sita watakaounda kamati tendaji  iliyopo chini ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Bagamoyo Mhe.Shauri Selenda.


Thursday, January 11, 2024

DC OKASH KUWACHUKULIA HATUA WAZAZI WASIOWAPELEKA WATOTO SHULE

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash amesema atawachukulia hatua Kali wazazi wote watakashindwa kuwapeleka watoto shule ifikapo Jumatatu tarehe  15 January,2024.

Akizungumza Kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya upokeaji wanafunzi katika Shule mbalimbali Halmashauri ya Bagamoyo alisema kuwa msako mkali utafanyika Kwa wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto shule.

" Niwaambie tu  ndugu zangu tutawashughulikia wazazi wote watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao Shule ifikapo Mwisho wa Wiki hii, na Jumatatu tutaanza msako mkali ". Alisema Mhe. Okash



DC OKASH AKEMEA UNYANYASAJI WA KIJINSIA BAGAMOYO.

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Halima Okash amekemea vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia unaendelea katika Wilaya ya Bagamoyo.

Akizungumza na wazazi pamoja na waalimu alipotembelea Shule ya Sekondari Nianjema Leo tarehe 10 Januari, 2024 alisema kuwa, kuna ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia katika maeneo mengi ya Bagamoyo ikiongozwa na Kata ya Mapinga pamoja na Nianjema.

"Niwaambie tuu kuwa, Mimi kama Mkuu nasikitishwa sana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea katika maeneo yetu hivyo hatutasita kuwachukulia hatua wahusika wote watakaobanika kujihusisha na vitendo hivyo.

Nawaomba wazazi muwe mstari wa mbele kuwalinda watoto wenu".Alisema Mhe. Okash.

Aidha Mhe. Okash aliwaomba wazazi kuwapeleka Shule watoto wote waliojiandikisha kuanza madarasa ya awali,la kwanza na kidato Cha Kwanza Kwa Sasa hakuna shida ya watoto kuripoti shuleni kwani Serikali Kwa makusudi imeondoa ada Ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata Elimu.

Aliwashauri walimu na wazazi washirikiane kuhakikisha kuwa watoto wanapata chakula shuleni Ili kuboresha Elimu.

" Natoa rai kwa walimu na wazazi  kushirikiana Kwa pamoja kupitia vikao vyenu kupanga Mipango ya kuwapatia watoto Chakula".Alisisitiza.

Ziara hiyo ya Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ni sehemu ya kukagua maendeleo ya  kuwapokea wanafunzi wa Shule za awali, msingi na kidato Cha Kwanza katika Kata mbalimbali ndani ya  Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.