Tuesday, June 23, 2026

TANROADS YATANGA BARABARA SITA ZA PPP KUUNGANISHA MIKOA YA DAR, PWANI, DODOMA, SINGIDA NA TANGA KM 969

 

Katika hatua nyingine kubwa ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Taifa, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umetangaza fursa za uwekezaji katika miradi sita mikubwa ya barabara yenye urefu wa kilomita 969 kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

 

Tangazo hilo la kimataifa la kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kubuni, kujenga, kugharamia, kuendesha, kutunza na hatimaye kukabidhi miradi hiyo kwa Serikali kupitia mfumo wa Design, Build, Finance, Operate, Maintain and Transfer (DBFOMT), linaendelea kudhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutumia nguvu ya sekta binafsi kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

 

Hatua hiyo pia inaakisi mafanikio ya mageuzi makubwa yanayosimamiwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) chini ya Mkurugenzi Mtendaji David Kafulila, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa miundombinu na huduma za kijamii nchini.

 

Miradi iliyowekwa mezani kwa wawekezaji ni pamoja na upanuzi wa Barabara ya Morogoro–Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 kuwa njia nne, Barabara ya Handeni–Kiberashi–Chemba–Kwamtoro–Singida yenye kilomita 384, upanuzi wa Barabara ya Chalinze–Segera–Tanga yenye kilomita 246 kuwa njia nne pamoja na ujenzi wa Kitonga Escarpment Bypass yenye kilomita 27.

 

Miradi mingine ni Dar es Salaam Port–Kibaha Expressway yenye kilomita 42 na Dar es Salaam CBD–Julius Nyerere International Airport Expressway yenye kilomita 10.

 

Kwa mujibu wa TANROADS, miradi hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari, kuboresha usafirishaji wa watu na mizigo, kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania na kuimarisha nafasi ya nchi kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Kwa ujumla, miradi hiyo ina urefu wa kilomita 969. Kwa makadirio ya wastani ambapo kilomita moja ya barabara inaweza kugharimu takribani Dola za Marekani milioni moja sawa na karibu tsh trilioni tatu za Kitanzania kwa zote.


TWPF YAKAGUA ENEO LAKE LA KIMKAKATI DODOMA

 

 

Na Oscar Mbuza, MNRT

 

BODI ya Mfuko wa Kuhifadhi Wanyawapori (TWPF) imetembelea kiwanja kinachomilikiwa na Mfuko huo  eneo la Njedengwa katika Manispaa ya Dodoma ambacho kitapangiwa matumizi yake hivi karibuni.

 

Msafara wa Bodi hiyo umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TWPF Profesa Jafari Kideghesho akiambatana na  Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora na baadhi ya wajumbe wa Bodi.

 

Wajumbe wengine ambao wameshiriki  ziara hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt. Eblate Mjingo na  Kamishna wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange.

 

Aidha ujumbe huo pia ulimjumuisha  Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCCA), Victoria Shayo aliyemwakilisha Kamisha wa Uhifadhi wa NCCA.

 

Akizungumza baada ya kukagua eneo hilo lililopo Kitalu Namba 16, lenye ukubwa wa mita za mraba 39,700, Profesa Kideghesho amesema ameridhishwa na usimamizi na uhifadhi wa kiwanja hicho ambacho kitapangiwa matumizi yake hususani kwenye maendeleo ya uhifadhi wa wanyamapori hivi karibuni.

 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Lobora amesema wizara italitumia eneo hilo kama eneo la mkakati la uendeshaji wa shughuli za uhifadhi wa wanyamapori nchini.

 

Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania ni wa kudumu maalum kwa ajili ya kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazohitaji fedha kwenye uhifadhi.

 

Madhumuni ya Mfuko ni kurahisisha na kusaidia uhifadhi wa wanyamapori, ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa. Bodi ya TWPF ina wajumbe tisa.

                


Monday, June 22, 2026

KATAMBI AWAONYA WAHALIFU NA MAANDAMANO HARAMU YA TAREHE 07

 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewaasa watu wanaotoa kauli za kichochezi katika mitandao ya kijamii, majukwaa ya kisiasa na maeneo mbalimbali ambapo kauli hizo za kibaguzi na kichochezi zinahusu Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi mbalimbali wa serikali au wa dini.

 

Waziri Katambi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waumini wa Msikiti wa Mukadam uliopo Kata ya Chang’ombe iliyopo wilaya ya Dodoma Mjini ambapo kumefanyika Mashindano ya Quran na Harambee ya Ujenzi wa Msikiti huo.

 

“Taifa hili limejengwa kwa maumivu makubwa ya waasisi, limejengwa kwa jasho na hata damu ilipobidi ili Taifa Tanzania liwepo, nitumie fursa hii kuwaomba sana na kuwaasa wale wote ambao wanatumia majukwaa ya kisiasa kuchonganisha wananchi, kuwajaza chuki, kuchochea lakini pia kuhamasisha kufanya uhalifu na wanaounda magenge ya uhalifu yanayolenga kuharibu taifa letu, niwasihi na kuwaomba waache mara moja kwasababu kufanya hivyo hakuna ambae atabaki salama tutaathirika sisi Watanzania wote na athari hii italiathiri taifa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.” amesema Waziri Katambi.

 

“Tutarudi nyuma kimaendeleo,tutashindwa kuswali, tutashindwa kwenda kanisani, tutashindwa kufanya kazi za kiuchumi, tutashindwa kujenga nchi yetu, tutashindwa kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, tuwakanye na kuwaelekeza vijana wetu wakaishi mwenendo mwema na uzalendo kwa taifa lao na pale yanapotolewa maonyo na maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama wasikaidi kwani kwenda kinyume ni kuvunja sheria, katiba na taratibu.” aliongeza Waziri Katambi.







VIONGOZI WA REA ZAMBIA, WAWASILI TANZANIA KWA ZIARA YA KIKAZI

 


Viongozi wa Mamlaka ya Nishati Vijijini (REA) kutoka nchini Zambia wamewasili nchini kwa ajili ya ziara ya kujifunza na kubadilishana ujuzi na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

 

REA Zambia ambao wameongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Zambia anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Arnold Simwaba wamewasili Tanzania Juni 21, 2026 katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Tanzania, Wilson Nyamanga pamoja na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA Tanzania, Mhandisi Jones Olotu, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa REA Tanzania, Renatus Msangira.

 

Uongozi wa REA Zambia utakuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya Siku 7 ambapo pamoja na vikao vya kubadilishana ujuzi, wajumbe hao wanatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini.






Saturday, June 20, 2026

SERIKALI YAAHIDI KUSIMAMIA HAKI ZA WAKIMBIZI

 


 

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

 

Serikali ya Tanzania imeahidi kuendelea kulinda, kusimamia na kutekeleza haki za binadamu ikiwemo haki za raia wa Tanzania na Wakimbizi kutoka nchi mbalimbali wanaohifadhiwa hapa nchini ambapo pia imesema itaendelea kusimamia Amani na Usalama ili madhila yanayotokea katika nchi nyingine yasitokee hapa nchini.

 

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Patrobas Katambi (MB) wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Tarehe 20 ya mwezi Juni, kila mwaka, huku kauli mbiu ya mwaka huu ikisema “Hadi Kila Mtu awe Salama”

 

Waziri Katambi akizungumza mbele ya Wakimbizi wanaoishi jijini Dar es Salaam ambao waliwawakilisha wakimbizi wanaoishi katika maeneo mbalimbali nchini amesema nchi ya Tanzania inajifunza kwa yaliyotokea nchi jirani huku akitoa ahadi ya serikali ya kuwahudumia Wakimbizi.

 

“Ni agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, watu wote ambao ni ndugu zetu Wakimbizi waliohifadhiwa hapa tutawahudumia hata pale itakapohitajika rasilimali za nchi yetu tutazitumia, Rais wetu amekua anafanya hivyo wakati wote hata pale tulipokosa ufadhili na fedha za wadhamini, UNHCR aliendelea kutushika mkono lakini wapo wengine ambao hawakupata tuliwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili wapate waongeze nguvu lakini zilipokosekana kabisa Rais wetu hakusita kuweka mkono wake ili Wakimbizi muendelee kuishi kwa amani na utulivu, tunawapenda ndugu zetu, mmetupa uzoefu mmetupa mifano na uhalisia na sisi tunajifunza kutoka kwenu” amesema Waziri Katambi

 

“Mmeeleza sababu zilizopelekea kukosekana kwa Amani katika nchi zenu, zipo sababu ambazo pengine zinafanana na zenu ikiwemo rushwa, kujipatia fedha kwa manufaa binafsi, utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na magendo yanayonufaisha wachache na kuumiza walio wengi, ubadhilifu, wizi wa mali za umma, kughushi na kufanya udanganyifu, uhalifu wa kiuchumi, makosa yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi, uhaini, uchochezi wa vurugu, vurugu za kisiasa, vyeo na mali, ubaguzi wa kidini, kikabila na ukanda, utapeli na dhulma kwa wananchi, unyanyasaji wa kijinsia.” aliongeza Waziri Katambi

 

Waziri Katambi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Katiba ya Mwaka 1977 na marekebisho yake chini ya Uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Bunge na Mahakama wataendelea kusimamia haki za binadamu, utii wa sheria, maslahi ya wananchi wote wakiwepo Wakimbizi.