Thursday, August 31, 2023

WAJUMBE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO WAJENGEWA UELEWA KUHUSU KANUNI ZA MADINI

 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo wamejengewa uelewa kuhusu Kanuni mbalimbali zinazosimamia Sekta ya Madini ili kuweka uelewa wa pamoja ikiwemo wizara kutoa taarifa kuhusu marekebisho yaliyofanywa kwenye Kanuni za Madini kuhusu Ushiriki wa Serikali kwenye Uchumi wa Madini.


Akitoa mada katika kikao hicho, Mwanasheria wa Wizara ya Madini Godfrey Nyamsenda amewaeleza wajumbe wa Kamati kuhusu Sheria zinazosimamia Sekta ya Madini na kuwaeleza kuwa ni pamoja na Sheria ya Madini, Sheria ya Baruti na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta pamoja na Gesi Asilia pamoja na Sheria nyingine za Nchi.


Aidha, amefafanua kuwa, kulingana na matakwa ya Sheria ya Madini, shughuli za uchimbaji wa madini ya vito zinapaswa kufanywa na watanzania pekee isipokuwa pale wanapotaka kuingia ubia na asiye Mtanzania, Sheria inamtaka mbia kumiliki si zaidi ya hisa za asilimia 50 na mtanzania kubaki na umiliki wa hisa za asilimia 50 kwenye madini hayo baada ya kupata ridhaa ya Waziri wa Madini.


Vilevile, ameeleza kuhusu taratibu za kisheria zinazopaswa kuzingatiwa kuomba na kupewa leseni za Madini ikiwemo utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini pamoja na utaratibu wa utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini


Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kutokana na wizara kuhamasisha uwekezaji, hadi sasa wizara imeweza kutoa leseni za uchimbaji mkubwa wa madini zipatazo 19 na kueleza kuwa, hadi kufikia mwaka 2025 miradi mikubwa ya madini ikiwemo ya Tembo Nickel, mgodi wa Nyanzaga na mingine itasaidia kuchangia maendeleo makubwa ya Sekta ya Madini.


Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza katika kikao hicho, amesema wizara itaendelea kufanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati. Ameongeza kuwa, wizara itaendelea kuweka mikakati ya kuiwezesha Sekta ya Madini kuchangia zaidi katika kuliingizia taifa fedha za kigeni ikiwemo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa na kuongeza kwamba, hivi sasa sekta ya madini inachangia takribani asilimia 56 ya fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi.


Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Simai Sadiki ameishukuru wizara kwa kutoa elimu hiyo kwa wajumbe wa kamati ambayo itawawezesha kuishauri wizara kikamilifu. 





SERIKALI IMEONYA MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII KUTUMIANA NYARAKA ZA SERIKALI- KIKWETE

 

Serikali imeonya matumizi mitandao ya kijamii kutumiana nyaraka za serikaki.


kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi Wa Umma na Utawala Bora, Ndg. Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali lililoulizwa na Jennyjerry Ntate (Mbunge) wa Viti Maalum , Bungeni Dodoma leo.


Akieleza Mh. Kikwete aliwakumbusha wabunge na wananchi kwa jumla kuwa mawasiliano serikalini yanasimamiwa na sheria na kanuni hivyo ni muhimu kwa wananchi kuzingatia taratibu hizo ili sheria zisiwabane na kuleta taharuki isiyokuwa ya msingi. 


Kufuatia kauli hiyo ya Serikali, Mbunge wa Viti Maalum Ndg.Mwakagendo akataka kujua ni jinsi gani serikali imejipanga kwenye ujenzi wa mifumo hasa ukizingatia teknolojia ndiyo inakwenda kwa haraka sana. 


Akijibu swali hilo , Naibu Waziri Kikwete alieleza kuwa wazi imeendelea kujenga mifumo mbalimbali ya tehama na uwepo wa sheria Namba 10/2019 umewezesha serikali kuwa na uhalali wa uundaji wa mifumo hiyo na hadi sasa mifumo mbalimbali imejengwa kusaidia mawasiliano serikalini na kurahisisha uchapaji kazi.





MANISPAA YA BUKOBA YATARAJIA KUPOKEA BILIONI 32 KUTOKA VYANZO VYA MAPATO MBALIMBALI.

 

Na Alodia Babara -ukoba. 


Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa mwaka 2023/2024 inatarajia kupokea na kutumia shilingi bilioni 32 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato.


Kiasi hicho cha fedha kimetajwa jana na mwenyekiti wa kamati ya fedha na Utawala Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gybson wakati akisoma taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo.


Amesema, mwaka 2022/2023 Manispaa ya Bukoba ilipanga kuidhinishiwa na kutumia shilingi bilioni 32 wakatumia shilingi bilioni 28.4 sawa na asilimia 89.


 "Kiasi hicho cha fedha ni kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo michango ya shule za sekondari, uchanguaji wa huduma za afya, ruzuku kutoka serikali kuu na wahisani wa maendeleo, hadi kufikia June 30,2023 Manispaa ilikusanya na kupokea shilingi bilioni 28.4 sawa na asilimia 89 ya makisio" amesema Gybson


Amesema kwa mwaka 2022/2023 makusanyo ya ndani walipanga kukusanya shilingi bilioni 3.5 zikakusanywa shilingi bilioni 3.2 sawa na asilimia 93.


Amesema halmashauri iliidhinishiwa kutekeleza miradi 52 ya maendeleo miradi 23 imekamilika, miradi 17 iko katika hatua za ukamilishaji na miradi 12 haijaanza kutekelezwa itatekelezwa katika kipindi cha robo ya kwanza mwaka 2023/2024.


Aidha diwani wa Kashai Ramadhan Kambuga amesema kamati ya fedha na Utawala wamebuni vyanzo vipya vya mapato ili Manispaa hiyo ipate fedha zaidi ya shilingi bilioni 3 ya sasa kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani.


Naye diwani wa kata ya Bilele Tawfiq Sharifu amesema kuwa, kiasi cha fedha shilingi milioni 5 kutoka mapato ya ndani zilizoidhinishwa na Baraza hilo kwa ajili ya kukarabati kila mwaka chumba kimoja cha darasa shule ya msingi Bilele ni kidogo kingeongezwa kutokana na uchakavu wa miundombinu ya shule hiyo ambayo ilijengwa tangu mwaka 1957.


Amesema, Manispaa ione umuhimu wa kuongeza kiasi cha fedha kwaajili ya  kukarabati vyumba zaidi ya kimoja kwa mwaka kwani vyumba hivyo vinaweza kusababisha hatari kwa watoto wao kutokana na kuchakaa na hasa katika kipindi cha mvua za vuli ambazo kwa Kagera zimeanza kunyesha.

Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gybson akitoa taarifa ya kamati ya fedha na Utawala katika Baraza la madiwani la Manispaa ya Bukoba.

Baraza la madiwani Manispaa ya Bukoba wakati likiendelea


RAIS SAMIA AZINDUA MATAWI YA BANK YA NMB NA PBZ PAJE ZANZIBAR.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt, Samia Suluhu HassanLeo Agosti 30, 2023 amezindua Tawi la Bank ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Tawi la Bank ya NMB yaliyopo Paje Zanzibar ambapo kwa Sasa Wananchi wa eneo Hilo watapata huduma mbalimbali za kifedha katika matawi Hayo.


Uzinduzi wa Tawi Hilo ni sehemu ya Tamasha kubwa la Burudani la Kizimkazi 2023 ambalo limeenda sambamba na Matukio ya Uzinduzi wa Miradi mbalimbali ya Maendeleo tangu lilipozinduliwa ikiwemo Elimu, Afya, Maji na Miradi mingineyo.


Tamasha la Kizimkazi 2023 litahitimishwa na Rais Dkt, Samia ambapo tangu Kuanza kwake limekuwa na neema kubwa kwa Wananchi wa Zanzibar.











MAGAZETI YA LEO ALHAMISI TAREHE 31 AGOSTI 2023.

 





























Wednesday, August 30, 2023

DAKTARI FEKI AKAMATWA MUHIMBILI

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili imemkamata mkazi wa Mbagala mkoani Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Mawa akijihusisha na utapeli kwa wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo.


Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa hospitali hiyo, Alfred Mwaluko amesema kuwa daktari huyo feki amebainika akiwa kwenye harakati za kuwatapeli wananchi wanaouguza ndugu yao aliyelazwa jengo la Mwaisela.


Kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka 35- 40 amesema ana takribani siku sita akifanya utapeli hospitalini hapo, na kueleza kuwa vazi la kidaktari alilianua wakati likiwa limeanikwa baada ya kufuliwa, na kitambulisho alitengenezewa na kijana aliyekuwa akipita eneo hilo.


Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Aminiel Aligaesha ametoa rai kwa watu wote wanaojihusisha na kutapeli wananchi katika eneo la hospitali kuwa ulinzi umeimarishwa na wakijaribu kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya usalama.

 

RAIS SAMIA YUKO SAHIHI KIKATIBA KUTEUA NAIBU WAZIRI MKUU


 Na Albert Kawogo


LEO hili Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri kwa kuteua Mawaziri wapya; kuwahamisha wengine; kuteua Manaibu Mawaziri na kuwahamisha wengine na kuwateua Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na kuwahamisha wengine.


Kingine na kikubwa zaidi ni uteuzi alioufanya Mhe. Rais Samia kumteua Dkt. Doto Biteko kuwa Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Hili ni kubwa kwakuwa limeanzisha mjadala kwa wadau, wakiwemo wanazuoni mbalimbali kudai kuwa uteuzi huo (wa Naibu Waziri Mkuu) umekiuka Katiba.


Kikatiba, Mhe. Rais yuko sahihi. Ibara ya 36, Ibara Ndogo ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Rais, pamoja na mambo mengine, kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inasomeka:


36.-(1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. 


(2) Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuziunaofanywa na Rais.


(3) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2), masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria yoyoteinayohusika, mamlaka ya kuwateua watu wengine wotewasiokuwa viongozi wala watendaji wakuu, kushika nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na pia mamalaka ya kuwapandisha vyeo watu hao, kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na mamlaka ya kudhibitinidhamu ya watu waliokabidhiwa madaraka, yatakuwa mikononi mwa Tume za Utumishi na mamlaka mengineyo yaliyotajwa na kupewa madaraka kuhusu nafasi za madaraka kwa mujibu wa Katiba hii au kwa mujibu wa sheria yoyote inayohusika. 


(4) Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) hayatahesabiwa kuwa yanamzuia Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu ya watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.


Ni wazi kuwa kabla ya leo ( achilia mbali wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi), hakukuwa na nafasi ya Naibu Waziri Mkuu. Leo, akitumia mamlaka yake kikatiba, Mhe. Rais ameanzisha nafasi hiyo ya Naibu Waziri Mkuu. Ili nafasi hiyo ifanye kazi, akamteua Dkt. Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.


Kwa mamlaka hayo hayo, leo hii hii, Mhe. Rais amefuta iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kuanzisha Wizara mbili: Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi. Na uteuzi wa Mawaziri; Manaibu Mawaziri na Makatibu Wakuu ukafanyika. Yote haya yamefanyika kikatiba.


Kimsingi, Katiba yetu ya sasa inaruhusu kuanzishwa na/au kufutwa kwa nafasi yoyote ile ya kimadaraka. Wengi wetu tunajua, kwa kutumia Katiba hii hii, Rais Mstaafu Mwinyi aliwahi kumteua Hayati Augustine Lyatonga Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Ilitumika Katiba hii hii na Ibara hii hii iliyorekebishwa mwaka 1984 na mwaka 2000.