Sunday, November 11, 2018

LUGOLA ASAFISHA JESHI LA POLISI, KIGOMA.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwaondoa katika madaraka Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma ambaye alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, Mkuu wa Operesheni  wa Mkoa huo, Mkuu wa Polisi  Wilaya ya Uvinza na Mkuu wa Intelejinsia wa wilaya hiyo.

Pia Lugola ameagiza askari wote wa kituo cha polisi Mpeta na Nguruka wilayani Uvinza wahamishwe haraka iwezekanavyo katika vituo hivyo.

Lugola ametoa kauli nzito kwa kuwaondoa katika nyadhifa zao maafisa wa juu wa jeshi hilo, kutokana na mapungufu aliyoyaona katika operesheni iliyofanyika mwezi uliopita ya kuwaondoa wakulima na wafugaji waliovamia ranchi za Taasisi ya NARCO ambao ipo chini ya Wizra ya Mifugo, ambayo katika operesheni hiyo askari polisi wawili na raia wawili waliuawa.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika  Kitongoji cha Mwanduhubandu, Kijiji cha Mpeta Wilayani Uvinza, leo, Waziri Lugola alisema viongozi hao wa Polisi wameshindwa kuifanya kazi hiyo kwa umakini ndio mana kulikua upungufu mkubwa katika operesheni hiyo, hivyo damu za waliouawa zinakua juu ya hao viongozi wa polisi mkoa na wilaya.

“Kutokana na hali hiyo, namuagiza IGP Sirro kuwaondoa kwenye madaraka hao wote niliowataja ifikapo kesho, na kesho Jumatatu nitakapo kuwa Dodoma nitakutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuona hatua nyingine za kinidhamu zitakazochukulia kwa hao niliowataja,” alisema Lugola.

Waziri Lugola aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi halina nia ya kuua mtu, kumuonea mtu, kudhulumu  mtu lakini pale inapotokea jeshi hilo limeshindwa kutekeleza wajibu wake vizuri, lazima yeye Waziri achukue hatua.

Hata hivyo, Lugola alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuvunjika moyo, litaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika kuhakikisha linapambana na uhalifu, kwa hayo ambayo yanayojitokeza hayana nafasi ya kuwakatisha tamaa wala kuwavunja moyo.

“Mimi Waziri wa Wizara hii, dhamana yangu na haya ninayoyafanya, vyombo vyangu vya ulinzi na usalama ninavyovisimamia msinione mimi kama mwanasiasa, msichukulie maagizo yangu na matamko yangu kama ya mwanasiasa, atyakaye jidanganya hivyo, itakula kwake,” alisema Lugola.

Lugola alioagiza waondolewe madaraka ni Mkuu wa Utawala wa Jeshi l aPolisi Mkoa wa Kigoma ambaye alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wakati operesheni hiyo ilipotokea, ACP Simon Ngowi, Mkuu wa Operesheni  wa Mkoa huo, SP Msembele, Mkuu wa Polisi  Wilaya ya Uvinza, SSP Mwakisambwe, na Mkuu wa Intelejinsia wa wilaya hiyo, InspektaDotto Daudi.

CHANZO FULL SHANGWE BLOG.

No comments:

Post a Comment