Sunday, March 31, 2019

KAZI YA KUREJESHA UMEME MLANDIZI PWANI YAENDA VIZURI.

Image may contain: 4 people, people standing, shoes and outdoor
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ameeleza kuridhishwa kwake na kazi kubwa iliyofanywa na TANESCO ya kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyokosa umeme kutokana na kuungua kwa transfoma ya Mlandizi yanapatiwa Umeme katika kipindi kifupi.


Hayo yalibainika wakati alipofanya ziara ya kukagua Kituo cha kupoza umeme cha Mlandizi mkoani Pwani kilichopata hitilafu tarehe 30/3/2019, majira ya Saa 1:50 asubuhi baada ya Transfoma katika kituo hicho kuungua na moto.


Akitoa maelezo kwa Kamishna, Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayesimamia mifumo ya Usafirishaji umeme kutoka TANESCO, Mhandisi Isaack Chanji, alieleza kuwa, maeneo yaliyoathirika na tukio hilo ni pamoja na Mlandizi yote, baadhi ya maeneo ya Chalinze, Kibaha, Kibamba, Mbezi kwa Msuguri na Kimara. 


Hata hivyo, maeneo yote hayo yalipatiwa Umeme kupitia vituo vya Ubungo, Chalinze na Mlandizi chenyewe baada ya kukamilisha matengenezo ya dharura.


Kamishna Luoga aliwataka Wataalam kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi ya ukarabati wa Transformer ya akiba yenye uwezo wa MVA 10 iliyopo katika Kituo hicho ifikapo tarehe 2/4/2019 ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana katika viwanda vilivyopo Kibaha pamoja na Mitambo ya maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu.


Aidha, aliitaka TANESCO kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto cha Mkoa wa Pwani ili kufanya uchunguzi wa chanzo cha moto huo pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha tatizo hilo halitokei tena.


Katika ziara hiyo, Mhandisi Luoga alikagua Kituo pamoja na kuongea na Wataalam wanaofanya kazi ya matengenezo katika kituo hicho akiwemo Mhandisi Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

WASICHANA 4,000 MKOA WA LINDI KUFIKIWA NA MRADI WA LISHE KWA WATOTO WA KIKE.

NA HADIJA HASSAN-LINDI

JUMLA ya Wasichana elfu 4000 kutoka Halmashauri ya manispaa ya Lindi na Nachingwea Mkoani Lindi wanatarajiwa kufikiwa na Mradi wa lishe kwa watoto wa kike (GIRLS POWERD NUTRITION) unaoendeshwa na  World Association of girls guide and girl scouts 


Hayo yameelezwa na Meneja wa Mradi huo  David Mbimila  leo Machi 31, 2019 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajewajengea uwezo wa usimamizi wa Mradi huo kwa Viongozi wa Girl Guide wa Manispaa ya Lindi


Mbumila alisema Mradi huo wa Lishe kwa watoto wa kike Duniani unafanyika kwa majaribio  katika Nchi tano ikiwemo Tanzania, Bagladesh, Sirilanka, Filipino na Madagaska


"kwa Tanzania Mradi huu unatekelezwa katika Mikoa sita ikiwemo Mkoa wa Dar-es-salaam, Tanga , Arusha, Lindi , Dodoma pamoja  na Mkoa wa Mara ambapo kwa Mkoa wa Lindi kwa kuanzia tutaanza na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi pamoja na Wilaya ya Nachingwea ambapo matarajio yetu ni kuwafikia wasichana elfu nne mpaka ifikapo 2020" alifafanua Mbimila


Mbimila aliyataja malengo makuu ya Mpango huo kuwa ni kutoa Elimu ya Lishe kwa watoto wa kike ili waweze kula vizuri, kukua vizuri, kuongeza nguvu kazi ya kitaifa


Alitaja malengo mengine ni kutaka kuishahuri Serikali kuweka Mada ya Lishe kwa Watoto wa kike katika vikao na mikutano yao wanayoifanya mara kwa mara , pamoja na kulipa kipaumbele swala la lishe kwa  Mtoto wa kike katika Sera na Sheria Mbali mbali ambazo wanazitengeneza


Nae kamishina wa Girls Guide Mkoa wa Lindi Grecy Chipanda alisema kuwa kati ya wasichana hao elfu 4000 watakaonufaika na Mradi  huo wasichana 2700 watatoka Halmashauri ya Manispaa ya Lindi huku 1500 watatoka Wilayani Nachingwea


"unaweza ukajiuliza ni kwanini Wasichana wengi wametoka Manispaa hii ni kwa sababu Viongozi wengi wa Mkoa tuko hapa , kwa hivyo bira shaka kwa kushirikiana kwa pamoja na viongozi wa Wilaya tunaweza kuunganisha nguvu zetu na kufanikisha mpango huu kufanyika vizuri" alisema Chipanda


Nae Mwenyekiti wa Girls Guide Mkoa wa Lindi Mwalimu mstaafu Zuhura Mohamedi alisema kuwa Baada ya mradi  huo wa Lishe kwa watoto wa kike  wa majaribio kumalizika mwaka 2020 matarajio yake ni kuona wasichana Wanashiriki kikamilifu katika masomo yao pasipokukosa kuhudhuria Darasani 


Alisema matarajio yao mara baada ya kumaliza kwa warsha hiyo walimu pamoja na viongozi wa girls guide walioshiriki mafunzo hayo wataenda kuwaelimisha wanafunzi pamoja na jamii kwa ujumla umuhimu wa kula chakula chenye lishe bora ili kumaliza changamoto zinazowakuta wasichana hasa wa umri kuanzia miaka 6 hadi 19 


Awali akifungua warsha  hiyo ya siku nne katibu tawala , utawala na rasilimali watu wa Mkoa wa Lindi  DKT Bora Haule alisema kuwa kama Mkoa wamefarijika kuona Mkoa wao ni miongoni mwa Mikoa sita inayotekeleza mradi huo, huku akieleza kwamba Mradi huo utakuwa unaunga mkono jitihada zinazofanywa na mkoa huo za kuongeza ufaulu kwa Watoto wakike sambamba na kutokomeza  mimba za utotoni kupitia kampeni ya "TUMSAIDIE AKUE, ASOME, MIMBA BAADAE"


Pamoja na mambo mengine Dkt Bora pia aliwataka washiriki wa Mafunzo hayo kwenda kuwajibika kikamilifu katika maeneo yao sambamba na kuwataka Wananchi wa Manispaa ya Lindi na wa Wilaya ya Nachingwea kuupokea mradi huo pamoja na kuwapa ushirikiano wa kutosha waratibu wakati wa kutekuleza Mradi huo

SERIKALI ITAFIKISHA UMEME KWA WATANZANIA WOTE.-SUBIRA MGALU.

Image may contain: 7 people, people sitting, table and outdoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kushoto), akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini wilayani Muheza (shati ya bluu-katikati), alipotembelea genge lake lenye vifaa vya kazi akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo Machi 29, 2019. Katikati-mwenye ushungi ni Mkuu wa Wilaya, hiyo Mhandisi Mwanaasha Tumbo na wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu.
.................................
Na Veronica Simba – Muheza

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwafikishia huduma ya umeme watanzania wote bila kubagua aina ya makazi yao na kwamba itaendelea kutekeleza jukumu hilo pasipo kukatishwa tamaa na yeyote.


Aliyasema hayo Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani Muheza, ambapo aliwasha umeme katika vijiji vya Mamboleo-Lusanga, Mamboleo-Nkumba na Misongeni. Vilevile, alikagua genge la Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani humo pamoja na kuzungumza na wananchi.


Naibu Waziri alisema kumekuwepo na maneno ya baadhi ya watu kubeza jitihada zinazofanywa na Serikali kuwaunganishia umeme watanzania wote hususani waishio vijijini pasipo ubaguzi, wakitoa sababu kwamba wenye nyumba za nyasi hawastahili kupatiwa huduma hiyo.


Akifafanua, alisema kuwa, wataalamu wa serikali wamekuwa wakihakikisha taratibu za usalama zinafuatwa wakati wa kuunganisha umeme katika nyumba za vijijini, hususani zilizoezekwa kwa makuti au nyasi.

 
Aliwataka wananchi kuondoa hofu kuwa madhara yanaweza kutokea katika nyumba za aina hiyo ambazo zimeunganishiwa umeme na badala yake wawapuuze watu wanaobeza jitihada hizo, na zaidi wautumie umeme kujiletea manufaa katika maisha yao.


Pia, Naibu Waziri alieleza kuwa, kazi ya kuwapelekea wananchi wa vijijini umeme inafanyika sambamba na zoezi la uhamasishaji wa kujenga makazi bora.


Alisema, mwananchi mwenye makazi duni akiunganishiwa umeme, anapata hamasa ya kuboresha zaidi makazi yake na hilo limekuwa likifanyika sehemu mbalimbali nchini kote.


“Maelekezo yetu kwa wakandarasi ni kutobagua nyumba ya aina yoyote. Watanzania wote wanahitaji umeme pasipo ubaguzi wa aina yoyote. Hakuna sababu ya mtu aliye karibu na miundombinu, halafu asiunganishiwe umeme,” alisisitiza.


Baadhi ya wananchi wenye nyumba zilizoezekwa kwa makuti wilayani Muheza na ambao wameunganishiwa umeme, akiwemo Musa Rashidi, mkazi wa kijiji cha Mamboleo, waliipongeza Serikali na kutoa shukrani nyingi kwa kuwapatia huduma ya umeme pasipo kuwabagua. Waliahidi kuboresha zaidi makazi yao.


“Naishukuru sana Serikali kwa kuniunganishia umeme katika nyumba yangu, maana kabla ya huduma hii, hali haikuwa nzuri hapa nyumbani. Nimefarijika sana,” alisema Musa.


Awali, akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Naibu Waziri alisema suala la kukatika-katika kwa umeme wilayani humo linatokana na njia inayotumika kusafirisha umeme, yenye msongo wa kilovoti 132 kuzidiwa nguvu kutokana na matumizi kuongezeka.


“Ndiyo maana serikali ikaja na mpango wa kujenga njia nyingine ya umeme yenye uwezo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi – Kibaha – Chalinze – Segera hadi Tanga ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme mkoani humu,” alisema Naibu Waziri.


Aidha, Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mkoani Tanga na nchi nzima kwa ujumla, kuboresha utoaji taarifa kwa viongozi na wananchi.


Aliwataka kutoa taarifa kwa wakati kunapokuwa na ratiba ya kukatika kwa umeme, ikiwa ni pamoja na kueleza umeme utakatika muda gani, kwa sababu gani, maeneo yatakayoathirika pamoja na hatua zinazochukuliwa kutatua tatizo husika.


Vilevile, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga, ambao wana utamaduni wa kuchoma moto maeneo mbalimbali kwa ajili ya kilimo, kuchukua tahadhari ili kutoathiri miundombinu ya umeme.


“Natoa rai kwa wananchi, unapohujumu miundombinu ya umeme ni kosa kisheria maana ni uhujumu uchumi. Na mkumbuke, serikali inatumia gharama kubwa kuwekeza katika miundombinu husika.”


Awali, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo, alimweleza Naibu Waziri kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikipata matatizo ya kukatika umeme mara kwa mara.

Naye Mbunge wa Jimbo la Muheza, Adadi Rajabu (CCM), alisema umeme wa REA umekuwa ni jambo la kufurahisha kiasi kwamba wale ambao hawajafikiwa na huduma hiyo wanalalamika. 


Hivyo, alimwomba Naibu Waziri kusimamia suala hilo ili vijiji na vitongoji ambavyo havijafikiwa, vipelekewe umeme mapema.


Taarifa ya TANESCO wilayani Muheza inabainisha kuwa; vijiji 87 kati ya 135 vya Wilaya hiyo tayari vina umeme ambapo ni sawa na asilimia 64. 


Mradi wa REA III Mzunguko wa I ukikamilika mwishoni mwa Juni mwaka huu, asilimia 75 ya vijiji vya wilaya husika vitakuwa na umeme.
 Image may contain: 1 person, standing, wedding and outdoor
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisalimiana na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza, alipowasili kwa ziara ya kazi, Machi 29, 2019. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya, Mhandisi Mwanaasha Tumbo.
 Image may contain: 3 people, people standing and outdoor

 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kulia) akimpa mkono wa pongezi mkazi wa kijiji cha Mamboleo-Nkumba, wilayani Muheza, Musa Rajabu, baada ya kumuwashia rasmi umeme katika nyumba yake, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo na wa pili-kushoto ni Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu.
 Image may contain: 3 people, including Subira Mgalu, people on stage and outdoor
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mamboleo-Lusanga, wilayani Muheza, kabla ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji hicho, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
Image may contain: one or more people, people standing, people on stage, crowd and outdoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akiwaonesha wananchi wa kijiji cha Mamboleo-Lusanga, wilayani Lushoto, kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) na kuwaeleza matumizi pamoja na faida zake, akiwa katika ziara ya kazi Machi 29, 2019. Naibu Waziri aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
Image may contain: 12 people, including Subira Mgalu, people smiling, people standing
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa ameshika taa ya Chemli na Kibatari, alizokabidhiwa na mkazi wa kijiji cha Misongeni wilayani Muheza (kulia kwa Naibu Waziri); baada ya kumuwashia rasmi umeme katika nyumba yake, Machi 29, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.