Friday, May 31, 2019

WAISLAMU WATAKIWA KUWASAIDIA MASIKINI.

 Mwenyekiti wa Taasisi ya  Adullah Aid Tanzania, Arif Yusuf
 ..........................................

Na Shushu Joel,chalinze.

TAASISI ya Miraj Islamic Centre yenye makao yake mkuu jijini Dar es Salaam imetoa wito kwa watu wote walio na nafasi ya kipato kuweza kuwasaidia wasio na kipato kama ilivyoagizwa katika vitabu vya Mungu. 


Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sheikh Arif Yusuf Abdulrehman maarufu Arif Tanzania alipokuwa akizungumza na baadhi ya waislamu wakati wa zoezi la kugawa futari kwa wakazi wa vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.


Arif, alisema kuwa Taasisi yake imekuwa miongoni mwa taasisi za kuigwa ndani na nje ya Tanzania kwa jinsi inavyojitolea kuwasaidia watanzania wote bila ya kujali dini zao wala kabila huku lengo likiwa ni kuwaonyesha wale wasio na uwezo kuona ni sawa na wenye uwezo.


"Unaposaidia wenzako Mwenyezi Mungu anakuongezea kutokana na jinsi wale unaowasaidia wanavyokuombea uweze kupata ili uendelee kuwasaidia zaidi"Alisema Arif Tanzania. 


Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki cha mwezi huu wa Ramadhani taasisi ya Miraj Islamic imewezesha sehemu mbalimbali kwa ajili wananchi vyakula na tende kwa baadhi ya mikoa kama vile Arusha, Pwani, Mwanza, Kigoma, Zanzibar na Mikoa mingine kwa kusudi la kuwasaidia wasio na uwezo wala kipato ila wanafunga Ramadhani.


Aidha alisema kuwa Taasisi yake imekuwa msaada mkubwa kwa serikali kutokana na jinsi inavyojitoa katika masuala ya kusaidia watu mbalimbali ili waweze kujikwamua katika maisha yao, watu hao ni pamoja na kuwasaidia usafiri walemavu, vijana kuwapatia mashine za kukamulia juice na wengine kuwapatia pikipiki kwa ajili ya kufanya shughuli za boda boda, kinamama kuwawezesha kwa Vyerehani ya ushonaji. 


Hivyo kama kila mwenye nafasi ya kipato akijitolea kwa moyo mmoja basi watakuwa wamewafikia watanzania wengi na kuwawezesha ili nao waondokane na umasikini walionao. 


Pia Arif Tanzania ameipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli kwa jinsi inavyofanya kazi zake na Viongozi wa Dini zote na kuwakomboa watanzania wa hali za chini. 


Kwa upande wake Ashura Juma (81) mkazi wa vikindu katika wilaya ya mkuranga mkoani Pwani ameipongeza taasisi ya Miraj Islamic Centre kwa jinsi inavyojitolea katika kutoa misaada mbalimbali kwa wanyonge.


 Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kupitia taasisi hiyo familia yake imekuwa moja ya wanufaikaji wakubwa kwa kupata misaada mingi ikiwemo Chakula kwa ajili ya futari, fedha na mahitaji mengine mengi ya kibinadamu. 


Aidha Mama huyo amemtaka Mwenyekiti wa taasisi hiyo Arif Tanzania kuendelea na tabia hiyo ya kujitolea kwani wanufaika wako wengi na wataendelea kumuombea ili aweze kupata. 


Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa halmashauri ya chalinze katika wilaya ya bagamoyo, Mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete amesema kuwa misaada hiyo inayotolewa na taasisi hiyo imekuwa na tija kubwa kwa waumini wa dini ya kiislamu kutokana na uhitaji wa futari kwenye kipindi hiki. 


Mbali na hilo Kikwete alisema kuwa pongezi hizo si kwa wananchi bali hata serikali imekuwa ikinufaika na Arif Tanzania kupitia taasisi zake zinazojitolea kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya wanyonge. 


"Kutokana na jinsi taasisi hii inavyojitolea katika ufanikishaji wa wa misaada ni lazima sie kama wawakilishi tuisemee vizuri ili wengine wajitokezw "alisema

SERIKALI YA MAREKANI YATOA MISAADA YENYE THAMANI YA DOLA 750,000 ILI KUTENGENEZA AJIRA KWA VIJANA WA VIJIJINI.

Bibi Abella Bateyunga (kulia) kutoka Tanzania Bora Initiative akipokea hundi ya shilingi milioni mia mbili na tisa elfu hamsini na saba mia sita sabini na nne, 209,057,674. ikiwa ni ruzuku ya Vijana kwaajili ya kujiendeleza, kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, wa pili ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo akifuatiwa na Mkurugenzi wa Mission wa USAID, Andrew Karas, kutoka sekta binafsi ni Mtaalamu wa Mradi wa Vijana, Joyce Mndambi, (PICHA NA UBALOZI WA MAREKANI).
 
Mkurugenzi wa Mission wa USAID, Andrew Karas, akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi hundi kwa vijana iliyofanyika Mkoani Mbeya. (PICHA NA UBALOZI WA MAREKANI).
....................................

 Serikali ya Marekani imetoa misaada yenye thamani ya dola 750,000 kwa taasisi tisa ambazo zinasaidia utengenezaji wa ajira, ujasiriamali, uongozi, na maisha bora kwa vijana.


Misaada hiyo imetolewa na mradi wa Inua Vijana wa Feed the Future Tanzania , inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na wanatarajia kutengeneza ajira 950 kwa vijana katika makampuni 700 mapya au ambayo yanaongozwa na vijana katika mikoa ya Iringa, Mbeya, na Zanzibar.


Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andrew Karas, na Mheshimiwa Suleiman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), walikabidhi misaada hiyo kwa taasisi husika.


Wakati wa hotuba yake, Bwana Karas alibainisha kuwa “Kuwekeza katika uongozi wa vijana nchini Tanzania ni kipaumbele cha USAID na Serikali ya Tanzania.


"Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana, na idadi ya wananchi wake inatarajiwa kuongezeka mara mbili ndani ya miaka 25 hadi 30 ijayo.


Jitihada za makusudi zinahitajika kwa serikali, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha kuwa nguvu, vipaji, na matumaini ya vijana wa leo, pamoja na kizazi kijacho, zinafanya Tanzania kuwa mahali pa mafanikio kwa wote.”


Mradi wa Inua Vijana unahamasisha vijana wa vijijini kushiriki katika sekta ya kilimo nchini Tanzania na kuwapatia fursa za kiuchumi vijana wenye umri wa miaka 15-35 pamoja na kuhamasisha uongozi na mienendo ya kiafya.


Kupitia misaada hii, Inua Vijana ya Feed the Future Tanzania itabadili changamoto kuwa fursa kwa vijana wa vijijini kuongoza na kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Tuesday, May 28, 2019

WASICHANA WAJENGEWA UWEZO NA ROOM TO READ.

 Meneja wa Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Taasisi ya Room to read, Zamaradi Saidi, akizungumza na wasichana, wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalinze.
 
Meneja wa Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Taasisi ya Room to read, Zamaradi Saidi, alipokuwa akizungmza na mwandishi wa BAGAMOYO KWANZA BLOG.
...................................... 

Taasisi ya Room to read Tanzania imeandaa semina kwa wasichana wanaosoma shule za sekondari Mkoani Pwani ili kuwajengea uweza wa maarifa ya vitu vya kufanya baada ya kumaliza masomo.


Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kufungua semina hiyo, Meneja wa Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Taasisi ya Room to read, Zamaradi Saidi, amesema wamekuwa wakiandaa semina kama hizo za ujasiriamali kwa wasichana ili watakapomaliza masomo yao waweze kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira.


Alisema jamii imejenga mazoea ya kusubiri kazi za kuajiriwa hali inayopelekea hata kijana aliyemaliza elimu ya chuo kikuu anashindwa kuendesha maisha yake mpaka apate kazi ya kuajiriwa.


Alifafanua kuwa, kufuatia dhana hiyo iliyojengeka katika jamii, Taasisi ya Room to read imekuja na mpango wa elimu kwa msichana ambao ndani yake wasichana wanafundishwa mbinu za kujiajiri.


Alisema kuwa, Room to read imekuwa ikitafuta walimu wa aina mbalimbali wa ujasiriamali ili wasichana hao pamoja na elimu ya sekondari wanayopata wawe na elimu ya ziada ya kujiajiri pindi wanaposhindwa kuendelea na masomo au kukosa kazi za kuajiriwa.


Aidha, aliongeza kuwa, elimu wanayopata wasichana hao tayari watakuwa na uhuru wa kuchagua aina tatu za mfumo wa maisha ili kuendesha familia zao.


Alizitaja aina hizo tatu za mfumo wa maisha kuwa ni kujiajiri, kuajiriwa na kujiajiri pamoja na kuajiriwa, ambapo uhuru huo wa kuchagua haupatikani ispokuwa kwa mtu ambae tayari amejitosheleza katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu ya darasani na ujasiriamli.


Alifafanua kuwa, Mradi wa elimu kwa msichana ambao ndani yake kuna elimu ya fedha na ujasiriamali, umelenga kumfanya msichana atambue kuwa, anaweza kujiajiri, kuajiriwa au vyote kwa pamoja.


Aliendelea kusema kuwa, miongoni mwa elimu wanazopata wasichana hao kupitia wawezeshaji wa semina hizo ni pamoja na nidhani ya matumizi inayokwenda sambamba na uadilifu katika matumizi.


Alisema mtu yeyote ili aweze kufanikiwa kuanzisha au kuendeleza mtaji ni lazima awe na uadilifu katika matumizi ya fedha na sio kutumia bila ya mpangilio.


katika semina hiyo iliyofanyika shule za skeondari Matimbwa na Chalinze wawezeshaji wa aina mbalimbali wamealikwa kwaajili ya kufikisha masomo ya ujasiriamali sambamba na uwekaji akiba kwaajili ya kuanzisha na kuendeleza mitaji.


Wawezeshaji kutoka Benki ya NMB wameweza kutoa somo la umuhimu wa kuweka akiba kwaajili ya kutimiza malengo mbalimbali ya kujiendeleza.


Waliwaeleza wasichana hao kuwa, ili kuweza kufanikiwa katika malengo mbalimbali lazima kuwa na nidhamu ya fedha ambapo unapaswa kujua mapato, matumizi, faida na hasara.


Kwa upande wao wasichana waliopata elimu hiyo kutoka shule ya Sekondari Chalinze na Matimbwa wilayani Bagamoyo, walisema wamefaidika sana na elimu hiyo ambayo imewatoa gizani.


Walisema kwa sasa wanajua kuanzisha biashara, kutafuta masoko na namna gani kuandaa bidhaa ili mteja iweze kumvutia.


Mradi wa elimu kwa msichana chini ya Room to read Tanzania umejikita katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuwasaidia wasichana wanaotoka kwenye mazingira magumu msaada wa vifaa vya shule, kuwapa stadi za maisha wasichana wote, kuwapa ushauri wa jumla kuhusu maisha yao ya shule na baada ya shule.


Hata hivyo elimu hiyo inaendelea pia kwenye jamii ambapo Room to read hufanya semina na wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili kuwaeleza umuhimu wa kumsaidia msichana kuweza kumaliza elimu yake ya sekondari na kupata stadi muhimu ambazo zitamsadia kufanya maamuzi sahihi za maisha yake.

 Muwezeshaji, Richard kutoka NMB akisisitiza  jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kuweka akiba.
 
Muwezeshaji, Rashid Shomvi, kutoka NMB akiwasilisha mada kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha, semina hiyo iliandaliwa na Room to read na kufanyika Shule ya Sekondari Chalinze.

 
Wasichana, wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalinze, wakinyoosha mikono kama ishara ya kuelewa somo lililofundishwa na muwezeshaji.