Tuesday, November 27, 2018

MHE HASUNGA ATAKA MBOLEA IWAFIKIE WAKULIMA KWA WAKATI


Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza jambo wakati alipotembelea kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea
ya Yara Tanzania Ltd ambayo kwa nchini Tanzania Makao makuu yake yapo Jijini Dar es salaam, Leo tarehe 27 Novemba 2018. (Picha zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
....................................................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amewataka
wafanyabiashara kusambaza mbolea haraka iwezekanavyo ili ziwafikie kwa wakati wakulima kwani msimu wa kilimo umeanza.

Mhe Hasunga ameyasema hayo tarehe 27 Novemba 2018 wakati
alipotembelea kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea ya Yara Tanzania Ltd ambayo kwa nchini Tanzania Makao makuu yake yapo Jijini Dar es salaam.

Waziri Hasunga ametoa wito kwa Taasisi zinazohusika na
upakuaji wa mizigo bandarini kufanya kazi ya upakuaji kwa haraka ili mbolea ziwafikie wakulima kwani msimu wa kilimo tayari umeanza.

Alisema kuwa sio jambo jema mbolea inayotakiwa kuwa
mashambani kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo kuendelea kukaa bandarini kwani kwa zaidi ya wiki moja.

“Kadri mbolea inavyochelewa kuwafikia wakulima
itasababisha kuongezeka kwa gharama zisizo na tija kwani atakayeumia ni mkulima jambo hili halipaswi kutazamwa kama jambo la kawaida badala yake wahusika wote watekeleze majukumu yao ipasavyo” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Wakulima wengi vijijini hawajui mambo ya kukaa muda
mrefu kwa mbolea bandarini wao wanachokijua serikali inatakiwa kuwapatia mbolea msimu wa kilimo unapofika, na mbolea inahitajika haraka kwani kilimo cha Tumbaku kinaendelea na tayari malalamiko yameanza”

Pamoja na mambo mengine Mhe Hasunga ameipongeza
kampuni hiyo ya mbolea ya Yara Tanzania Ltd, ambayo imewekeza katika maabara ya kupima udongo ili kuweza kutambua virutubisho vilivyopo na vinavyokosekana kwenye udogo. 

Meneja wa kampuni hiyo nchini Tanzania na Rwanda Bw
William Ngeno, alisema “lengo kuu la kampuni ya Yara Tanzania kuweka
maabara ya udongo, ni kuweza kuwapa wateja wao huduma nzuri na mpangilio sahihi wa lishe bora na linganifu ya mimea”

Alisema mara baada ya matokeo ya udongo kampuni
hiyo kupitia wataalamu wake hutoa ushauri kwa wakulima nini cha kufanya kulingana na zao lililolimwa au linalotarajiwa kulimwa. 
Aidha, alimpongeza Waziri huyo wa Kilimo kwa kutembelea kampuni hiyo kujionea hali ya utendaji kazi.

Mbolea za YARA zimegawanyika katika makundi
makuu matano Yara Mila:  Kundi hili lina aina za mbolea zenye
madini makubwa matatu NPK  (Nitrogen, Phosphorus, Potassium), Yara
Liva:  
Kundi hili lina aina za mbolea zenye asili ya Calcium
Nitrate 
ambazo ni kama vile Nitrabor, Tropicoti na
Calicinite, Yara Bela:  Kundi hili ni Kundi lenye mbolea zenye
asili ya Ammonium Sulphate Nitrate, zina Nitrojen na Sulphur ambazo ni Sulfan,

Yara Vita:  Kundi hili ni la mbolea zile zenye madini
yanayohitajika kwa kiwango kidogo na mmea (MicroNutrients) lakini muhimu katika ukuaji wa mmea sambamba na Yara Vera:  Kundi la tano ni mbolea za UREA.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua kiwanda cha kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea ya Yara Tanzania Ltd ambayo kwa nchini Tanzania Makao makuu yake yapo Jijini Dar es salaam, Leo tarehe 27 Novemba 2018.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiagana na Meneja wa Kasmpuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea ya Yara Tanzania Ltd Bw William Ngeno wakati wa ziara yake ya kikazi Leo tarehe 27 Novemba 2018 Jijini Dar es salaam

No comments:

Post a Comment