Tuesday, December 24, 2019

WANANCHI MOROGORO WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWA JESHI LA POLISI

Na.Farida Saidy,Morogoro

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP)  wilbrod mutafungwa, ametoa wito kwa wanachi mkoani humo, kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili taarifa zote zinazohusu viashiria vya uhalifu  vifanyiwe kazi mara moja.


Ametoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari  amesema hali ya mkoa huo ni shwari na kwamba hakuna matukio makubwa yanayotishia usalama wa raia na mali zao, na kuongeza kuwa bado wanaendelea na jitihada mbalimbali za kukabiliana na matukio ya kiuhalifu na wahalifu.


Mutafungwa amesema katika msimu huu wa sikukuu za krismas na mwaka mpya polisi mkoa wa morogoro wamejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanahudhuria katika nyumba za ibada na kushiriki ibada za kusherehekea siku hizi kwa utulivu na amani.


Hata hivyo, kamanda mutafungwa amesisitiza kuwa kutakuwa na ulinzi wakutosha katika nyumba za ibada, majengo ya serikali, benki, masoko, kumbi za starehe, viwanja vya michezo pamoja na kuimarisha doria katika barabara zote kuu pamoja na barabara za mitaani, kwamba kutakua na doria za masafa marefu, pamoja na doria za miguu na doria zinazoambatana na wanyama wakali (mbwa wa polisi).


Katika hatua nyingine jeshi la polisi limetoa motisha kwa askari wake ambapo walishiriki kuokoa maisha ya baba na motto ambalo limetokea siku chache zilizopita katika maporomoko ya nguzo campsite.


Kwa upande wake diwani wa kihonda khamisi kilongo, ambapo ndio wanapoishi baba huyo na mwanaye amelipongeza jeshi la polisi kwa hatua iliyochukua na kusema ni hatua kubwa katika kuleta hamasa kwa askari katika kufanya vizuri na ameomba hii iwe zoezi endelevu kimkoa na ikiwezekana hata taifa zima.


Onesmo kahemere ni miongoni mwa askari walioshiriki uokoaji ameelezea jinsi hali ilivyokua ambapo amesema kama askari licha ya kuwa alikua akitimiza wajibu wake lakini pia aliguswa kibinaadamu kufanya hivyo.

MLANDIZI QUEEN'S YAVAMIA MKUTANO WA UWT


Pichani Zuhura Mizava mmoja wa wajumbe wa (UWT) Kibaha Vijijini akisaini karatasi ya kuchangia klabu ya soka ya Wanawake ya Mlandizi Queen's inayoshiriki Ligi kuu ya Wanawake, kulia ni Nahodha wa timu hiyo Wema Richard. Picha na Omary Mngindo.

Picha ya kwanza Diwani wa Kata ya Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Euphrasia Kadala akisaini karatasi ya kuchangia klabu ya soka ya Wanawake ya Mlandizi Queen's inayoshiriki Ligi Juu ya Wanawake, kushoto Nahodha wa timu hiyo Wema Richard. Picha na Omary Mngindo.
........................................

Na Omary Mngindo, Mlandizip

UONGOZI wa klabu ya soka ya Wanawake ya Mlandizi Queen's inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ya Mlandizi Mkoa wa Pwani, umevamia Mkutano wa Jumuia ya Wanawake (UWT) wilayani hapa wakihitaji ushirikiano wao.

Nahodha wa timu hiyo Wema Richard akiambatana na mchezaji mwandamizi wa timu hiyo, Jamila Hassan, Wema aliwaambia wana-UWT hao wa Kibaha Vijijini kwamba, timu yao ipo kambini kwa muda mrefu na kwamba wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema kuwa wanashiriki Ligi Kuu ya wanawake inayoshirikisha timu 12 kutoka mikoa mbalimbali, ambapo katika kinyang'anyiro hicho pamoja na kupambana kuuwakilisha Mkoa wa Pwani, wanakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba wanahitaji ushirikiano wa hali ya juu.

"Tulivyosikia Mama zetu mpo hapa kwa ajili ya kikao cha kikazi, nasi watoto wenu tukaona tutumie fursa hii kuja kuwataka muungane nasi kwa hali na mali katika ushiriki wetu, kwani tunawawakilisha wanawake wote kuanzia hapa Mlandizi na Mkoa kwa ujumla," alisema Wema.

Kwa upande wake Jamila alisema kuwa ligi hiyo yenye ushindani wa hali ya juu, pamoja na kupambana kwao lakini wanakabiliwa na ukata wa kifedha, hivyo kuwaomba wana-UWT hao na wapenda michezo popote walipo wawaunge mkono katika hilo.

"Ligi ya msimu huu yenye timu 12 inayochezwa nyumbani na ugenini, imekuwa na ushindani wa hali ya juu, na kwamba tumecheza mechi 4, tumeshinda moja, tumepoteza tatu, lakini tunawaahidi tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi," alisema Jamila.

Mmoja wa wana-UWT hao Salha Adinani amewapongeza kwa ushiriki wao, na kwamba kikubwa wanatakiwa kuendelea kupambana katika ushiriki huo, huku akiwaomba wasichana kujitambua katika mavazi.

Sunday, December 22, 2019

VULU AMSHUKURU RAIS MAGUFULI.

 Na Omary Mngindo, Kibiti

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa namna anavyoitekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vulu ametoa kauli hiyo akiwa ziarani katika wilaya za Kibiti, Kisarawe na Kibaha Mji, akihudhuria Mabaraza ya Jumuia ya Wanawake (UWT- CCM) yaliyofanyika kwenye wilaya hizo.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, imedhamiria kuwakomboa wananchi kwa kujenga hospitali mpya kila wilaya, ujenzi wa vituo vya afya, zahanati ikiwemo ununuzi wa ndege na miundombinu ya umeme, barabara sanjali na usafiri wa reli na bahari.

Akiwa Kibiti kwenye siku yake ya kwanza ya ziara hiyo, Vulu akizungumza na wana-UWT hao alisema kuwa Rais Magufuli amezifanyia kazi sekta zote, huku akishukuru zaidi sekta ya afya inayolenga kuhakikisha wanaanchi wananufaika na huduma hiyo.

"Rais wetu amefanya mambo mengi makubwa na anaendelea na juhudi hizo, niwaombe wana-UWT wa Kibiti na wilaya zote tumuunge mkono katika harakati hizo za kimaendeleo anazozitekeleza, kwa fedha zetu za ndani" alisema Vulu.

Aidha amekabidhi kipimo cha sukari na presha kwenye Kituo cha afya Kibiti, huku akimshukuru Mbunge wa Jimbo hilo Ally Ungando, Madiwani, Mkuu wa wilaya na viongozi wote sanjali na wananchi katika kujiletea maendeleo.

Akiwa Kisarawe alizungumza na wana-UWT hao kisha kuwakabidhi boksi za karatasi (rimu) kwa ajili ya matumizi ya Jumuiya zote pamoja na chama ikiwa na lengo la kuboresha utendajikazi kwa wana-CCM hao, huku akimshukuru mbunge Alhaj Suleiman Jafo kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya.


Juzi alikuwa Kibaha Mji, ambapo Vulu aliwapongeza wana-Jumuiya kwa kufanikisha ushindi serikali za mitaa, huku akimpongeza mbunge wa Jimbo Silvestry Koka kwa kazi anayoifanya akishirikiana na Mkuu wa wilaya, Madiwani na ofisi ya Mkurugenzi kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mji Judith Mluge alimpongeza Vulu na wabunge wote wa Viti Maalumu kwa namna wanavyoshirikiana katika kuiendeleza Jumuiya hiyo.

Baadhi ya wenyeviti wa UWT kata zinazounda wilaya ya Kibaha mji
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, (mwenye kilemba cha kijani) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa jumuiya ya wanawake Kibaha mji muda mfupi baada ya kuzungumza na kukabidhi boksi za karatasi

PICHA ZOTE NA OMARY MNGINDO.