Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akikagua shamba la mahindi
wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro alipotembelea Taasisi ya
Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
............................................
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga, 24 Novemba
2018 ametangaza kiama kwa wafanyabiashara wa mbegu nchini wanaouza Mbegu feki
zilizopigwa marufuku na serikali.
Amewataka wafanyabiashara wote wa mbegu ambao
wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa kuwauzia wakulima mbegu feki zilizopigwa
marufuku na serikali kuacha haraka iwezekanavyo kwani serikali itawachukulia
hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo ya serikali.
Ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Morogoro
ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa
Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi iliyopewa jukumu na serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania la usajili wa wafanyabiashara wa mbegu (Seed Dealers).
“Serikali imepokea malalamiko mengi kwa wananchi
kuhusu Ubovu wa mbegu jambo ambalo limepelekea kwa kiasi kikubwa kuwa na mavuno
kidogo pasina kukidhi matakwa ya wakulima wetu nchini” Alikaririwa Mhe Hasunga
Waziri huyo pia ameiagiza Taasisi ya udhibiti
Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kutimiza majukumu yao kwa kuwabaini
wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya serikali pamoja na taratibu na sheria za
nchi.
“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi
kuhusu mbegu feki jambo hili serikali haiwezi kukubaliana nalo hivyo TOSCI
wanapaswa kusimamia kwa weledi ukaguzi na usajili wa Mbegu bora, pia ni lazima
kuwabaini wasambazaji feki wa mbegu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi
yao” Alisisitiza Mhe Hasunga
Alisema Wizara ya Kilimo imepewa jukumu mahususi
la kuhakikisha sekta ya kilimo inaimarika kwa usimamizi madhubuti wa sera,
kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali hivyo kunapokuwa na kelele za wananchi
kuhusu mbegu feki ni dhahiri kuwa Taasisi zenye jukumu hilo hazitekelezi kazi
yake kwa weledi.
Mhe Hasunga alieleza kuwa serikali imejipanga
kuhakikisha kuwa inaongeza thamani ya mazao yote yanayozalishwa nchini,
sambamba na kutafuta masoko mazuri.
Vilevile, ameitaja Wizara ya Kilimo kuwa ina
wataalamu wengi hivyo unaandaliwa mfumo mzuri wa kuwaunganisha watalaamu hao
ili kujadili kwa pamoja namna ambavyo kilimo kinaweza kubadilika kutoka kilimo
cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara ili kutoa malighafi za kutosha
zitakazohuisha serikali ya viwanda.
No comments:
Post a Comment