Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi
....................................................
Na Grace Semfuko-MAELEZO
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi
amewataka waandishi wa habari kutumia haki na wajibu wao katika kulinda maadili
yao ya uandishi na kutotumia taaluma yao kukejeli na kuchafua
watu wengine
Amesema Sheria mpya namba 12 ya mwaka 2016 ya
huduma za vyombo vya habari kifungu cha 7 ingawa inawapa Waandishi wa
Habari kukusanya,kuhariri na kusambaza habari lakini haiwapi fursa waandishi
hao kuandika habari ambazo zinachafua wengine.
Dkt Abbasi aliyasema hayo katika mahojiano na kipindi
cha Hallow Tanzania
kinachorushwa na Radio Uhuru ya Jijini Dar Es Salaam alipokuwa akijibu maswali
ya wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali Nchini.
“Sheria Mpya ya Habari inawapa fursa Waandishi
kufanya kazi zao za kukusanya,kuhariri na kusambaza habari,sheria hii
haijamnyima Mwandishi wa Habari kupata habari, lakini pia haijatoa fursa za
kusambaza habari za kukejeli na kuchafua wengine, sheria itachukua nafasi yake
kwa atakaebainika kufanya hivyo” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa
Serikali.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi
wa Rais Magufuli kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilichukuliwa hatua
za kisheria ikiwa ni sehemu ya kulinda maadili ya uandishi wa habari na
kuvitaka vyombo vingine kuendelea kuheshimu,kulinda na kutetea maslahi ya
Taifa.
Akihojiwa na Mtangazaji wa kipindi hicho Aggrey
Manzi kuhusiana na baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii katika
kuchafua wengine, Dkt Abbasi alisema sio sahihi kutumia mitandao hiyo katika
kuona wengine hawafai, bali mitandao itumike kutangaza habari za Maendeleo.
Kuhusu wanaobeza Maendeleo ya nchi yanayofanywa na
Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli
swali lililoulizwa na Mkuu wa Vipindi wa Radio hiyo Bw. Abdallah Hussein
,Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi alisema Serikali itaendelea kufanya
Maendeleo na kwamba wanaobeza hawazuii utekelezaji huo
“Walisema hakuna ndege, ziliponunuliwa pia
walisema kuwa nani atapanda, wakasema hakuna miundombinu ya barabara inajengwa
bado wanasema, pia daraja la Mfugale limejengwa, Mradi Mkubwa wa umeme wa
Stiglers Gorge unajengwa, Reli ya Kisasa ya standard Gauge inajengwa lakini
bado wanasema, waache waseme tu, hawatuzuii kufanya miradi ya Maendeleo kwa
ajili ya wananchi”
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa uchumi kwa wananchi
mmoja mmoja swali lililoulizwa kwa njia ya simu na Abdallah Athumani Mkazi wa
Chalinze Dkt Abbasi alisema ukuaji wa uchumi unatokana na kuimarisha miradi ya
Maendeleo na kwamba wakazi wanaponufaika na miradi hiyo uchumi unakua kwa mtu
mmpja mmoja.
“Unapoenda kutibiwa kwa gharama nafuu katika
Hospitali ambazo zimejengwa na Serikali unakuwa umehifadhi fedha zako ambazo
zitatumiwa kwa matumizi mengine hii ina maana umeepukana na matumizi makubwa ya
gharama za hospitali, tunaposema elimu bure ina maana Mzazi halipii gharama za
elimu na fedha hizo zinafanya kazi nyingine, kwa ujumla uchumi umekua kwa nchi
na kwa mtu mmoja mmoja” alisema Dkt Hassan Abbasi Msemaji Mkuu wa Serikali.
No comments:
Post a Comment