Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar
es Salaam (DAWASA) imefanikiwa kuvutia mamia ya Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
kuomba kurejeshewa huduma ya maji safi baada ya huduma hiyo kusitishwa hapo
awali kutokana na wateja hao kushindwa kulipa madeni ya ankara za maji
kwa kipindi kilichopita.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa
Mamlaka hiyo Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa wananchi wote waliokatiwa
maji kwa muda mrefu kufika katika Ofisi za DAWASA zilizopo katika maeneo
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Viunga vyake pamoja na Kibaha na
Bagamoyo Mkoani Pwani ili taratibu za kuwarejeshea maji zifanyike.
Akizungumzia lengo la Mamlaka hiyo
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa ni kuhakikisha kuwa inaongeza wateja na
pia kuwarejesha wale waliokatiwa maji kwa muda mrefu baada ya kushindwa kulipa
bili zao ambapo sasa wataingia makubaliano maalum na Mamlaka hiyo
yatakayowawezesha kupata huduma ya maji na kuendelea kulipa deni kidogo
kidogo kulingana na makubaliano hadi watakapomaliza madeni yao.
Hatua zinazochukuliwa na Mamlaka hiyo
katika kuboresha huduma zake ni pamoja na kuvutia wateja wapya na kurejesha
wale waliokatiwa maji kwa muda mrefu.
Sehemu ya Taarifa ya Mamlaka hiyo
kupitia mtandao wake wa kijamii wa Tweeter inasema kuwa wananchi
wameonesha mwitikio mkubwa katika maeneo yote yanayohudumiwa na DAWASA hasa kwa
kuwasilisha maombi ya kurejeshewa huduma hiyo.
“ Kutoka mkoa wa Kinondoni wateja
zaidi ya 50 wamejitokeza kuomba kurejeshewa huduma ya maji safi na salama hivyo
ni mwanzo mzuri kutokana na mwitikio huu ambao umeonesha wazi kuwa wananchi
wanaunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha wanafikiwa na huduma bora”;
inasisitiza sehemu ya taarifa ya Mamlaka hiyo.
Hatua nyingine zinazochukuliwa
na Mamlaka hiyo ni pamoja na kudhibiti mivujo ya maji, kufikisha huduma ya maji
maeneo ya pembezoni na pia kuhakikisha kuwa maeneo ya viwanda yanafikiwa na
huduma hiyo ili kuchochea uchumi wa viwanda.
DAWASA imekuwa ikitekeleza miradi
yakimkakati inayolenga kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma ya
majisafi na salama katika Jiji la Dar es Salaam na Pwani tangu Mamlaka hiyo
ilipoundwa upya baada kuvunjwa kwa DAWASCO hivi karibuni na majukumu yake
kuhamishiwa DAWASA.
No comments:
Post a Comment