Friday, March 27, 2020

MWANDISHI WA HABARI, ASHA MUHAJI AZIKWA DAR.

 Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa msemaji wa Simba SC na Mwandishi mkongwe wa habari za Michezo nchini,Marehemu Asha Muhaji ukipelekwa kwenye gari maalum tayari kuelekea kumhifadhi katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya Mwinyimkuu,Magomeni jijini Dar.
......................................


Watu kadhaa wakiwemo waandishi wa habari wa kada mbalimbali na wanamichezo wamejitokeza kwa wingi katika mazishi ya aliyekuwa Mwandishi wa habari nguli za michezo Asha Muhaji (50) ambaye amezikwa katika makaburi ya Mwinyimkuu Magomeni jijini Dar es Salaam.


Katika mazishi ya marehemu Asha, viongozi wa vilabu mbalimbali na wadau wa soka wameeleza kuwa kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya Michezo na sekta ya habari hasa za Michezo kwani enzi za uhai wake wake Asha alikuwa Mwandishi mahiri wa Michezo na alikuwa mfano kwa wengine.

Kabla ya mwili wake kupelekwa kwenye makaburi hayo kwa ajili ya kupumzishwa, msiba ulikuwa nyumbani kwao Kijitonyama, Mtaa wa Mabatini jijini  Dar s Salaam, na baada ya mwili wake kuondolewa nyumbani hapo wadau walipata nafasi ya kutoa salamu zao.

Baadhi ya waombolezaji waliohudhuria msiba wa Asha Muhaji ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Wallace Karia na Katibu wake, Wilfred Kidau, Msemaji wa Simba SC, Haji Manara, Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire,  wachezaji na wadau mbalimbali.

Akizungumza msibani hapo Rais wa TFF Karia amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Asha Muhaji na kwamba enzi za uhai wake ametoa mchango mkubwa kwa TFF katika kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua katika soka huku akieleza namna ambavyo alijitoa kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘ Taifa Stars’

“Tumepoteza mtu kwenye michezo, ila rai yetu tunayo nafasi ya kuendeleza yale mema ambayo amefafanua kwa maendeleo ya soka letu.
 

Wakati huo huo Kocha Msaidizi wa Klabu ya Simba na Mwalimu wa Soka nchini Suleiman  Matola amesema ni pigo kubwa na kwamba yeye amebahatika kufanya naye kazi kwa nyakati tofauti hasa kwa kuzingatia kuna wakati alikuwa naye Simba Simba akiwa Mwalimu na Asha Muhaji akiwa msemaji wa Klabu hiyo.

Msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema yeye anafahamu uwezo mkubwa aliokuwa nao Asha Muhaji enzi za uhai wake katika eneo la uandishi wa habari za michezo na kwamba mchango wake katika kuhakikisha eneo la michezo linasonga mbele nchini Tanzania hautasahaulika huku akieleza kuwa Asha alikuwa ni Mwandishi ambaye muda wowote aliohitajika kufanya kazi yake alikuwa tayari na sio   miongoni mwa waandishi ambao wamekuwa na kasumba ya kuomba fedha kwa watoa taarifa.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau,  kwa upande wake ameeleza namna ambavyo alikuwa akipata ushirikiano wa  kutosha kutoka kwa Asha Muhaji na kwamba ni moja ya waandishi wa habari za Michezo ambaye amejitoa kwa sehemu kubwa  kufanikisha timu ya taifa inafanya vema katika medani ya soka.

Mdau mwingine wa michezo nchini kutoka Jeshi la Wananchi  wa Tanzania( JWTZ) Luteni Suleiman Semunyu amesema  kuwa Asha Muhaji enzi za uhai wake alihakikisha anatumia taaluma yake ya uandishi wa habari za Michezo kuandika habari za aina mbalimbali za michezo ikiwemo ile ambayo haina umaarufu mkubwa.

Amesema kuwa Asha Muhaji enzi za uhai wake hakuwa akiandika habari za mpira wa miguu bali alihakikisha anaandika na habari za Michezo mingine kama Gofu na tenisi.

”Ametangulia mbele za haki lakini ukweli mchango wake katika medani ya michezo tutaendelea kuukumbuka, kwetu sisi kila tulipomuhitaji alikuja na pale aliposhindwa alikuwa anatuletea Mwandishi mwingine, aliaminiwa kwenye kupika waandishi mahiri wa habari za Michezo.”


Jeneze lenye Mwili wa Marehemu Asha Muhaji ukiswaliwa nyumbani kwao  Kijitonyama,Jijini Dar kabla ya kumpumzisha kwenye nyumba yake Milele jioni ya leo katika Makaburi ya Mwinyimkuu,Magomeni jijini Dar es Salaam.


Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa msemaji wa Simba SC na Mwandishi mkongwe wa habari za Michezo nchini,Marehemu Asha Muhaji likipakizwa kwenye gari maalum tayari kuelekea kumhifadhi kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni jijini Dar es salaam.

Baadhi ya watu mbalimbali wakishiriki mazishi ya aliyekuwa Msemaji wa Simba SC na Mwandishi mkongwe wa habari za Michezo nchini,Asha Muhaji



 Rais wa TFF Wallace Karia (wa pili kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau (wa kwanza kulia) wakijadiliana jambo na baadhi ya Wadau wa Michezo,walipofika kutoka salamu za polenyumbani kwa familia ya Marehemu Asha Muhaji,ambaye amezikwa leo makaburi ya Mwinyimkuu,Magomeni jijini Dar es salaam.

Msemaji na Mhamasishaji maarufu wa Simba SC akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Uongozi wa Timu hiyo pamoja na Wapenzi wa Klabu hiyo nyumbani kwa Marehemu jioni ya leo kabla ya maziko kufanyika katika makabuli ya Mwinyimkuu Magomeni,Jijini Dar es salaam.

Ndugu,jamaa na Marafiki wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa marehemu Asha Muhaji wakiomboleza jioni ya leo kabla ya Maziko kufanyika.

Wadau mbalimbali wakishiriki ibada ya mazishi nyumbani kwa Marehemu Asha Muhaji,maeneo ya Kijitonyama,jijini Dar es Salaam leo.Marehemu amezikwa jioni ya leo katika makaburi ya Mwinyimkuu,Magomeni jijini Dar es Salaam.