Tuesday, November 13, 2018

AMANA BANK, PIL WAZINDUA MIKOPO YA VIWANJA KWA WATEJA WAO.

 Mkuu wa Kitengo cha Biashara Amana Bank, Munir Rajabu akimkabidhi zawadi Mteja wao Aisha Sfana ambae amekamilisha mkopo wake wa kiwanja katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya Amana Bank jijini Dar es Salaam, anaeshuhudia katikati ni  Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado. 

  Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado, akimkabidhi hati ya kiwanja, Aisha Sfana mara baada ya kukamilisha mkopo wake Amana Bank, kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara Amana Bank, Munir Rajabu
 Mkuu wa Kitengo cha Biashara Amana Bank, Munir Rajabu, akizungumza na waandishi wa Habari katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Amana Bank Jijini Dar es Salaam, kulia ni Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado.
..................................... 

Amana Bank Ltd. kwa  kushirikiana na Property International Ltd (PIL) wanaadhimisha miaka mitatu ya ushirikiano wa kibiashara kati yao huku wakiwa wamefanikiwa kuwawezesha wateja wao zaidi ya 300 kumiliki viwanja kwa njia ya mikopo katika maeneo mbalimbali ambayo PIL imepima viwanja.

Wakizungumza katika Makao Makuu ya Amana Bank jijini Dar es Salaam, kwenye hafla fupi ya kuwakabidhi hati za viwanja wateja waliofanikiwa kukamilisha mikopo yao, Maafisa wa Amana Bank Ltd. na Property International Ltd, walisema wanayo furaha na wanajivunia ushirikiano wao ambao umewawezesha watanzania wa hali zote kumiliki viwanja.

Munir Rajabu ni Mkuu wa kitengo cha Biashara kutoka Amana Bank Ltd. amesema Amana Bank siku zote inabuni mbinu na njia rahisi za kuwawezesha wateja wao kumiliki vitu mbalimbali ikiwemo Biashara, Nyumba, Magari, Viwanja NK.

Munir alisema kuwa, katika huduma ya kuwakopesha viwanja wateja wao, Amana Bnak imekuwa ikishirikiana na Property International Ltd ambao ni wataalamu wa upimaji na umiliki wa viwanja na hivyo kurahisisha mikopo ya viwanja kupitia Benki hiyo.

Alisema wateja wanaokopeshwa viwanja bila ya riba sio tu wanafaidika na viwanja, bali wanafaidika kwa kumiliki viwanja vyenye hati ambavyo ni dhamana ya kukopa vitu vingine vitakavyowaletea maendeleo katika maisha yao.

Aliongeza kwa kusema kuwa, hiyo ni njia rahisi kwa watanzania kumiliki viwanja ikiwa ni daraja la kufikia malengo ya kibiashara na kimaendeleo kwa kujenga misngi ya uaminifu katika marejesho ya mikopo hiyo.

Aidha, aliendelea kusema kuwa, kwa namna ambavyo, Amana Bank inavyowajali wateja wake, imeamua kuongeza muda wa malipo kutoka mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu na kupunguza faida kutoka asilimia 14 hadi asilimia 12 kwa mwaka, jambo ambalo limewavutia wateja wengi na kujitokeza kuomba mikopo hiyo ya viwanja.

Munir Alifafanua kuwa, katika mkopo huo wa kumiliki viwanja, mteja anatakiwa kutanguliza asilimia ishirini ya thamani ya kiwanja alichochagua kama malipo ya awali na kuendelea kulipa kiasi kilichobaki katika kipindi kisichozidi miaka mitatu.

Alisisitiza kuwa, Amana Bank ni Benki pekee hapa nchini inayofuata sheria ya kiislamu hivyo mikopo hiyo ya viwanja pia inazingatia misingi ya sheria za kiislamu licha ya kuwa wakopaji ni wateja wa dini tofauti na hata wasiokuwa na dini.

Alisema katika sheria ya kiislamu imeruhusiwa kufanya biashara na imeharamishwa riba, kwa kulizingatia hilo Amana Bank tayari inavyo vitu inamiliki na kisha kuwakopesha wateja wake kwa kulipa kidogo kidogo kama inavyofanya kwenye viwanja kwa kushirikiana na (PIL) 

Mkuu huyo wa kitengo cha Biashara alitumia nafasi hiyo keleza kuwa, katika wiki ya huduma kwa wateja, wateja wa Amana Bank, watapata fursa ya kununua viwanja kwa punguzo maalum la bei ambapo atakuwepo mwakilishi wa (PIL) katika kipindi chote cha wiki ya huduma kwa wateja katika matawi yote ya Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho cha wiki ya huduma kwa wateja, Munir alitoa wito kwa wateja wa Amana Bank Ltd. na watanzania kwa ujumla kutembelea matawi ya Amana Bank ili kupata fursa ya kununua viwanja kwa bei ya punguzo.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado alisema anafurahia ushirikiano kati yao na Amana Bank kwakuwa wameweza kuanzisha huduma hiyo rafiki kwa wateja.
"Mpango huo wa mikopo unaotekelezwa na Amana Bank ni mpango ambao una msaada mkubwa kwa mwenye kutaka kumiliki kiwanja". Alisema Obado.
Akielezea kapuni ya PIL, Obado, alisema imeanzishwa Mwezi January 2014 ikiwa inajishughulisha na upimaji wa viwanja katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ili kuwawezesha wanunuzi wa viwanja kununua viwanja vilivyopimwa.

Alisema katika upimaji wao wa viwanja wanazingztia kanuni na sheria za mipango miji ikiwa ni pamoja kuainisha Barabara ili kurahisisha kufika kwenye makazi husika.

Alisema wananchi wengi wamekuwa wakinunua viwanja ambavyo havina hati hivyo PIL imekuja na suluhisho la kupata hati miliki ya Ardhi kwa kusimamia na kushughulikia mpaka mteja anakuwa na kiwanja chenye hati.

Aidha, Bwana Obado alitaja maeneo ambayo tayari PIL imeshapima viwanja ni Kimbiji Sea View Kigamboni, Magodani Mkuranga, Mapinduzi residence, Chekeni Farm Mwasongfa Tundwi, Fukayosi Residence Bagamoyo, The Dar es Salaam Automobile Zone, (DAZ) Riverside Residence, Coco Palms, Royal Palm Estate Mwasonga, African Palm Estate na Dege Residence. 
 
Mkuu wa Kitengo cha Biashara Amana Bank, Munir Rajabu akimkabidhi zawadi Mteja wao Stephano mara baada ya kukabidhiwa hati yake ya kiwanja baada kukamilisha mkopo wake Amana Bank
anaeshuhudia katikati ni  Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado.
     Mkuu wa Kitengo cha Biashara Amana Bank, Munir Rajabu akimkabidhi zawadi Mteja wao Nora Laizer, mara baada ya kukabidhiwa hati yake ya kiwanja baada kukamilisha mkopo wake Amana Bank
anaeshuhudia katikati ni  Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado.


 Hafla hiyo ilipambwa na keki inayoonyesha miaka mitatu ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Amana Bank Ltd. na Property International Ltd.
 Wateja wa Amana Bank na PIL wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya kukamilisha mikopo yao na kukabidhiwa rasmi hati za viwanja vyao, hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Amana Bank Jijini Dar es Salaam, katika picha hizo anaeonekana upande wa kulia ni Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. George Obado. 
    Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Property International Ltd. (PIL) George Obado, akionyesha kipeperushi kinachoelezea huduma zinazotolewa na PIL.
 
Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa, (kulia) akibadilishana mawazo na Meneja wa Tawi la Tandamti, Juma Yamlinga, kushoto, mara baada ya kumaliza hafla hiyo fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Amana Bank.
 Picha ya pamoja kati ya Maafisa wa Amana Bank Ltd, na wale wa Property International Ltd. (PIL) pamoja na wateja wao watatu waliokabidhiwa hati za viwanja vyao Novemba 12, 2018. Shughuli iliyofanyika Makao Makuu ya Amana Bank Jijini Dar es Salaam.

 Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya Habari wakichukua kumbukumbu ya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment