Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga
Na Mathias Canal-Wizara ya kilimo, Mtwara
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa
wizara yake itatekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Dkt John Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa korosho yote inabanguliwa hapa nchini.
Ameyasema hayo jana tarehe 13 Novemba 2018 wakati
akieleza malengo ya ziara yake mkoani Mtwara na Lindi alipokuwa akizungumza na
vyombo vya habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kabla ya
kuanza kukagua maghala ya kuhifadhia korosho.
Hasunga alisema kuwa kuruhusu wafanyabiashara
kubangulia nje ya nchi korosho za wakulima wa Tanzania ajira nyingi zilikuwa
zikipotea huku watanzania wakisalia kuhangaika kutafuta ajira kwani ajira
nyingi zilipelekwa nje ya nchi.
“Baada ya kujiridhisha tumeamua sasa hahutasafirisha
korosho ghafi tunataka korosho yote iwe inachakatwa nchini kwenye viwanda
vyetu, kwa hiyo korosho zote zilizokuwa zinachukuliwa na wafanyabiashara kwenda
kubanguliwa sijui wapi huko tumezuia” Alikaririwa Mhe Hasunga
Alisema kuwa viwanda vya kubangua korosho nchini
vingi vimekufa kwa sababu ya ubadhilifu wa wananchi wachache na baadhi ya
hujuma za watu lakini serikali imedhamiria kuanza kubangua kwenye viwanda
vilivyopo kabla ya hatua za kuanzisha viwanda vingi vya ubanguaji.
“Tunamuwezesha mkulima kwa bei ya shilingi 3300
ili imsaidie kufanya kazi zake zingine ili aweze kuongeza uzalishaji katika
msimu ujao wa mwaka 2018/2019 na kuepuka kushuka kwa uzalishaji” Alisisitiza
Mhe Hasunga
Alisema baada ya kukamilika uhakiki wa maghala
yote ya kuhifadhia korosho serikali itaanza kulipa malipo yote stahiki kwa
wakulima yatakayotolewa na Benki ya kilimo Tanzania (TADB).
“Na tumeshaandaa fedha zao tunataka wakulima
walipwe haraka iwezekanavyo lakini tumeanza kumjali mkulima kwanza halafu
taasisi zingine zinazofaidika na korosho zitafuata” Alisisitiza
Mhe Hasunga amewapongeza wakulima kwa kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito wakati serikali ilipokuwa ikitafuta
ufumbuzi wa zao la korosho.
No comments:
Post a Comment